Wachezaji chipukizi na Klabu za soka ya mastaa katika mji mkuu wa Ghana, Accra wamekutana kuomboleza kifo cha mchezaji wa kimataifa wa nchi hiyo Christian Atsu aliyepatikana akiwa amefariki, baada ya majuma mawili kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililotokea nchini Uturuki.
Wakiwa katika uwanja wa mazoezi, mmoja wa wachezaji hao Kweku Ajimai alisema “matendo mema ya Christian Atsu watu hawawezi kuyaona, aliwasaidia maskini katika jamii zao, katika kijiji chake, hapa Accra, hapa Ghana, na kote na amekwenda kimwili lakini yupo nasi rohoni.”
Kwa upande wake Meneja wa Atsu nchini Uturuki, Murat Uzunmehmet akiongea na vyombo vya Habari alisema mwili wake ulipatikana chini ya vifusi vya nyumba za kifahari zilizobomoka katika jimbo la kusini la Hatay nchini humo.
Awali, kulikuwa na ripoti kwamba mchezaji huyo wa zamani wa Chelsea na Newcastle alikuwa ameokolewa siku moja baada ya tetemeko hilo, lakini hizi ziligeuka kuwa ni habari za uwongo baada ya mwili wake usio na uhai na simu yake kupatikana.
Wizara ya mambo ya nje ya Ghana, ilisema imepokea habari hizo za kusikitisha na itakumbukwa kuwa dada na pacha wa Christian Atsu na afisa wa ubalozi wa (Ghana nchini Uturuki), walikuwepo kwenye eneo hilo wakati mwili ulipopatikana.