Chelsea imekuwa gumzo baada ya kuonyesha umwamba wa kutumia pesa ndani ya mwaka mmoja uliopita. Miamba hiyo ya Stamford Bridge baada ya kuwa chini ya mmiliki mpya, bilionea Todd Boehly hakuna kilichobadilika kwenye matumizi ya mkwanja, baada ya kutumia Pauni 600 kwenye madirisha mawili tu ya usajili.
Ukiweka kando matumizi ya pesa nyingi kwenye usajili, Chelsea pia ndiyo timu ilikuwa na bili kubwa ya mishahara kuliko timu nyingine zote kwenye Ligi Kuu England kwa msimu huu.
Kwa kuzingatia timu zile zinazotajwa kuwa ni Big Six, cheki hapa msimamo wa timu iliyokuwa na bili kubwa ya mishahara kwenye Ligi Kuu England msimu huu, huku Chelsea ikithibitisha kwamba wakati mwingine pesa haiwezi kununua mapenzi.
1. Chelsea - Pauni 216.6 milioni
Kwa mujibu wa ESPN, Chelsea ilitumia Pauni 600 milioni kusajili wachezaji wapya 16 tangu ilipokuwa chini ya bilionea Todd Boehly na kwenye usajili huo, upo uliovunja rekodi ya Uingereza wa Enzo Fernandez, Pauni 106.8 milioni. Na kwenye hilo, Chelsea imejikuta ikiwa timu yenye bili kubwa zaidi ya mishahara, Pauni 216.6 milioni - ikitumia kulipa mastaa wake zaidi ya 30 waliopo kwenye kikosi.
2. Man United - Pauni 213.3 milioni
Manchester United imeshuka hadi namba mbili kwenye ishu ya kuwa na bili kubwa ya mishahara baada ya kumwondoa Cristiano Ronaldo kwenye kikosi chao. Mreno huyo alikuwa analipwa pesa nyingi sana na sasa yupo zake Al-Nassr huko Saudi Arabia. Bili ya sasa ya mishahara ya Man United ni Pauni 213.3 milioni, huku mchezaji mwenye mshahara mkubwa ni kipa David De Gea anayelipwa Pauni 375,000 kwa wiki.
3. Man City - Pauni 186.16 milioni
Mambo makubwa matumizi kidogo ya pesa, hivyo ndivyo wanavyofanya Manchester City. Timu hiyo, ambao ni mabingwa mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu England bili yao ya mishahara kwa mwaka ni Pauni 186.16 milioni. Na hiyo licha ya kikosi chao kuwa na mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kuliko wote kwenye Ligi Kuu England, Kevin De Bruyne, anayepokea Pauni 400,000 kwa wiki.
4. Liverpool - Pauni 164.5 milioni
Liverpool inashika nafasi ya nne kwenye orodha ya timu zenye bili kubwa ya mishahara kwa upande wa Big Six kwenye Ligi Kuu England. Miamba hiyo ya Anfield bili yao ya mishahara kwa mwaka ni Pauni 164.5 milioni. Na bili hiyo inaweza kupungua zaidi kutokana na kuwapo mastaa kibao watakaoondoka mwisho wa msimu. Mohamed Salah ndiye anayelipwa mshahara mkubwa, Pauni 350,000 kwa wiki.
5. Arsenal - Pauni 110.3 milioni
Arsenal walikuwa na kiwango bora sana kwenye Ligi Kuu England msimu huu na kujikuta wakimaliza nafasi ya pili. Hata hivyo, bili yao ya mishahara wala sio kubwa, wakishika nafasi ya tano kwenye Big Six kutokana na kutumia Pauni 110.3 milioni kulipa mishahara kwa mwaka. Bukayo Saka, aluyesajili mkataba mpya hivyo karibuni, ndiye anayelipwa mshahara mkubwa Emirates, Pauni 300,000 kwa wiki.
6. Tottenham - Pauni 110.2 milioni
Tottenham Hotspur ndiyo wanaoshika mkia kwenye orodha ya timu za Big Six zenye bili kubwa ya mishahara kwa mwaka kwenye Ligi Kuu England. Spurs bili yao kwa mwaka ni Pauni 110.2 milioni. Kwenye kikosi hicho, mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi ni straika Harry Kane, Pauni 200,000 kwa wiki - huku Manchester United ikimpa ofa ya kwenda kumlipa Pauni 300,000 kwa wiki akitua Old Trafford.