Baada ya ushindi wa mabao 2-1 ilioupata Coastal Union dhidi ya Kagera ugenini, leo Mei 25 itakuwa katika Uwanja wa CCM Mkwakwani mjini Tanga kuikaribisha JKT Tanzania.
JKT Tanzania
Mchezo huo utakaozikutanisha timu hizo ikiwa ni mzunguko wa pili baada ya awali Coastal kuondoka na pointi tatu dhidi ya wanajeshi wa JKT.
Coastal ipo nafasi ya nne na pointi 41 kwenye michezo 28 ikishinda 11, sare nane na kupoteza tisa ikifunga mabao 22 na kuruhusu mabao 19 ikiwa ni miongoni mwa timu zilizoruhusu mabao machache.
Kwa JKT yenyewe ipo nafasi ya 10 na pointi 31, ikishinda sita, kupoteza tisa na sare 13 ikiruhusu jumla ya mabao 28 na kufunga 21.
JKT ikishinda mchezo huo itatoka nafasi ya 10 na kusogea hadi sita ikifikisha pointi 34 huku Coastal ikishinda itaendelea kusalia nafasi ya nne na pointi 43.
Mbali na hilo, hiyo inaweza kuwa nafasi kwa viungo wa timu zote mbili, Daudi Semfuko (Coastal Union) na Danny Lyanga (JKT Tanzania) wenye mabao manne katika ligi kuonyesha uwezo wa kucheka na nyavu.
MBINU ZA MAKOCHA
Kocha wa Coastal mkenya, David Ouma amekuwa akitumia mfumo wa kuzuia akiwatumia mabeki wake wa kati wakati huo huo akishambulia jambo ambalo amefanikiwa hadi sasa kuruhusu mabao mengi.
Kwa JKT, Malale Hamsini amekuwa akicheza kwa kushambulia zaidi jambo linaloigharimu timu hiyo inaposhambuliwa kwa kushtukiza huruhusu mabao.
MAKOCHA
Kocha wa Coastal Union, David Ouma amesema: "Jambo la muhimu wachezaji wote wameingia kwenye falsafa yangu, hivyo ninapotengeneza mpango wa kusaka ushindi wanakuwa wanaelewa nini nahitaji kutoka kwao, katika mechi zilizosalia ni za kutimiza malengo.
"Ingawa wakati mwingine wapo ambao walipata majeraha na kupona, lakini bado kikosi kipo imara, naamini kila mmoja wao atafurahia kumaliza msimu salama."
Kwa upande wa kocha wa JKT Tanzania, Malale Hamsini amesema hawana namna zaidi ya kushinda mechi zilizosalia mbele yao, ili kutoka nafasi ya 10 kupanda juu zaidi.
"Mechi za mwisho zinakwenda kutimiza malengo ya kila timu, kwa upande wetu tupo tayari kupambana, mzunguko wa kwanza tulipoteza kwa bao 1-0, hivyo hatutakubali kufungwa ndani, nje.
WASIKIE WADAU
Kipa wa zamani wa JKT Tanzania, Shaban Dihile amesema: "Mchezo utakuwa mgumu, kutokana na uzoefu wa Coastal kwenye Ligi Kuu, lakini naona JKT ipo vizuri zaidi."
Beki wa zamani wa Coastal Union, George Mbwana amesema anaamini mchezo huo utakuwa mgumu ingawa Coastal ina nafasi kubwa ya kushinda kutokana na msimamo ulivyo, lakini kupambania nafasi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani.