Nyota wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Al Nassr ya Saudi Arabia, Clara Luvanga ameendelea kuwa moto katika Ligi Kuu ya Wanawake na ndiye kinara wa kutupia mabao akiwa nayo 10.
Luvanga ambaye amecheza mechi 10 hadi sasa amefikisha idadi hiyo ya mabao akiwaacha nyota wenzake wa ligi hiyo, Ibtisam Jraidi, Oriana Altuve, Shilhan Nooraldin wenye mabao tisa na Linah Boussaha mwenye mabao nane huku akifichua siri ya kufanya hivyo ni juhudi binafsi.
Clara ameliambia Mwanaspoti sababu ya kuwa bora muda wote na kufunga ni kutokana na kupambana na juhudi anazozionesha uwanjani.
"Ligi ya huku ni ngumu na hadi kocha anakuamini na kukupa nafasi ni wazi ameona uwezo wako, hivyo ili kumthibitishia naweza kucheka na nyavu, ninafanya juhudi za ziada uwanja wa mazoezi na ndio maana nafunga sana," alisema Clara ambaye kwa sasa amerudi nchini kwa mapumziko.
Straika huyo wa zamani wa Yanga pamoja na kufunga lakini ameisaidia Al Nassr kuongoza kwenye msimamo wa ligi na pointi 28.
Uwezo wa Clara umekuwa tishio nchini humo kiasi cha kuwania tuzo za mchezaji bora wa mwezi mara tatu mfululizo, mwezi Desemba, Januari na Februari kwa kupigiwa kura mtandaoni ambazo hakuwahi kushinda lakini akichukua tuzo ya goli bora.
Ukiachana na Clara yupo pia Mtanzania mwenzake, Enekia Lunyamila ambaye timu yake Eastern Flames iko nafasi ya saba na pointi nne kwenye msimamo na yeye akiwa kwenye orodha ya wafungaji akifunga mabao sita kwenye mechi 10.