Akiwa kijana mdogo aliyebeba ndoto kubwa kwenye miguu yake, ilihitajika imani ya Nasredine Nabi juu ya kipaji chake ili kuunda neno bahati kwenye kichwa chake.
Ikawa mchana, ikawa usiku ndipo neno bahati likachomoza na nuru.
Ilikuwa ni bahati kwake, bahati ya kwanza kuaminiwa akiwa kijana mdogo, Bahati ya pili alijua anaenda kuvaa nembo inayobeba hisia na mapenzi ya watu wengi, Bahati ya tatu alijua anaenda kuondoka neno umasikini kwenye kamusi ya maisha yake.
Baada ya miguu ya Fiston Mayele kuagwa. hapo ndipo kila kitu kilibadilika, kioo cha kukitazama kilipotea kwenye mboni za Clement Mzize, mbaya zaidi Clement aligeuzwa kuwa kioo kinachotazamwa zaidi, huku hakuna mtu anayejali kuhusu umri wake.
Ninaamini kwenye umri wa Clement Mzize unahitaji mshambuliaji tegemezi wa kumuongoza kijana mdogo. Mbaya zaidi si Konkon wala Guede wamegeuka kuwa kioo kinachoweza kutazamwa vyema na Clement Mzize.
Huenda huu ndio ukawa msimu wake bora Mzize, lakini nyakati njema hazijawahi kuwa rafiki kwake, wananchi wameamua kumbebesha lundo la chuki kwenye kila nafasi anayokosa, hakuna tena anayejali kuhusu umri wake, hakuna mtu tena anayejali kuhusu uzoefu wake mdogo.
Ni msalaba wa Yesu kwenye mabega ya Clement Mzize kwenye umri mdogo.
Wakati Christian Ronaldo anatua Manchester United ilimlazimu kukaa benchi kuwatazama wanaume wakivuja jasho, alikutana na vioo vinavyoweza kutazamika na ukajifunza muda wote. Ilikuwa bahati kwake. Ndio bahati aliyokosa Clement Mzize msimu huu.
Wananchi wameamua kubebesha taji la chuki kwenye vifua vyao, wakiamini kuwa kila nafasi anayokosa ni matokeo ya uzembe. ukweli ni kuwa ni muda wa kusubiri ubora uliojificha ndani ya Clement Mzize. Kila kitu anachokifanya ni funzo kwake, bahati mbaya zaidi wananchi hawana muda wa kusubiri.
Muda ndio rafiki pekee unaoweza kumhukumu Clement Mzize.