Kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama huwenda akawa ni miongoni mwa Usajili Bora kabisa kuwahi kufanywa na Klabu hiyo ya Msimbazi hasa kutokana na kiwango chake uwanjani sanjari na mafanikio binafsi anayopata nyota huyo.
Takwimu zinambeba sana ‘Mwamba wa Lusaka’ kutokana na kile anachokifanya uwanjani ambacho kimekuwa na matokeo chanya kwa Simba SC.
Msimu huu wa mwaka 2022/23, Chama ameendelea kuwa kinara wa pasi za mwisho zilizo zalisha magoli (assit) akiwa amefikisha 14.
Mbali na hilo mpaka sasa, Clatous Chama anashika nafasi ya pili NBC Premier League msimu huu kuhusika kwenye ushiriki wa magoli (Goal Involvements ) akifikisha 17 nyuma ya Ntibazonkiza mwenye 19.
Hapa tuna mzungumzia, Chama ambaye Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) linamtambua kama Mchezaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa mechi ya hatua ya Makundi ya mzunguko wa nne (4).
CAF pia ilimtaja kiungo huyo raia wa Zambia kwenye orodha ya Kikosi Bora cha wiki kwa Klabu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Msimu wa 2019/2020, Chama alitangazwa kama Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya VPL na kutwaa tuzo hiyo akiwashinda Bakari Nondo Mwamnyeto akiwa Costal Union na Nicolas Wadada wa Azam FC.
Usiku huo wa msimu 2019/2020, Clatous Chama alishinda pia tuzo ya Kiungo Bora wa mwaka akiwashinda Lucas Kikoti wa Namungo na Mapinduzi Balama kutoka Yanga.
Chama pia alikuwa miongoni mwa wachezaji walio tajwa kuunda Kikosi Bora cha mwaka. Huo msimu alimaliza akiwa kinara wa ‘assist’ baada ya kufikisha 10.
Aliondoka na tuzo ya Mchezaji Bora wa Michuano ya Kombe la Azam Sports Federation Cup na ya mdhamini wao mkuu kwa wakati huo SportPesa.