Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chelsea, Real Madrid katika 18 za Masaka

Aisha Masaka 18 Chelsea, Real Madrid katika 18 za Masaka

Wed, 25 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mambo yamejipa, ndivyo unavyoweza kusema baada ya kile kilichokuwa kichwani mwa mchezaji wa kike wa Kitanzania, Aisha Masaka baada ya chama lake, BK Hacken la Sweden kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya Ulaya na litakutana na Real Madrid (W) pamoja na Chelsea (W).

BK Hacken imetinga hatua hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo wa mkondo wa pili ugenini huko Uholanzi ambako ilikuwa ikimalizana na wenyeji wake, Twente na kwenye mchezo wa kwanza ilitoka sare ya mabao 2-2.

Ushindi wa jumla ya mabao 3-2, umelifanya chama hilo la Masaka kutinga hatua ya makundi ambayo imepangwa sambamba na vigogo wawili kwenye soka la Ulaya upande wa wanawake, Chelsea ya England na Real Madrid ya Hispania.

Akizungumzia kitendo cha kupangwa kundi moja na vigogo hao, Masaka amesema ni fursa ambayo alikuwa akitamani kuipata kwani kucheza dhidi ya Chelsea, Real Madrid na hata Paris FC ya Ufaransa si jambo dogo.

“Moja kati ya ndoto yangu ni kucheza kwenye ligi kubwa zaidi Ulaya, hivyo kwenda England, Hispania na Ufaransa ni fursa ya kuonyesha kipaji changu maana mashindano haya yanafuatiliwa na klabu nyingi, nina imani Uefa itanifungulia milango ya kupiga hatua zaidi,” anasema na kuongeza;

Haikuwa kazi nyepesi kwetu kuingia hatua ya makundi, mchezo wa kwanza tulitoka sare nyumbani, tulikuwa na kazi ngumu na kubwa ya kufanya ugenini lakini jambo zuri ni mpango wetu ambao tulienda nao Uholanzi ulifanikiwa na ndoto sasa zimetimia za kucheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa.”

Kocha wa BK Hacken, Mak Lind amewapongeza wachezaji wake kwa kazi kubwa ambayo waliifanya Uholanzi hadi kutinga hatua ya makundi huku ikishuhudiwa Manchester United, VfL Wolfsburg zikitupwa nje.

“Shabaha yetu kwa sasa ni kufanya vizuri pia kwenye hatua ya makundi, tutajiandaa na yoyote ambaye atakuwa mbele yetu,” anasema kocha huyo. Hizi ni dondoo muhimu za wapinzani wa BK Hacken ambayo anaichezea Masaka.

CHELSEA (W)

Klabu ya Wanawake ya Chelsea ni timu yenye makao yake makuu Kingston upon Thames, London. Ilianzishwa mwaka wa 1992, inashindana katika Ligi Kuu ya Wanawake England na hucheza michezo yake nyumbani katika uwanja wa Kingsmeadow na baadhi ya michezo iliyochaguliwa huko Stamford Bridge.

Tangu 2004, klabu hiyo imekuwa ikishirikiana na Chelsea F.C. Timu ya wanaume kwenye Ligi Kuu ya England, Chelsea ya Wanawake ilikuwa mwanachama mwanzilishi wa Super League mwaka 2010. Kuanzia 2005 hadi 2010, timu hiyo ilishiriki Ligi Kuu ya Ligi Daraja la kitaifa, daraja la juu la soka la wanawake England wakati huo.

Mojawapo ya klabu zilizofanikiwa zaidi katika kandanda ya Uingereza ya wanawake, Chelsea imeshinda rekodi ya kutwaa mara sita ubingwa wa Ligi ya Wanawake ya Super League, pamoja na FA WSL Spring Series mwaka 2017.

Pia, imeshinda mataji matano ya Kombe la FA la wanawake, mataji mawili ya Kombe la Ligi ya Wanawake ya FA, ilishinda Ngao ya Jamii ya FA kwa wanawake mwaka wa 2020. Ilifika fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kwa Wanawake mwaka 2021na ilimaliza kama mshindi wa pili.

REAL MADRID (W)

Real Madrid ni klabu ya soka ya wanawake ya Uhispania. Ilianzishwa kama klabu huru ya Deportivo TACON 2014, baadaye ilipitia mchakato wa kuunganishwa na ununuzi na Real Madrid kuanzia 2019 na ilibadilishwa jina rasmi kama sehemu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Real Madrid 2020.

CD TACON ilianzishwa Septemba 12, 2014 na ilianza kucheza katika ngazi ya juu mwaka wa 2016. Jina TACON (kisigino) ni kifupi cha Trabajo (kazi) Atrevimiento (kuthubutu/ushujaa) Conocimiento (maarifa) Organización (shirika) Notoriedwn (kuonekana/kurejeshwa).

Katika msimu wa kwanza wa ushindani, 2015-16, klabu ilisajili timu ya vijana chini ya miaka 14 pekee. Juni 2016, TACON iliunganishwa na CD Canillas kwa kujumuisha timu za wakubwa na za chini ya miaka 19.

Katika msimu wa kwanza katika ngazi ya wakubwa, katika Divisheni ya Segunda ya 2016–17, TACON ilimaliza ya pili katika kundi lake la kanda, chini ya Madrid CFF, ambao ilishinda daraja hadi Primera Division.

Juni 2017, Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, alidai klabu hiyo ingeunda timu yake ya wanawake tangu mwanzo, na si kununua klabu iliyopo.

Kwenye Gazeti la El Larguero 2017, Perez alisema: “Bila shaka tutakuwa na timu ya wanawake. Tunaifanyia kazi, lakini itatoka kwenye nafasi ya klabu mpya, si timu ambayo tutaleta mchezaji bora kutoka Ujerumani, Brazil....” Juni 25 2019, bodi ya wakurugenzi ya Real Madrid CF ilitangaza pendekezo la kuunganisha TACON kama sehemu ya timu yao upande wa wanawake ili kuwasilishwa kwa jamii (wanachama) wao. Kama sehemu ya makubaliano, TACON ingecheza mechi zake za msimu wa 2019-20 huko Ciudad Real Madrid wakati wa mpito, huku muungano ukikamilika rasmi Julai mosi 2020.

PARIS (W)

Paris FC ni klabu ya soka ya wanawake ya Ufaransa yenye makao yake Mjini Viry-Châtillon, kitongoji cha Paris. Klabu hiyo ni sehemu ya wanawake ya klabu ya wanaume ya Ligue 2 Paris FC.

Paris FC ilianzishwa mwaka wa 1971 kama Etoile Sportive de Juvisy-sur-Orge, sehemu ya soka ya wanawake ya klabu ya ES Juvisy, yenye makao yake Juvisy-sur-Orge. Baada ya miaka 14, sehemu hiyo ilijitenga na klabu, ikaunda klabu yake chini ya jina la Klabu ya Soka Féminin Juvisy Essonne na kuhamia katika wilaya ya Viry-Châtillon.

Licha ya kuhama kutoka Juvisy-sur-Orge, klabu ya wanawake ilihifadhi jina FCF Juvisy huku kukiwa na usaidizi wa kifedha na usaidizi kutoka kwa jumuiya na Baraza Kuu la Essonne.

Katika msimu wa 1991-92, Juvisy ilishinda ubingwa wake wa kwanza wa Divisheni ya 1 ya Féminine. Kati ya miaka ya 1994-2003, klabu ilishinda mataji manne ya ligi na baadaye kushinda taji la Challenge de France 2005 na kuifanya Juvisy kuwa moja ya klabu zilifanikiwa zaidi katika soka la Ufaransa kwa wanawake.

Juvisy ilikuwa ikishiriki mara kwa mara katika Kombe la UEFA la wanawake. Julai 6, 2017, FCF Juvisy iliuzwa kwa Paris FC.

Klabu hiyo inasimamiwa na Emmanuel Beauchet na nahodha wa kimataifa wa Ufaransa Gaetane Thiney.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live