Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha, wametangaza uzinduzi rasmi wa mashindano ya mpira wa miguuni Jimbo la Arusha Mjini maarufu kama Chuga Cup 2023.
Mashindano hayo yatazinduliwa rasmi Agosti 19, 2023 na kuhusisha timu 32 ambapo timu 25 zitatoka Wilaya ya Arusha na timu 7 kutoka Monduli na Arumeru ambazo zimegawanywa katika makundi nane ya timu nne kila kundi.
Baada ya hatua ya makundi kukamilika timu zitaingia hatua ya 16 Bora kisha Robo Fainali, nusu na hatimaye fainali.
Mshindi wa kwanza atajinyakulia kitita cha Tsh milioni 5, wa pili Tsh milioni 3 na wa tatu Tsh milioni 1.
Pia kutakuwa na zawadi ya mchezaji bora, mfungaji bora, kipa bora na mwamuzi bora wa mashindano hayo mara baada ya kukamilika kwa ligi hiyo.
Aidha, Gambo amesema kuwa Agosti 13, 2023 vitagaiwa Vifaa vya Michezo kwa timu zote kwenye ukumbi wa Gran Melia kuanzia saa 8 Mchana.