Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Coastal Union inapopitia kifo cha Kiswahili

Coastal Pic Coastal hali haijatulia

Sat, 26 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Hali ya mambo ndani ya klabu ya Coastal Union inatia huruma jahazi linazidi kuzama kuna vurugu nyingi kuliko utulivu kila siku mpya kuna jipya linaibuka ambalo linasikitisha.

Kocha Mkuu wa timu hiyo raia wa Marekani Melis Medo ameachia ngazi akiamua kukaa pembeni baada ya kuona maji yanamzidi kimo timu ikiwa inakosa matokeo lakini vurugu za ndani zikiwa nyingi.

Nilikuwepo pale Uwanja wa CCM mkwakwani wakati Coastal Union wakicheza dhidi ya Yanga wenyeji wakipoteza kwa mabao 2-0.

Kumbuka msimu uliopita tu Coastal wakiwa katika uwanja huohuo waliichapa Yanga mabao 2-1 tena wakionyesha kiwango bora wakitoka nyuma na kuja kushinda.

Msimu huohuo Coastal walifikia hatua mbaya wakicheza play off dhidi ya Pamba kuamua kubaki kwao ligi kuu vinginevyo hali ingekuwa mbaya zaidi kwao.

Mpira wa ‘kiswahili’

Baada ya kufungwa na Yanga, Coastal katika ubora wa akili zao waliona kama Yanga sio kitu ambacho kinakubalika kwao kwamba wamezidiwa, kazi kubwa ilikuwa kumsaka mchawi, nguvu kubwa ilikuwa inaelekezwa kutafuta nani amehujumu timu.

Coastal walishindwa kukubali wala kujifunzwa kwamba Yanga waliyoifunga ilikuwa na utulivu mkubwa wa kujipanga wakianzia katika usajili mzuri na hata makocha wengine na wengi wao wakiingia watu wenye ubora mkubwa.

Hebu jiulize timu ya ligi Kuu inafungwa halafu inaelekeza nguvu katika kisomo cha ‘albadili’ kwamba waliohujumu klabu wapate matatizo.

Mechi ya mwisho kushinda mwamuzi afungiwa

Mchezo wa mwisho Coastal kushinda ilikuwa ni dhidi ya Mbeya City, ilikuwa ni Desemba 24, 2021 katika ushindi ambao ulilalamikiwa sana hasa bao la penalti ambayo ilitolewa kiutata na mwamuzi Ahmeid Arajiga kutoka Manyara ambaye hivi unavyosoma hapa anatumikia kifungo cha soka kufuatia penalti hiyo.

Mechi tano bila ushindi

Baada ya kushinda mechi hiyo kiutata Coastal wamecheza jumla ya mechi tano na hawajashinda hata moja wakianza na Mtibwa Sugar hadi hii ya mwisho dhidi ya Geita Gold hakuna ushindi waliopata.

Kumbuka mechi hizo tano, tatu katika ya hizo walikuwa nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar, Yanga, Namungo na mbili wakiwa ugenini dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold.

Hapa unapata tafsiri kwamba kuna shida ndani ya kikosi chao kuhusu ubora wa timu kujua kipi kinawaumiza na mambo yakiendeshwa kiswahili badala ya utaalam wa mpira.

Makosa ya aina moja

Mabao mengi ambayo Coastal yamekuwa yakiwamaliza yamefungwa kwa krosi hasa mipira ya juu kama kuna watu wa ufundi kuanzia kwa Mkurugenzi wa Ufundi hadi kocha mkuu walitakiwa kujiuliza na kutafuta tiba ya changamoto hizo.

Vurugu za kiuongozi

Kuna vurugu nyingi katika uongozi wa Coastal Union tukumbuke hii ndio klabu ambayo anatoka Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto lakini pia huwezi kuitenganisha na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia ambaye alitokea pale.

Hivu karibuni lilitoka kundi la mashabiki wakiwalaumu viongozi wao wakiona kama hawaisaidii timu yao lakini hatua ya kwanza ambayo ilipaswa kufanyika ni kukutana kisha wakazungumza changamoto zao walizonazo ndani na kupata suluhu.

Kitu kibaya zaidi Coastal imekuwa kama nyumba ya migogoro kumekuwa na makundi mengi sana ambayo yamekuwa yakiivuruga timu hiyo, hata wadhamini wamekuwa wakikimbia kutokana na kukosa afya ya wao kubaki klabu imekuwa na kila mtu msemaji wenye fedha huwa hawapendi vurugu za namna hii.

Kilichobaki sasa ni watu kuamua kufanya kama hisani kama ambavyo wanafanya Bin Slum ambaye ni shabiki wa timu hiyo hawezi kuikimbia, kama kungekuwa na utulivu wangekuja wadhamini wengi zaidi ya GSM na wengine.

Kauli ya Medo inatishia

Sio rahisi sana kuona kocha wa kigeni akizungumzia mambo ya kiswahili lakini maneno ya Medo yanaleta kiza kingine ndani ya Coastal hata kama kocha alifeli kazi yake lakini kama kweli kutakuwa na mambo ya kishirikina sana kuliko utaalam wa kisayansi basi anguko litakuwa kubwa zaidi.

Mnguto asijisahau arudi nyumbani

Tiketi ya Mnguto kuwa Mwenyekiti wa bodi ameipata Coastal Union ambayo sasa inashika nafasi ya 9 kwenye msimamo wa ligi sio mbali sana na mkiani kutokana na mbio za ligi hasa msimu huu kuna haja ya haraka Mnguto hata ikiwezekana Karia warudi nyumbani kutuliza nyumba lakini hasa Mnguto.

Kama Coastal ikishuka Mnguto anapoteza sifa ya kushika kiti alichoshika kama kiongozi anapaswa kurejea na kutafuta salama ya klabu yao hasa wakati huu ambao wanaonekana kama wako sana jijini Dar es Salaam wakiitupa klabu yao.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz