Wakati Coastal Union ikiendelea kuwaaga baadhi ya wachezaji katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu 2023/24, Uongozi wa klabu hiyo ya jijini Tanga umeanza hesabu za kumrejesha aliyekuwa nyota wao, Haji Ugando.
Ugando aliyewahi kuichezea Coastal Union alijiunga na Ruvu Shooting msimu uliomalizika, lakini baada ya timu hiyo kushuka daraja na mkataba wake kumalizika inataka kumrejesha ili akaitumikie msimu ujao. Akizungumzia dili hilo Ugando amesema zipo timu zilizoonyesha nia ya kuhitaji saini yake, lakini kwa sasa anapumzika kabla ya uamuzi.
“Kama ambavyo mashabiki wanatambua nilikuwa majeruhi tangu Aprili, ila namshukuru Mungu nimeanza mazoezi mepesi, hivyo ni matumaini yangu nitarudi nikiwa imara zaidi,” amesema.
Ugando ameongeza kuwa majeraha ya misuli ya paja aliyoyapata kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC yalimrudisha nyuma na kushindwa kuipigania Ruvu.
Coastal ambayo imeachana pia na benchi la ufundi inahitaji kuboresha kikosi baada ya kutangaza kuachana na mastaa 10. Mastaa walioachwa ni Joseph Zziwa, Emery Nimubona, Mahamoud Mroivili, Djibril Naim Olatoundji, Yema Mwamba, Yusuph Jamal, Yusuph Athuman, Juma Mahadhi, William Kisinga na Aboubakar Abbas.