Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Clatous Chama, mwanzo wa mwisho wake?

Realclatouschama Clatous Chota Chama.

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Namna nyakati zinavyokwenda kasi. Jumamosi usiku kwa mara nyingine tena Clatous Chotta Chama alitokea katik benchi kwenda kujaribu kuokoa jahazi la Simba ambayo ilikuwa inazihitaji pointi tatu kutoka kwa Waydad Casablanca.

Tayari katika pambano lililopita pale Francis Town, Chama alitokea katika benchi kwenda kuchukua nafasi ya mchezaji yule yule ambaye kwa mara nyingine alikuwa amemsugulisha tena benchi pale Marrakech, Willy Osamba Onana.

Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha ameona nini kwa Onana ambacho kinamtofautisha na Chama kwa kiasi cha kuanza katika mechi mbili za kimataifa za Simba zilizopita? Hatuwezi kujua. Wote tulimuona Onana alivyocheza ovyo pale Botswana lakini bado alifanikiwa kumshawishi Benchikha ampange tena mbele ya Chama.

Mchezaji kutokea benchi katika mechi mbili hauwezi kuwa mwisho wake. Kuna wakati huwa inawatokea wachezaji wanapokuwa wamechoka, au wametoka katika majeraha. Kinachonishangaza ni namna ambavyo mashabiki wa Simba wamekuwa wakiipokea habari hii ya Chama kupigwa benchi. Hawashangai sana.

Kuna yule Chama ambaye kama angepigwa benchi katika mechi hizi muhimu basi kocha angeweza kufungasha virago vyake na viongozi. Sasa hivi kinachoendelea pale Msimbazi ni kama vile mashabiki na viongozi wa Simba wanahafiki uamuzi wa kocha moja kwa moja.

Sio kwamba wanahafiki Onana kucheza, hapana, isipokuwa hawapingi Chama kukaa benchi. Nadhani kuna kutazamana vibaya kati ya mashabiki wa Simba na Chama. Lakini pia kuna kutazamana vibaya kati ya mabosi wa Simba na Chama.

Kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa watani zao, Yanga kiliongeza nyufa katika uhusiano mbovu kati ya Chama na mashabiki wa Simba. Wapo mashabiki wengi ambao wameendelea kumshutumu Chama kwa kucheza ovyo katika pambano hili la watani. Sio la siku zile tu, bali siku zote.

Ukienda katika ukurasa wake binafsi wa mtandao wa Instagram Chama amekuwa akishutumiwa vikali na Wanasimba kuhusu kiwango chake cha siku hizi, hasa pambano la Yanga. Hata akiposti mambo yake binafsi mashabiki wamekuwa wakimshukia kuhusu kiwango chake.

Lakini mashabiki wanaamini Chama anawasumbua na amekuwa na urafiki na baadhi ya vigogo wa watani wao. Mfano ni namna alivyogoma kwenda kambini Uturuki akidai atimiziwe baadhi ya madai yake.

Mshabiki wengi hawakupenda na walimuona kama msaliti. Walitamani kumuona kambini kwanza Uturuki halafu mambo mengine ndio yafuate. Wanaamini moyo wa Chama haupo moja kwa moja katika klabu ya Simba.

Haishangazi kuona hawasimami nyuma yake pindi Kocha Benchikha anapochukua maamuzi ya kumuweka benchi. Kumbuka ni mashabiki hawahawa ndio waliolipuka kwa hasira wakati kocha aliyepita Robertinho alipomtoa Chama uwanjani katika dakika ya 30 ya pambano lake la kwanza tangu awe kocha wa Simba.

Sasa hivi maisha yamekwenda kasi kiasi mashabiki wa Simba hawahoji tena uamuzi wa Kocha Benchikha kumuweka benchi Chama. nje ya bifu la Chama na mashabiki wa Simba, inadaiwa Kocha Benchikha haliridhishwi na kiwango cha mchezaji huyo.

Haamini kama ana msaada mkubwa katika timu kutokana na kucheza taratibu huku akiwa hana msada mkubwa wakati timu inapokuwa haina mpira. Benchikha ni mkali na anataka wachezaji wanaojituma zaidi huku akiwa haangalii sana historia ya wachezaji waliofanya makubwa klabuni.

Ndio maana Chama na swahiba wake, Jose Luis Miqussone wanasugua benchi kwa sasa.

Mpira uko kwa Chama mwenyewe. Ana muda wa kumthibitishia kocha kwamba anamfikiria tofauti. Lakini ana muda pia wa kuwathibitishia mashabiki kwamba yeye ndiye mfalme halisi ndani ya Simba. Pambano dhidi ya Jwaneng nusura aipatie Simba bao kama mpira wake usingegonga mwamba. Kama mpira ungeingia katika nyavu labda ingesaidia kutibu ugonjwa wa uhusiano mbovu kati yake na mashabiki.

Kama hali ikiendelea kuwa hivi sioni kama Chama atakuwa na muda mrefu Simba. Tatizo kubwa kwa upande wa uongozi ni kwamba wameshindwa kupunguza umuhimu wa Chama klabuni kwa kuleta wachezaji wa aina ya Pacome Zouzoua ambao wangeweza kuifanya vema kazi yake.

Matokeo yake Chama ameendelea kuwa mmoja tu ndani ya Simba. Ni uamuzi wake kuona kwamba anaweza kubakia Simba. kwa kipaji chake siku moja tu, tena ndani ya dakika chache za mechi anaweza kubadili mawazo ya Wanasimba wote. Ni maamuzi yake.

Lakini kama akiweka kinyongo na kuendelea kuchukia uamuzi wa kocha huku akiwa hafanyi jitihada zozote basi ni wazi kwamba mwisho wake utakuwa umekaribia Simba. Siku yoyote ambayo watampata mchezaji au wachezaji wa maana katika nafasi yake wanaweza kumuonyesha mlango wa kutokea.

Chama aelewe tu kwamba yupo katika nyakati ambazo mashabiki hawapo nyuma yake. Kama utawauliza watu wa Simba ni mchezaji gani muhimu zaidi kwao sasa hivi wanaweza kukutajia hata Kibu Dennis mbele ya Chama ingawa wanafahamu Chama ana kipaji kikubwa.

Mchezaji ukiwa unapitia nyakati kama hizi unahitaji uamuzi mgumu. Hasa kama uliwahi kuiweka timu mkononi. Kitu kibaya zaidi ni kwamba watu wa Simba wanaonekana kumwamini Benchikha kuliko mchezaji mwenyewe na ndio maana hawajahoji uamuzi wake.

Kasheshe itakuja pale mwishoni mwa msimu ambapo kocha anaweza kubaki na kuchukua uamuzi mzito dhidi ya baadhi ya wachezaji.

Nasikia jambo hili lipo na lipo njiani kutimia. Benchikha ameshahakikishiwa kwamba anaweza kufanya uamuzi wa kuachana na baadhi ya mastaa. Hata uongozi wenyewe nasikia nao unafikiria kuchukua uamuzi mzito kwa baadhi ya wachezaji wakubwa ndani ya timu.

Wamechoka na namna msimu ulivyokwenda na wanaamini watani wao wanasonga mbele vizuri kwa sababu wana tabia ya kuchukua uamuzi mgumu kwa baadhi ya wachezaji. kumbuka kilichowakuta Mkoko Tonombe, Yannick Bangala na Djuma Shaaban.

Chanzo: Mwanaspoti