Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Cheki skwadi la Afrika Mashariki VPL

Skwadi Pic Data Cheki skwadi la Afrika Mashariki VPL

Sun, 28 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

UMEWAHI kujiuliza ingekuwaje wachezaji kutoka nchi zingine za Afrika Mashariki mbali na Tanzania wanaocheza Ligi Kuu Bara (VPL) wangeunda timu yao? Basi ondoa shaka, VPL imekusanya wachezaji wa kigeni kutoka ukanda huo kwa maana ya Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda. Hapa haijajumuisha nyota wa Tanzania kwenye skwadi hilo, kwani wenyewe wanaunda chama lao kiroho safi na kuliamsha hata na mapro hao wa kigeni wa ukanda huo. Mwanaspoti linakuchambulia na kukuletea mfano wa kikosi kinachoweza kupatikana kutokana na wachezaji kutoka nchi za Afrika Mashariki wanaocheza Bara.

JONATHAN NAHIMANA

Ni kipa wa Namungo ambaye pia anaidakia timu ya taifa ya Burundi.Alitua Tanzania misimu miwili iliyopita na kujiunga na KMC  timu ambayo aliidakia kwa mafanikio kabla ya msimu huu kutimkia Namungo.

Uwezo wake unamfanya kuwa namba moja kati ya wale wanaotoka katika nchini za Afrika Mashariki waliokuja kucheza soka la kulipwa akiwaweka nje Kipa wa Yanga, Farouk Shikalo ambaye ni raia wa Kenya, makipa kutoka Uganda ambao ni Mathias Kigonya (Azam) na James Sstuba (Biashara United).

NICHOLAUS WADADA

Uzoefu wake katika ligi ya Tanzania sio wa kutilia shaka hata kidogo.

Nyota huyu wa timu ya Taifa ya Uganda yupo Bongo tangu 2018 alipojiunga na Azam FC akitokea Vipers ya Uganda.



Tangu atue kwa wanalabalamba hao ameonekana kuhimiri lango la timu hiyo kutokana na uimara wake akicheza eneo la beki wa kulia ambapo anasifika kuwa bora kwenye kukaba na kupandisha mashambulizi.

YUSUPH NDIKUMANA

Ndikumana ni raia wa Burundi ambaye msimu ulioisha alisimama vyema eneo la ulinzi la KMC na kabla ya hapo alikuwa Mbao FC alikocheza kwa mafanikio.

Huyu ni beki wa viwango vya juu na hadi sasa yupo katika kikosi cha KMC, lakini amekuwa akisumbuliwa na majeraha muda mrefu na kwa sasa ameanza kuimarika. Kwenye mchezo wa Kombe la Azam dhidi ya KMC na Kurugenzi alicheza mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu kupita.

JOASH ONYANGO

Moja ya mabeki wa Ligi Kuu Bara ambao kwa sasa ukiingia sokoni kutaka kuwanunua utakutana na bei kubwa ni huyu mwamba kutoka Kenya.

Onyango ambaye amesajiliwa msimu huu na Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya ameonyesha kiwango bora zaidi na kuwafunga midomo mashabiki waliombeza wakati anasajiliwa wakisema kuwa ni mzee na kumtania kwa kumuita jina la babu.



Sio Simba tu, Onyango pia amekuwa beki tegemeo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ na ubora wake umeonekana kuimarika siku hadi siku.

JEAN MUGIRANEZA

Kwa mfumo wa 3-5-2, Mugiraneza ‘Migi’ atacheza eneo la mbele ya mabeki na kucheza kwa ufasaha. Huyu ni raia wa Rwanda ambaye moto wake sio wa kitoto. Mugiraneza ni moja kati ya wachezaji viongozi katika kikosi cha KMC ambapo kwa nyakati tofauti amekuwa akikitumikia kama nahodha na ana uwezo mkubwa wa kupunguza presha ya timu inapozidiwa. Kwa nyakati tofauti amekuwa akiitwa timu yake ya taifa. KMC walimsajili kutoka APR ya Rwanda.

THADEO LWANGA

Injinia - ndilo jina wanalomuita siku hizi mashabiki wa soka Bongo. Lwanga alisajiliwa na Simba kwenye dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, mwaka huu kwa lengo la kumpa nguvu na changamoto kiungo Jonas Mkude aliyeonekana kutawala dimba la kati la timu hiyo peke yake kwa muda mrefu.

Wakati Lwanga anasajiliwa na Simba alikuwa na zaidi ya miezi sita hajacheza mechi za mashindano baada ya kuachana na klabu ya Tanta ya nchini Misri.

Alipowasili Simba alianza kupiga tizi la maana ili kurudisha utimamu wa mwili na sasa gari limewaka - na kocha Didier Gomes amemwamini na kumfanya kuwa chaguo la kwanza kwenye nafasi ya kiungo mshambuliaji. Pia hivi karibuni karudishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uganda, jambo ambalo linalomuingiza kwenye kikosi bora cha wachezaji kutoka nchi za Afrika Mashariki wanaokuja kucheza soka la kulipwa.

STIVE NZIGAMASABO

Kama unaangalia vyema Ligi Kuu Bara utakuwa umewahi kumuona au kusikia hili jina hususani Namungo inapokuwa uwanjani. Stive ambaye ni raia wa Burundi, ni mchezaji anayemudu kucheza maeneo yote ya kiungo - kwa maana ya kiungo mshambuliaji na mkabaji. Nje ya Namungo, Stive amekuwa akiitumikia timu ya taifa ya Burundi kwa miaka isiyopungua mitano na hivi karibuni alishiriki katika michezo ya timu hiyo kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Africa (Afcon) mwakani nchini Cameroon.

HARUNA NIYONZIMA

Ukongwe kwenye ligi ya Bongo, uzoefu wa mechi za kimataifa na ubora mkubwa kwa muda mrefu vinamfanya Niyonzima kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha wachezaji wanaotokea nchi za Afrika Mashariki kuja kucheza Tanzania.

Mnyarwanda huyo amecheza Bongo kwa zaidi ya miaka saba kwani mwaka 2012 ndio alijiunga na Yanga akitokea APR ya nchini kwako na kukaa Jangwani hadi msimu wa 2017-18 alipohamia kwa watani zao, Simba kisha mwaka jana alirejea Yanga alipo mpaka sasa.

MEDDIE KAGERE

Huyu ndiye mshambuliaji mwenye mabao mengi mpaka sasa kwenye Ligi Kuu ndani ya msimu wa tatu sasa mfululizo.



Kagere ambaye ni mfungaji bora wa misimu miwili mfululizo tangu ajiunge Simba, bado ameendeleza moto wake licha ya kupata nafasi finyu ya kucheza, lakini hadi sasa ana mabao tisa kileleni kwenye orodha ya wafungaji msimu huu. Kwa rekodi hizo anaingia moja kwa moja kwenye kikosi bora cha wachezaji wa nchi za Afrika Mashariki wanaocheza soka Tanzania kwenye Ligi Kuu.

SAIDO NTIBANZOKIZA

Staa huyu raia wa Burundi amejiunga na Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea Vital’O ya nchini humo.

Uwezo wa Saido sio wa kubeza hata kidogo, kwani tangu amejiunga na Yanga ameleta mabadiliko makubwa katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kutokana na uwezo wake wa kucheza huku akiwaelekeza wenzake.

Pamoja na yote hayo, Saido pia ndiye mchezaji mwenye mafanikio makubwa kisoka kuliko wote wanaoshiriki Ligi Kuu Bara kwani amewahi kucheza klabu kubwa kama Nec Nijmegen, Cracovia, Akhisar Belediye SM Cean na Kaysar Kyzylorda.

FRANCIS KAHATA

Ukienda nchini Kenya utakuta wanamuita ‘Kachi’. Huyu ni fundi wa soka hasa. Anatema kulia, anafukia kushoto. Ni miongoni mwa viungo wa soka wanaofanya kazi ya kucheza mpira kuonekana rahisi kumbe ngumu.

Kahata kwa ubora wake, moja kwa moja anaingia katika kikosi cha wachezaji wa Afrika Mashariki wanaocheza soka la kulipwa Tanzania.

AKIBA

Mbali na hao, pia kuna nyota wengine wa kigeni wa ukanda huo wanaokaa benchi na wakiingia wanaliamsha tu wakiwamo Warundi Bigirimana Blaise, Eric Kwizera, Emmanuel Mvuyekure, Fiston Abdulrazaq, Fransic Mostafa huku pia Waganda Mathias Kigonya na James Sstuba; Mkenya Farouk Shikhalo; Mnyarwanda Ally Niyonzima na wengine kibao.

MFUMO: 3-5-2

Kocha: Francis Baraza

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz