Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chelsea haimtaki tena straika Lukaku

Lukaku Nyavu Lukaku

Fri, 7 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Chelsea haitakubali maombi yoyote ya mkopo kuhusu straika Romelu Lukaku kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi na kusisitiza inachokikaribisha mezani ni dili la kumuuza jumla Mbelgiji huyo.

Lukaku aliitumikia AS Roma kwa mkopo kwenye msimu uliopita na sasa atarudi kwenye klabu yake huko Stamford Bridge.

Huo ulikuwa msimu wa pili mfululizo wa mkopo na awali alikuwa kwenye kikosi cha Inter Milan.

Chelsea ililipa ada iliyovunja rekodi ya klabu ya Pauni 97.5 milioni iliponasa saini ya Lukaku mwaka 2021, lakini staa huyo alishindwa kufikia matarajia ya mabosi wa The Blues na alipoteza kwa mkopo baada ya kucheza kwa msimu mmoja tu Stamford Bridge.

Na sasa Chelsea inataka kuondokana kabisa na kibarua cha kulipa mshahara wa Pauni 325,000 kwa wiki, hivyo itakubali ofa ya Pauni 37 tu milioni kwa timu itakayokuwa inahitaji huduma ya jumla ya mshambuliaji Lukaku.

AC Milan na Napoli zinahitaji huduma ya Lukaku, lakini zote hazina pesa ya kutosha kulipa kiasi hicho kinachohitajika na Chelsea.

Napoli imemteua Antonio Conte kuwa kocha wao mpya, hivyo Mtaliano huyo anamtaka Lukaku, ambaye walibeba ubingwa wa Serie A walipokuwa pamoja huko Inter Milan.

Kwenye mipango yao, Napoli inataka kufanya dili la kubadilishana Lukaku na straika Victor Osimhen, lakini shida inakuja sehemu moja, Chelsea haina mpango wa kumsajili Mnigeria huyo, ambaye anathaminishwa kuwa na thamani inayozidi Pauni 100 milioni.

Kwa sasa chelsea inachokitaka ni kumpiga bei jumla Lukaku, ambaye alitua Stamford Bridge wakati kikosi hicho kilipokuwa chini ya kocha Thomas Tuchel.

Chanzo: Mwanaspoti