Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Coastal Union yapigishwa kwata na JKU

Coastal Vs JKU.jpeg Coastal Union yapigishwa kwata na JKU

Fri, 12 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Uhondo wa michuano ya Kombe la Kagame 2024 umeendelea mchana huu baada ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union kushindwa kuhimili vishindo vya maafande wa JKU ya Zanzibar kwa kufumuliwa mabao 2-0 katika mechi ya Kundi A, iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.

Huo ulikuwa ni ushindi kwa kwanza kwa JKU ambayo ilianza michuano hiyo kwa kufungwa bao 1-0 na Al Wadi ya Sudan, huku Coastal ikishinda mchezo wa kwanza dhidi ya Dekadaha ya Somalia. Al Wadi na Dekadaha zinatarajiwa kushuka uwanjani saa 10:00 jioni kuumana katika mchezo mwingine wa kundi hilo utakaopigwa hapo hapo KMC.

Katika mchezo uliomalizika muda mchache uliopita, JKU ambayo ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar na wawakilishi wa visiwa hivyo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikipangiwa kuanza kuumana na Pyramids ya Misri na mshindi wa mchezo huo kuumana na mshindi kati ya Azam na APR ya Rwanda, ilipata mabao kila kipindi na kuifanya ivune pointi tatu na kuongoza kundi hilo kwa sasa.

Mbogo Pict Baobab Pict

Bao la kwanza liliwekwa kimiani na Nassor Matta dakika ya 29, lililodumu hadi mapumziko, licha ya nyota wa Coastal kucharuka kutaka kulisawazisha bao hilo na kipindi cha pili Wagosi walishtukizwa kwa kufungwa bao jingine lililokuwa la pili dakika ya 79 kupitia kwa Neva Adeline.

Kwa matokeo hayo JKU inaongoza msimamo kwa kufikisha pointi tatu kama ilizonazo Coastal na Al Wadi isipokuwa inabebwa na mabao mawili iliyonayo, licha ya kufungwa moja pia, ilihali Dekadaha inaburuza mkia ikiwa haina pointi na itakuwa na nafasi ya kujiuliza baadae itakapovaana na Wasudan.

Mara baada ya mechi hiyo ya Al Wadi na Dekadaha, saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, utapigwa mchezo mwingine utakaozikutanisha SC Villa ya Uganda dhidi ya Singida BS za Kundi C, kisha saa 3 usiku itakuwa zamu ya APR itakayoumana na Al Merrikh ya Sudan Kusini.

Kesho kutakuwa na mechi mbili za Kundi B kwa Mabingwa wa Kenya, Gor Mahia itakuwa inajiuliza mbele ya Asas ya Djibouti utakaopigwa saa 3 usiku, lakini mapema Al Hilal ya Sudan itaumana na Reds Arrows ya Zambia iliyowapasua K'Ogalo katika mechi ya raundi ya kwanza uliopigwa juzi uwanjani hapo.

Chanzo: Mwanaspoti