Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

City: Nani ashuke? Subirini muone!

Mbeya City Kushuka Wachezaji wa kikosi cha Mbeya City

Tue, 18 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Pamoja na kukiri mambo magumu, lakini Mbeya City imesema kushuka daraja kwao haiwezekani huku wakisisitiza katika mechi nne zilizobaki hawaachi kitu wakiwataka mashabiki kuwa na uvumilivu.

City ilianza na kasi ligi kuu msimu huu hadi kufika robo fainali ya kombe la shirikisho (ASFC) ikiwa ni mara ya kwanza kwao lakini kwa sasa imeonekana kuwa na matokeo yasiyoridhisha na kuwafanya mashabiki na wadau wa soka jijini Mbeya kuwa na hofu kwa timu hiyo kushuka daraja.

Hadi sasa timu hiyo yenye rekodi ya kudumu ligi kuu tangu ilipopanda msimu wa 2013/14 ipo nafasi ya 13 kwa pointi 27 na imebakiza mechi nne ikianzia ugenini dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold kisha kurejea nyumbani kuikabili Yanga na KMC na kusubiri hatma yake.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Anthony Mwamlima alisema pamoja na matokeo ya sasa kutokuwa rafiki, lakini haijawakata nguvu na wanamatumaini ya kuendelea kubaki ligi kuu msimu ujao akisema mechi nne zilizobaki watampiga yeyote.

Alisema hawawezi kujiamini kupitiliza kutokana na vita ilivyo akibainisha kuwa wanaendelea kujipanga kuhakikisha wanaanza na ushindi kwenye mechi ijayo dhidi ya Kagera Sugar, Aprili 21 kisha kuwapigia hesabu nzito Geita Gold na kurejea nyumbani na alama sita.

“Ni kweli matokeo si mazuri sana lakini kwa hesabu zetu tunaona dalili njema kwa sababu tumejipanga kutumia vyema michezo iliyobaki kutopoteza pointi yoyote, tunaanza na Kagera na uhakika wa alama tatu upo, kimsingi mashabiki wasiwe na presha City hatushuki daraja,” alisema Mwamlima.

Kwa upande wake kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Richardson Ngy’ondya alisema matokeo ya Namungo ndio yaliharibu upepo wao licha ya kupambana kusaka alama tatu na kwamba kwa sasa wanajipanga upya na michezo ijayo na kuahidi City itafanya vizuri na kubaki salama.

“Malengo yetu ni kubaki ligi kuu haijalishi upepo uliopo hivi sasa na hatuwezi kukata tama kwa sababu ligi iko hivyo na hadi sasa hakuna ambaye ameshajihakikishia kubaki ukiachana na zile nne za juu, tunaamini tutafikia malengo,” alisema nyota huyo.

Chanzo: Mwanaspoti