Chelsea haitaki kabisa kusikia jibu la hapana kwenye msako wao wa kumfukuzia winga wa Crystal Palace, Michael Olise, huku wakijaribu kila njia ya kunasa saini yake hata kama kwa dili la kubadilisha wachezaji.
Ripoti zinadai kwamba Chelsea ipo kwenye hatua nzuri katika kufukuzia huduma ya Olise na huenda ikashinda vita hiyo dhidi ya wababe wengine wa Ligi Kuu England ambao pia wamekuwa wakipambana kumsajili winga huyo mzaliwa wa England, aliyeichezea Ufaransa kwenye soka la vijana, huku akiwa na asili pia ya Nigeria.
Olise anayechezea timu ya taifa ya Ufaransa chini ya miaka 22, aliibukia kwenye akademia ya Chelsea, kabla ya kuachana na klabu hiyo ya Stamford Bridge wakati alipokuwa na umri wa miaka 14.
Kwa sasa, Olise amejipambanua kama mmoja wa mastaa kwenye Ligi Kuu England. Baada ya kuanzia kwenye ligi ya chini akiwa na Reading, alijiunga na Crystal Palace mwaka 2021 na hadi sasa amefunga mabao 14 na asisti 22 katika mechi 82 alizochezea kikosi cha Eagles kwenye ligi.
Chelsea ilishindwa kidogo kumnasa Olise mwaka jana, ambapo winga huyo alikubali kusaini dili jipya huko Selhurst Park.
Lakini, baada ya kufunga mara 10 katika dakika zisizozidi 1,300 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, hadhi yake imepanda zaidi.
Ripoti zinadai kwamba Chelsea imepanga kumtoa ofa Trevoh Chalobah au Noni Madueke kuwa sehemu ya dili hilo la kumnasa Olise.
Wachezaji wengine waliodaiwa kuwekwa kwenye mpango huo ni Armando Broja na Cesare Casadei, huku kinachoelezwa ni kwamba Palace wao, wanaweza kushawishika na mpango wa kumchukua winga wa zamani wa PSV Eindhoven, Madueke.
Thamani ya Olise inaripotiwa kuwaPauni 60 milioni kitu ambacho kinaipa shida Chelsea kwa kuwa hawajafunzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, hivyo bajeti yao inabana, labda kama tu itauza mastaa wake kibao kumfanya kocha Enzo Maresca amnase Olise anayemtaka.