Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chukwu: Nimekuja kupiga kazi sio kuuza sura

Morice Chukwuu Kiungo mpya wa Singida Fountain Gate kutoka Rivers United ya Nigeria, Morice Chukwu

Mon, 28 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kiungo mpya wa Singida Fountain Gate kutoka Rivers United ya Nigeria, Morice Chukwu mwenye umri wa miaka 21 ameanza kuwasha moto katika kikosi hicho ikiwa ni miezi michache tangu timu yake ya zamani kutolewa na Yanga kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa jumla ya mabao 2-0.

Morice anaetumika kama kiungo mkabaji na mchezeshaji, rasmi msimu huu ameanza kutumika ndani ya kikosi cha Singida akiwa ni miongoni mwa wachezaji wapya wa kigeni waliosajiliwa.

Chukwu aliyehusishwa na timu tofauti tofauti ikiwemo Simba na Yanga kabla ya kujiunga na kikosi cha Singida alionekana zaidi wakati wa mashindano ya Kombe la Shirikisho walipokutana na Yanga msimu uliopita.

ILIVYOKUWA

Kiungo huyo anasema wakati alipotoka kwenye mechi ya marudiano ya robo fainali alipokea simu nyingi kutoka timu kadhaa alifurahi zaidi kupokea simu ya Raisi wa Singida na kuongea nae kumwambia malengo yao na ubora aliokuwa nao.

“Simu ya raisi wa timu ilinifanya kujiona wa thamani zaidi lakini kubwa zaidi ni malengo yao ya kutaka kukua zaidi msimu huu mzima Kimataifa na ndani ya Ligi yakinishawishi."

KILICHOMVUTIA SINGIDA

Morice anasema kilichomfanya yeye kuchagua timu hiyo ni kwa sababu ya nafasi nzuri waliomaliza nayo katika msimamo wa Ligi na wanacheza kimataifa ikiwa ni timu ambayo inaonyesha mwanga mzuri wa mafanikio.

Anasema Singida inampa furaha kwani ni timu ambayo ina malengo makubwa na yenye kutamaniwa na kila mchezaji mwenye shauku ya kufika mbali zaidi katika safari yake ya soka.

"Niliichagua Singida kwani ni timu kubwa ambayo inakuwa kwa kasi na kwangu itaniongezea kukua zaidi kwani najua sehemu yoyote yenye viongozi wenye malengo kuna nafasi kubwa ya kukua,"

"Rais wa Singida alinipigia simu baada ya mechi na Yanga na kuniambia kuwa anahitaji huduma yangu msimu ujao kwangu sikuona kama kawaida kwani ulkiuwa ni heshima kubwa na kupewa mipango ulionivutia zaidi," anasema kiungo huyo Morice.

UTOFAUTI WAKE

Wapo wachezaji kutoka Nchini kwao waliokuja kucheza katika Ligi hii na hawakuwa na mafanikio na msimu uliopita waliondolewa,Morica anasema kuhusu hilo kwake iko tofauti kwani anajua kile anachotakiwa kufanya hivyo hana cha kupoteza.

Kiungo huyo anasema ujio wake ni kwajili ya kazi na ndio maana akachagua timu ambayo ataweza kucheza mechi nyingi na ili aweze kuonyesha ubora wake katika kila mechi.

"Waliofanya vibaya hao sio sehemu yangu ila najali kile kilichonileta hapa bila kuangalia historia mbaya za wengine au nzuri kwani kila mtu anautofauti na malengo yake."

MAISHA YA SINGIDA

Morice aliyejiunga na timu hiyo wakiwa kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu anasema kwa muda mfupi aliokaa Arusha amewaona wachezaji wote na Singida ina kikosi chenye furaha na upendo muda wote.

Kiungo huyo anasema kwake haikuwa rahisi kukutana na watu wapya lakini hali ya hewa ya baridi ilikuwa changamoto kubwa ila umoja wa wachezaji ulimfanya kujihisi kama yupo nyumbani.

"Maisha ya Singida kwangu yamekuwa mazuri na ya amani muda mwingi nikitoka mazoezi nakula na kupumzika hivyo hakuna kikubwa zaidi ya familia hii mpya ambayo imenipokea vizuri." anasema Morice.

MANENO YA KOCHA

Morice anasema wakati anaingia kambini alikutana na kocha Hans Pluijm, alimpokea na kumweleza namna alivyofurahi kumuona kikosini kwani ni mchezaji alietamani kuwa nae msimu huu.

Anaendelea kusema kwake ilikuwa ni furaha kukutana nae kwa mara ya kwanza kwani hakutegemea ukarimu na mapokezi ya makubwa kutoka kwa kocha wake huyo mpya ambae hajawahi kufanya nae kazi.

"Mwalimu yoyote anatamani matokeo mazuri ndio maana wanasajili ili kuongeza nguvu hivyo namuelewa sana anaposema kuwa nataka kuniona mbali kwani nafahamu faida yake na ukubwa wake."

MIPANGO MIKALI

Morice ambae ameonyesha uwezo mkubwa katika mechi zote alizocheza akiwa na timu hiyo msimu huu anasema anachokitamani ni kufanya vizuri zaidi katika Ligi hata kimataifa hali itakayomfanya awe mahali pazuri kirekodi lakini hata ubora kwani lengo lake ni kucheza kwa mafanikio.

"Naamini sana kwenye mpira kuongea na sio mimi hivyo tusubiri tuone matokeo mazuri na sio kingine ila naahidi kutoa nguvu,ushirikiano na ubora unaohitajika ili kuhakikisha mafanikio yanapatikana," anasema kiungo huyo.

MAYELE YUKO MOYONI

Morice anasema katika Ligi ya Tanzania,alikuwa anafuatilia wachezaji wengi tangia alipofahamu tu kuwa watakutana na Yanga kucheza nao lakini aliendelea kumfuatilia Mayele hata walipomaliza kucheza nao.

Anaendelea kusema ijapokuwa ameondoka lakini kwake anaona ni mmoja kati ya washambuliaji bora aliowahi kuwafahamu na kuwafuatilia katika soka kwa ujumla.

“Ni mchezaji mwenye juhudi na kiu ya mafanikio kwa timu yake alikuwa anapambana na kuonekana kuwa kuna jambo analihitaji pindi awapo uwanjani kuna vitu vingi vya kujifunza kutoka kwake.”

KIDOGO AWE WAKALA

Kiungo huyo anasema anapenda mpira wa miguu tangu utotoni na hakufikiria kufanya kazi yoyote nje na hiyo lakini kama ingeshindikana kupata nafasi ya kucheza basi angekuwa wakala wa wachezaji.

“Nisingecheza mpira basi ningekuwa nauza wachezaji kutoka timu moja kwenda nyingine kwani hii kazi ipo kwenye damu hivyo nisingeweza kucheza ila ningekuwa nafanya hata kwa namna hii."

MOTO UTAWAKA

Kiungo huyo mwenye uwezo wa kutumika kama namba 6 au 8 anasema malengo yake ni kufanya vizuri kimataifa na kuifanya timu yake mpya kufikia malengo yake kwa ukubwa hasa kwa upande huu ambao ni mgeni.

Anasema ana uzoefu wa mechi hizo na kucheza michuano mikubwa hivyo ana uhakika kwa timu yake mpya wanakwenda kufanya makubwa kwani amekutana na kikosi chenye shauku ya matokeo.

“Tunakwenda kufanya makubwa kwani msimu huu nimekutana na wachezaji wenye malengo makubwa na uwezo ambao utakwenda kuufanya msimu huu kuwa wa kihistoria kwa timu yetu lakini hata Ligi yetu kwa ujumla.

Wengi wetu ni vijana na tuna uzoefu na nguvu na mazoezi yetu ni mazuri hivyo basi mashabiki watajionea wenyewe kile ambacho tunakwenda kukitengeneza msimu huu katika kila mechi.”

KAZINI KUNA KAZI

Morice anasema kwa kipindi kifupi alichofanya mazoezi ameona mengi lakini kubwa ni namna wachezaji wa kikosi hicho walivyobora na kutumia vizuri kila nafasi wanayoipata.

Anasema vita ni kupata namba kwani sio kazi rahisi kwenye timu yenye wachezaji wengi wazuri na wanataka kucheza hivyon ukizubaa kidogo nafasi inabebwa na mtu mwingine.

"Jitihada zinahitajika ili kupata nafasi kwani haitakuwa kazi rahisi ila nafurahi kwani ni changamoto mpya na nzuri kwangu inanijenga kuwa bora zaidi na kuwa makini uwanjani.”

MSOSI KAMBINI

Morice anasema kwake amevutiwa na vyakula vya huku japokuwa ni vigeni kwake ila anafurahia kula chapati kuliko vingine alivyowahi kuvila kama ugali,wali nyama na vinginevyo.

"Napata changamoto ya chakula kwani vingi sijavizoea kwa sasa ila naamini muda unavyozidi kwenda nitaweza kula kila kitu kwani naamini ni vizuri na vitamu pia ila sipendi wali."

CHANGAMOTO

Kiungo huyo anasema kwake ilikuwa kazi ngumu kidogo kukabiliana na hali ya hewa ya Arusha alipofikia kambini kwani muda mwingi ni baridi ila sasa mwili wake umeshazoea hewa ya huku kwa ujumla.

"Mabadiliko ya kimazingira huwa yanaleta shida katika mwili wa binadamu ila sasa nimekaa sawa kabisa ijapo mwanzoni nilijiuliza kama nitaweza maana nilifika Dar es salaam kuna joto na nikaenda Arusha penye baridi kali."

Chanzo: Mwanaspoti