Chelsea wanaripotiwa kutafuta uwezekano wa kumsajili nyota wa Borussia Dortmund Youssoufa Moukoko katika dirisha la usajili la Januari.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 18 amejiweka katika kikosi cha kwanza mara kwa mara akiwa na kikosi cha Bundesliga msimu huu, na kuandikisha mabao sita na kusaidia mengine sita katika mechi 22 alizocheza kwenye michuano yote.
Kiwango cha kuvutia cha Moukoko kilizawadiwa kwa kuitwa kwenye kikosi cha Ujerumani kwa ajili ya Kombe la Dunia 2022 na kijana huyo akawa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea katika timu hiyo alipotoka kwenye benchi katika mechi ya mwisho ya kichapo cha 2-1 dhidi ya Japan.
Kinda huyo wa BVB anatazamiwa kuwa miongoni mwa vijana wanaotafutwa sana wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa tena mwaka mpya, huku klabu za Chelsea, Manchester City, Manchester United, Liverpool, Barcelona na Real Madrid zikipigania saini yake.
Kwa mujibu wa gazeti la The Athletic, Chelsea wanafikiria uwezekano wa kumnunua Moukoko na vilabu vingine vya Ligi Kuu ya Uingereza vinaamini kwamba harakati za The Blues kumnasa fowadi huyo ziko katika hatua ya juu, ingawa uhamisho huo haufikiriwi kuwa karibu kwa sasa.