Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chelsea na Arsenal wapo darajani, Man United, City wana jambo lao

Che Vs Ar Chelsea na Arsenal wapo darajani, Man United, City wana jambo lao

Sat, 21 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ule uhondo wa Ligi Kuu England unarudi tena wikiendi hii, huku macho na masikio ya wengi yatategwa huko Manchester United kujua kitatokea nini. Wanalo hilo.

Mechi nane zitapigwa leo Jumamosi, huku Man United iliyoponea chupuchupu kuchapwa tena na kushinda 2-1 baada ya mabao ya dakika za majeruhi ya kiungo, Scott McTominay kwenye mechi yao dhidi ya Brentford. Leo hii itakipiga na Sheffield United ugenini.

Kingine kitakachovutia leo ni kipute cha Merseyside derby, ambapo Liverpool itakuwa nyumbani Anfield kukipiga na mahasimu wao Everton. Hata hivyo, mechi hiyo haitazamwi kama itakuwa na mvuto sana kutokana na kiwango cha sasa cha Everton.

Huko Stamford Bridge pia kutakuwa na moto, ambapo Chelsea itakuwa na kazi nzito ya kuikabili Arsenal, inayocheza kandanda la kibabe sana msimu huu, huku Manchester City itajiuliza baada ya vichapo viwili mfululizo wakati itakapokuwa Etihad dhidi ya Brighton.

Man United na Sheffield United mchezo wao wa Bramall Lane utakuwa wa 11 kukutana kwenye Ligi Kuu England, na katika mechi 10 zilizopita, Man United imeshinda saba, nne ikiwa nyumbani na tatu ugenini, huku Sheffield imeshinda mbili, moja nyumbani na nyingine ugenini. Mechi moja ilimalizika kwa sare, lakini mchezo wa mwisho kukutana, Man United ilikubali kichapo cha 2-1 Old Trafford.

Mahasimu wa Merseyside derby, rekodi zao zinaonyesha wamekutana mara 62 kwenye Ligi Kuu England, ambapo Liverpool imeshinda 27, mara 16 ikiwa Anfield na 11 ugenini, wakati Everton imeshinda 10, saba ikiwamo Goodison Park na tatu ugenini, huku mechi 25 zilimalizika kwa sare. Zilipokutana mara ya mwisho, Liverpool ilishinda mabao 2-0 uwanjani Anfield. Itashinda tena? Ngoja tuone.

Man City baada ya kuchapwa mara mbili mfululizo kwenye ligi, dhidi ya Wolves na Arsenal, itakuwa Etihad kuwakaribisha wagumu wengine, Brighton. Rekodi zinasoma, Man City na Brighton zimekutana mara 12, mechi moja ilimalizika kwa sare na Brighton imeshinda moja tu, ilipokuwa nyumbani - wakati Man City imeshinda 10, sita nyumbani na nne ugenini. Zilipokutana mara ya mwisho ndipo sare ilipopatikana.

Kutakuwa na kipute cha London derby huko Stamford Bridge, ambapo The Blues iliyoanza msimu kwa kusuasua itakuwa na kazi ya kukutana na moto wa Arsenal. Kutatokea nini?

Namba zinaonyesha, miamba hiyo kwenye Ligi Kuu England imekutana mara 62, ambapo Chelsea imeshinda 20, mara 13 nyumbani na saba ugenini, huku Arsenal ikishinda 25, mara 15 nyumbani na 10 ugenini, wakati mechi 17 zilimalizika kwa sare. Mechi tatu zilizopita, Arsenal imeshinda zote ikiwamo ya mwisho ya mabao 3-1 Emirates.

Newcastle United itakuwa na kasheshe la kuikabili Crystal Palace uwanjani St James’ Park, ambapo rekodi zinaonyesha miamba hiyo imekutana mara 24 kwenye Ligi Kuu England, Newcastle ikishinda 11, sita nyumbani na tano ugenini, huku Palace yenyewe imeshinda tano, mbili nyumbani na tatu ugenini na kuna mechi nane ziliisha kwa sare. Mechi mbili za mwisho, timu hizo zilitoka sare ya bila mabao.

Bournemouth itakuwa na kazi nzito dhidi ya Wolves, wakati Brentford itakuwa nyumbani kumaliza machungu ya kuchapwa dakika za majeruhi kwenye mchezo uliopita kwa kuwaalika Burnley.

Nottingham Forest itajimwaga kwao City Ground kucheza dhidi ya Luton, mechi inayotajiwa kuwa na mvuto mkubwa kutokana na nafasi inazoshika timu hizo kwenye msimao wa Ligi Kuu England.

Kesho, Jumapili kutakuwa na mechi moja tu, huku Villa Park - ambapo Aston Villa zitakuwa na kazi ya kuulizana na maswali na West Ham United.

Rekodi zinaonyesha kwamba timu hizo zimekutana mara 48 kwenye Ligi Kuu England, ambapo Aston Villa imeshinda 13, tisa nyumbani na nne ugenini, huku West Ham ikishinda 14, nane nyumbani na sita ugenini, wakati mechi 21 zilimalizika kwa sare.

Vinara wa Ligi Kuu England msimu huu, Tottenham Hotspur wenyewe watasubiri hadi Jumatatu watakapokuwa nyumbani kuwakabili wababe wengine wa London, Fulham. Miamba hiyo ina rekodi ya kukutana mara 32 kwenye Ligi Kuu England, ambapo Spurs imeshinda 18, mara 10 nyumbani na nane ugenini, wakati Fulham imeshinda saba, tano nyumbani na mbili ugenini.

Mechi saba baina yao zilimalizika kwa sare, huku mechi tatu zilizopita, Spurs imeshinda zote dhidi ya Fulham. Itakuwaje safari hii. Ni mambo ya kusubiri na kuona.

Ligi Kuu England inarejea baada ya mapumziko ya wiki mbili kupisha mechi za kimataifa.

Chanzo: Mwanaspoti