Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chico akoleza moto Yanga

Chico Pic Chico akiwa mazoezini

Sat, 22 Jan 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na dakika 26 alizotumia kucheza mechi yake ya kwanza akiwa na uzi wa Yanga, ujio wa mshambuliaji Chico Ushindi umeelezwa utakoleza moto zaidi kwa vinara hao wa Ligi Kuu Bara. Chico amesajiliwa na Yanga dirisha dogo akitokea TP Mazembe ya DR Congo na juzi kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Mbuni iliyopo First League aliingia dakika ya 64 akimpokea Deus Kaseke.

Ndani ya dakika hizo 26, nyota huyo anayemudu wingi zote aliwapagawisha mashabiki, lakini inaelezwa ujio wake unazidi kukoleza moto uliopo Jangwani kwa sasa kiasi cha kutetemesha wapinzani. Chico anatua Yanga wakati timu hiyo ikiwa kileleni mwa msimamo ikikusanya pointi 32, ikifunga mabao 22 na yenyewe ikiruhusu kufungwa mabao machache.

Licha ya kuwa mbele kwa mchezo mmoja zaidi ya watani wao, Simba wanaoshika nafasi ya pili, bado hata kama watetezi hao watashinda kiporo chao na Kagera Sugar bado kutakuwa na pengo la pointi tano baina yao na Yanga.

Simba imecheza mechi 11 na kukusanya pointi 24, ikifunga mabao 14 na kufungwa matano na kuifanya Yanga iwe na jeuri msimu huu ikiamini kama itaenda na moto huo huo. Hata hivyo jeuri yote ya Yanga mbele ya Simba hadi sasa inaonekana kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na mastaa wake watatu kwa kuifanya timu hiyo ikimbie kwa kasi katika safari ya kusaka ubingwa.

Wachezaji hao ni Fiston Mayele, Feisal Salum na Saido Ntibazonkiza.

Watatu hao kwa pamoja wamefunga zaidi ya 50% ya mabao yote ambayo Yanga imepachika msimu huu yaliyoiweka kileleni huku kukiwa hakuna utatu mwingine uliohusika na idadi kubwa ya mabao kuliko huo sio tu kwenye kikosi cha Simba bali pia hata timu nyingine kiujumla.

Ntibazonkiza, Mayele na Feisal kwa pamoja wamefunga mabao 14 ambayo ni sawa na 63.64% ya mabao yote 22 ya Yanga lakini mabao hayo ni sawa na mabao yote 14 yaliyofungwa na Simba katika mechi zake 11 ilizocheza.

Ukiondoa Simba, idadi hiyo ya mabao 14 yaliyofungwa na Feisal, Mayele na Ntibazonkiza ni sawa na jumla ya mabao yaliyofungwa na Azam FC na mbali na hizo, timu pekee ambayo imewazidi mabao watatu hao ni Mbeya City iliyofunga mabao 16. Lakini mbali na Simba, Azam na Mbeya City, hakuna timu hata moja kati ya 14 zilizobakia ambayo imeweza kufunga idadi kubwa ya mabao kuzidi yale yaliyopachikwa na wachezaji hao watatu tu wa Yanga.

Polisi Tanzania, Biashara United, Namungo FC, KMC, Mbeya Kwanza na Ruvu Shooting kila moja imepachika mabao 11 huku Geita Gold ikifunga mabao tisa na Dodoma Jiji imefunga mabao tisa.

Timu ambazo kila moja imefunga mabao nane ni Coastal Union, Prisons na Kagera Sugar wakati Mtibwa Sugar imefunga nusu ya mabao yaliyopachikwa na Mayele, Ntibazonkiza, Mayele na Feisal ambayo ni saba.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa alisema; “Timu iko vizuri na usajili uliofanyika ni wa wachezaji wa viwango vya juu ambao wamekuwa na mchango mkubwa kikosini hivyo Wanayanga wawe watulivu na waendelee kuiunga mkono timu, mambo mazuri yanakuja.” Kwa upande wake Saido alisema; “Lengo letu kuu msimu huu ni kutwaa ubingwa wa ligi hivyo ni jukumu la kila mchezaji kucheza kwa kujitolea ili tupate ushindi kwenye mechi zetu na tuweze kulitimiza.”

KAZE NA CHICO

Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alimzungumzia Chico; “Mchezaji anayetambua umuhimu wa timu aliyopo naamini kwa kushirikiana na wachezaji wengine watafanya vizuri zaidi,” alisema Kaze aliyesisitiza anaamini Yanga inazidi kuimarika kwa wachezaji waliongezwa dirisha dogo mbali na Chico, lakini kuna kipa Abuutwalib Mshery, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Winga Denis Nkane na mshambuliaji Crispin Ngushi.

Naye Chico alisema alichojifunza kwa mashabiki ni kujiamini na kujua kitu gani wanakitaka ili kuwapa raha na atajitahidi kutumia vyema nafasi ya kucheza atakazopata kuiwezesha timu kutimiza malengo na mikakati iliyojiwekea.

Chanzo: Mwanaspoti