Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chilunda, Wazir JR wapata chimbo jipya

Chilundaaaaaaaaaaaaaaa Chilunda, Wazir JR wapata chimbo jipya

Fri, 12 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mastaa mbalimbali wa Ligi Kuu Bara wakiwamo nyota wa zamani wa Simba na Yanga, akiwamo Shaaban Idd Chilunda na Waziri Junior wameonekana kupata chimbo jipya baada ya kufumaniwa wakijifua kwenye Uwanja wa Bora, uliopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam wakijiweka fiti kwa msimu ujao wa mashindano.

Mwanaspoti limeshuhudia wachezaji hao, wakijifua katika mazoezi hayo chini kocha wa timu ya vijana ya Simba, Mohammed Mrishona ‘Xavi’, ambapo asilimia kubwa yalionekana ni ya kujenga fitinesi na kuchezea mipira.

Baadhi ya mastaa hao ni Waziri Junior anayehusishwa na timu mbalimbali za ndani na nje, Chilunda aliyekuwa anacheza KMC kwa mkopo akitokea Simba iliyoachana naye, Tiba John alikuwa nje ya nchi, Shelda Boniface (JKT Queens) ambaye alikuwa anafanya mazoezi na wanaume.

Ukiachana na hao kuna beki Shomari Kibwana ambaye amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kusalia Yanga, ambayo tayari wachezaji wanafanya mazoezi na kurudi nyumbani.

Kibwana alizungumzia mazoezi hayo kwamba ni ya kujiongeza ili aendelee kuwa bora zaidi muda ambao wataingia kambini moja kwa moja.

“Umenikuta hapa ni mazoezi binafsi, maana ya timu nakwenda kufanya jioni, mazoezi ya maandalizi ya msimu ni magumu, lazima nijitoe kweli kweli, jioni naenda kufanya ya timu,” alisema.

Kwa upande wa kocha Xavi, alisema anapokea wachezaji mbalimbali wa ndani na nje, ambao wanakuwa na programu ambazo wanapewa na makocha wao na wengine wanakuwa na za kwao wenyewe.

“Wapo ambao wanakuwa wanajua udhaifu wao, hivyo wanakuwa wanaomba niwaelekeze jinsi ya kuondoa udhaifu wao, wengine wanakuja na programu za makocha,” alisema.

Kwa upande wa Junior alisema anafanya mazoezi hayo kwa ajili ya kujiweka fiti, ili atakapoanza kazi katika timu atakayokuwepo asianze na sifuri.

“Tunaenda kwenye maandalizi ya msimu, mazoezi yake ni magumu, hivyo lazima nijipange vilivyo kuhakikisha niwe fiti na tayari kuendana na programu za kocha,” alisema.

Alipoulizwa msimu ujao anakwenda timu gani, Waziri Junior alijibu kwa ufupi; “Kwa hilo naomba mnivumilie, mambo ni mengi, nikisaini mtajua nitacheza wapi?”

Chanzo: Mwanaspoti