Klabu ya Chelsea wanatazamia kukusanya Pauni 500 milioni kutoka kwa taasisi za fedha za Marekani kwa mujibu wa ripoti.
Hiyo ni kwa sababu wapigaji pesa wakubwa wa Stamford Bridge wanatafuta mkopo, kitu ambacho hata klabu zingine za Ligi Kuu England zimefanya katika miaka ya hivi karibuni.
Hatua hiyo inakuja baada ya matumizi makubwa kufanyika katika usajili wa wachezaji chini ya mmiliki mpya Todd Boehly.
Mmarekani huyo mwenye umri wa miaka 50, ametumia Pauni Bilioni 1 katika madirisha matatu ya usajili hivi karibuni, hata hivyo licha ya kutumia pesa nyingi katika usajili wa wachezaji bado timu inasuasua.
Makocha Thomas Tuchel, Graham Potter na Frank Lampard wote waliondoka katika mazingira magumu msimu uliopita, huku Mauricio Pochettino akiendelea kukisuka kikosi chake.
Chelsea ilihusishwa na Ivan Toney wa Brentford na Victor Osimhen wa Napoli ni washambuliaji wawili wanaolengwa na The Blues.
Lakini mchezaji wa zamani wa Chelsea Frank Leboeuf anahisi mmiliki wa sasa wa klabu hiyo (Boehly) anaweza kuiweka katika hali mbaya.
"Hebu tuseme ukweli - Chelsea ni klabu ya kati kwa sasa. Kuvutia wachezaji kutakuwa ngumu na wachezaji kama Kylian Mbappe hawatakuja. Wachezaji wakubwa wanataka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Arsenal walikuwa na tatizo kama hilo kwa miaka mingi, bila kuisahau Manchester United." alisema Leboeuf