Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chelsea ni kuuza tu hakuna namna

Chelsea 2023 24 Chelsea ni kuuza tu hakuna namna

Sun, 3 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wapinzani wa Chelsea wanafahamu wazi miamba hiyo ya Stamford Bridge itawafungulia mlango wa kutokea mastaa kibao itakapofika Juni 30 ili kwenda sawa na ishu ya Financial Fair Play.

Chelsea imetumia zaidi ya Pauni 1 bilioni kwenye usajili tangu ilipoanza kuwa chini ya mmiliki mpya, bilionea Todd Boehly mwaka 2022.

Usajili wao mkubwa hauendani na wanachovuna ndani ya uwanja na kikosi hicho kipo mbali sana na Top Four kwenye msako wao wa kutafuta nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.

Ishu ya mapato na matumizi imekuwa siriazi kwenye Ligi Kuu England msimu huu na Everton imekatwa pointi sita baada ya kuonekana ilizidisha matumizi.

Ili kukwepwa kukumbwa na kilichowakuta Everton, Chelsea italazimika kuuza wachezaji wake ikiwamo kadhaa waliokuwa wamebeba matumaini makubwa kwenye kikosi cha kwanza.

Na kinachoelezwa, Chelsea italazimika kuuza kabla ya kufika Juni 30 ili kuchangisha Pauni 100 milioni ambayo itawaweka sawa kwenye vitabu vyao vya mapato na matumizi.

Tarehe hiyo iliyotajwa itakuwa katikati ya michuano ya Euro 2024 na Copa America, hivyo Chelsea itakuwa kwenye purukushani kubwa kwenye masuala ya usajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Taarifa za kutoka ndani ya Chelsea zinadai wachezaji wengi watauzwa dirisha lijalo ili kuleta wachezaji wengine wenye vipaji bora zaidi.

Miongoni mwa mastaa ambao watafunguliwa mlango wa kutokea ni pamoja na straika Romelu Lukaku, ambaye imeelezwa dau la Pauni 37 milioni limeshakubaliwa ili ajiunge jumla AS Roma, licha ya kwamba Chelsea ililipa Pauni 99.5 milioni kunasa saini yake mwaka 2021.

Wachezaji wengine ambao safari inaweza kuwahusu ni Ian Maatsen, Reece James, Conor Gallagher, Trevoh Chalobah, Armando Broja, Marc Cucurella na Kepa Arrizabalaga.

Chanzo: Mwanaspoti