Ofa ya Pauni 80 milioni ya Chelsea iliyotolewa kwa ajili ya kiungo Moises Caicedo imepigwa chini na kumpa presha Kocha Mauricio Pochettino.
Kwa mujibu wa mkali wa usajili, Fabrizio Romano amesema Brighton inataka Pauni 100 milioni ndio imuachie kiungo huyo wa kimataifa wa Ecuador.
Caicedo, 21, aliweka wazi nia yake ya ya kutaka kuhamia Stamford Bridge alipoulizwa na mashabiki wakati anawasainia jezi kwenye maandalizi ya msimu mpya.
Naye Kocha Pochettino alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kusajili kiungo mpya kufuatia sare ya bao 1-1 dhidi ya Newcastle kwenye mechi ya kirafiki akajibu: “Klabu inafanya jitihada na ndio mipango yangu kwa sasa. Tunahitaji wachezaji wapya. Tunahitaji wachezaji wenye uzoefu. Inategemea ni wachezaji wa aina gani. Tunataka mmoja au zaidi.”
Wakati wa ziara ya maandalizi ya msimu mpya amekwenda na wachezaji 29 wa kuchagua nani atakuwepo kwenye kikosi msimu mpya utakapoanza.
Pochettino alisema: “Tuna wachezaji 29 kwa sasa. Hii italeta taharuki kwenye timu. Huwezi kuchezesha wachezaji wengi, muhimu ni kutengeneza timu na kuna wachezaji ambao watapata nafasi na wengine watagombeana nafasi.”
Chelsea ilimaliza nafasi ya 12 ikiwa na alama 44 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu uliopita, sasa imepania kurudi kwa kishindo msimu ujao.