Timu ya Coastal Union imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Bao la wenyeji lilifungwa na nyota wa kikosi hicho, Gustapha Saimon katika dakika ya 54 ya mchezo na kuihakikishia ushindi wa saba msimu huu baada ya kucheza michezo 27 ikitoa sare tisa na kupoteza 11.
Coastal imeendeleza kiwango kizuri kwani katika michezo mitano iliyopita ya Ligi Kuu Bara, timu hiyo imeshinda mechi tatu na kutoka sare miwili ikishika nafasi ya 10 baada ya kukusanya pointi 30.
Kwa upande wa Mtibwa Sugar hiki ni kipigo cha nne mfululizo kwenye Ligi Kuu Bara huku mara yao ya mwisho kushinda ilikuwa ni ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji Februari 11, mwaka huu.
Huu ni mchezo wa 27 pia kwa Mtibwa na kati ya hiyo imeshinda saba, sare minane na kupoteza 12 ikiwa nafasi ya 11 na pointi 29.
Ushindi huu kwa Coastal ni wa kulipa kisasi kwani katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Novemba 16, mwaka jana, ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro, sasa Coastal wamesogea hadi nafasi ya tisa kwenye msimamo, huku Mtibwa wakishuka hadi nafasi ya 10.