Juzi Singida FG ilianza vyema mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuichapa Future ya Misri bao 1-0 ikiwa ni mechi ya kwanza ya hatua ya kwanza huku kiungo wake Mnigeria, Morice Chukwu akisema kazi bado.
Singida ambayo inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza ikiwa ni msimu wake wa pili tangu ipande Ligi Kuu, ilicheza mchezo huo katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi na kupata bao hilo dakika ya 72 lakini bado ina kazi ya kufanya kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa Cairo, Misri.
Akizungumza nasi, kiungo huyo alisema mchezo huo ulikuwa mgumu kipindi cha kwanza na kuwafanya wachezaji wote kuumiza vichwa wakati wa mapumziko na kubadilisha mfumo kwa kushambulia ili kupata ushindi.
Aidha alisema matokeo waliyoyapata hayajawa makubwa kama ilivyofikiriwa kwani inafahamika katika uwanja wa nyumbani lazima ushinde mabao mengi.
Alisema wapinzani wao walikuwa na kikosi kizuri na walipania kupata ushindi na hivyo walishambulia na kukaba muda mwingi ili mchezo wa marudiano wasiwe na kazi kubwa .
“Viungo wa timu pinzani walitupa shida ila tumesoma mbinu zao na mchezo wa marudiano tunakwenda kufanya kazi moja tu kuzuia kile tulichokipata kwani tunahitaji sana kuingia makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ili kuandika historia mpya.
“Tunajua watataka kutushambulia mwanzo mwisho wakiwa kwao.
“Tunakwenda Misri kulinda kile tulichokipata hapa na malengo yetu ni kucheza kimataifa, hivyo hatutatumia nafasi tuliyopewa vibaya na tunakwenda kujijenga na kurekebisha makosa yote tuliyoyafanya tutawashangaza Misri.”