Mnahesabu lakini? Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Yanga juzi kupata ushindi wa 21 katika michezo 25 iliyochezwa katikaa Ligi Kuu Bara.
Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa na kuifanya ifikishe jumla ya pointi 65 na sasa inahitaji pointi nane tu ili kutangaza ubingwa mapema.
Bao pekee la dakika ya 41 kupitia Joseph Guede liliifanya Yanga kuwa timu iliyovuna pointi na mabao mengi zaidi hadi sasa kulinganisha n timu nyingine 15 zilizopo katika ligi hiyo.
Watetezi hao wa ligi hiyo imefunga jumla ya mabao 56 kwa sasa, huku yenyewe ikifungwa mabao 11 tu katika mechi hizo 25, ikipoteza michezo miwili na kutoka sare mbili pia.
Jumla ya wachezaji 13 wa timu hiyo wameifungia timu hiyo mabao iliyonayo Yanga hadi sasa, huku Stephane Aziz KI akiwa ndiye kinara akifunga 15 na kuasisti saba, akifuatiwa na Maxi Nzengeli mwenye tisa na kusisti mbili, Mudathir Yahya akiwa wa tatu akifunga manane na kuasisti moja.
Pacome Zouzoua aliyerejea kwa sasa kutoka kwenye majeruhi ndiye anayefuta katika orodha hiyo, akifunga mabao saba na kuasisti matatu, kisha Joseph Guede anafuatia akiwa na mabao matano na asisti moja, huku Clement Mzize akiwa nyuma yake na mabao manne na asisti tano na Kennedy Musonda akifunga matatu na kuasisti moja.
Wengine walioifungia timu hiyo mabao ni Dickson Job, Hafiz Konkoni, Augustine Okrah, Skudu na Yao Kouassi ambao kila mmoja alifunga bao moja.
Hata hivyo, Kouassi akifunika kwa kuasisti mara saba, Nickson Kibabage (4), Jesus Moloko (3), Khalid Aucho (2), Konkoni, Okrah, Bakar Mwamnyeto na Joyce Lomalisa kila mmoja akiasisti mara moja.
Moloko na Konkoni waliondoka Yanga katika dirisha dogo, lakini mchango wao bado umesalia klabuni.
VINARA POINTI NYINGI
Katika pointi 65 ilizovuna katika mechi 25 za sasa, kuna klabu zilizochangia kwa kiasi kikubwa kwa watetezi hao kujiweka pazuri kutetea taji kwa msimu wa tatu mfululizo akiwamo KMC na Simba zinazochuana kileleni mwa orodha za timu zilizokuwa 'mama huruma'.
KMC ndio timu ya kwanza kuipa Yanga pointi sita na mabao manane, kutokana na kufungwa mechi zote mbili kwa mabao 5-0 na 3-0 mtawalia, huku Simba ikifuta nafasi ya pili kwa kugawa pointi sita na mabao saba, kwani ilifungwa nje ndani kwa mabao 5-1 kisha 2-1 mtawalia.
Timu nyingine zilizofuata kwa kuipa Yanga pointi nyingi na mabao ni; Singida Fountain Gate iliyogawa pointi sita na mabao matano ikiwa ni ya tatu baada ya kufungwa 2-0 na 3-0, huku Geita Gold ikifuata kwa kugawa pointi sita pia na mabao manne kwa kulala 3-0 na 1-0 mtawalia.
Namungo ni timu ya tano kuipa Yanga pointi nyingi, ikigawa pia sita na mabao manne, ikifuatiwa na Mashujaa iliyogawa pointi sita na mabao matatu ikiwa ni ya sita na timu ya saba ni Wagosi wa Kaya, Coastal Union, iliyogawa pointi sita na mabao mawili kwani ilifungwa 1-0 nje ndani na timu ya nane kuipa Yanga alama nyingi ni JKT Tanzania iligawa nne n mabao matano kwani ilifungwa 5-0 ktika mechi ya mkondo wa kwanza na kugoma ziliporudiana kwa kutoka suluhu
AZAM NA IHEFU WABISHI
Licha ya kwamba Azam ndio timu inayoshika nafasi ya 11 kwa zile zilizoipa Yanga pointi na mabao nyingi, lakini ni kati ya wabishi wawili waliwagomea watetezi hao kuzoa pointi zote katika mechi mbili za msimu huu ikiwamo Ihefu.
Azam iliyopoteza katika mechi ya kwanza mbele ya Yanga kwa 3-2 na kuipa alama tatu na mabao matatu, ilikataa kugeuzwa mteja kwa kuwafunga watetezi hao 2-1 ziliporudiana ikiwa ni timu ya pili kuitibulia Yanga baada ya Ihefu iliyoshinda ktika mchezo wa kwanza pia kwa mabao 2-1.
Hata hivyo, Ihefu ililegea iliporudiana na Yanga kwa kufumuliwa mabao 5-0 na kufanya iwe miongoni mwa timu zilizoipa wababe hao mabao mengi kwani iligawa sita, licha ya yenyewe kupata mawili, wakati Azam imeenda ngoma droo kwa kufungwa mabao manne na kufunga manne.
KAGERA SUGAR NOMA
Wakata Miwa wa Kagera Sugar ni kati ya timu tano pekee ambazo bado hazijarudiana na Yanga katika msimu huu, lakini yenyewe ikiwa ni kiboko kwa kugoma kufungwa bao lolote, licha ya kuipa Yanga alama moja kwa kutoka suluhu.
Mashabiki wa soka wanasubiri kuona kama Kagera itashikilia bomba pale zitakaporudiana jijini Dar es Salaam, lakini ndio timu pekee iliyoonyesha kuwadindia Yanga hadi sasa ikigoma kabisa kutoa pointi tatu kama ilivyo kwa timu zingine hata zile zilizocheza na Yanga mara moja kwa msimu huu.
Kagera ndio inayoonekana kuwa bora zaidi kuliko hata Azam na Ihefu zilizoshinda mechi za nyumbani na kupoteza ugenini, kwani Wakata miwa hawafungwa bao lolote zaidi ya kutema pointi moja.
Timu nyingine zilizoipa Yanga pointi tatu katika mechi za kwanza na kusubiriwa kuona kama zitajibu vipi zitakaporudiana, ni Tabora United na Dodoma Jiji zilizofungwa bao 1-0 kila moja, huku Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar zenyewe zimetema pointi tatu na kuipa Yanga jumla ya mabao sita, kwani Mtibwa ilipoteza kwa mabao 4-1, huku maafande wa Prisons ikilala 2-1.
UTAMU ZAIDI
Katika mechi 25 ilizocheza Yanga na kuiweka kileleni, lakini rekodi zinaonyesha vinara hao wameruhusu mabao katika mechi tisa pekee, huku 16 ikigoma kwa kupata clean sheet zilizomfanya kipa Diarra Djigui kuwa kinara kwa sasa akiwa na 12 akiwafunika makipa wa timu nyingine 15.
Mechi ambazo wapinzani walizigusa nyavu za Yanga ni zile za Simba na Azam kwani nyumbani na ugenini hazikuwa na clean sheet.
Nyingine ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Tanzania Prisons pamoja na mechi moja moja dhidi ya Ihefu, Mashujaa na Namungo, huku mechi 16 ilizocheza bila nyavu zao kuguswa ni dhidi ya JKT Tanzania, KMC, Geita Gold, Singida FG na Coastal Union kila moja zote mbili.
Pia zipo zile dhidi ya Namungo, Dodoma Jiji, Tabora United na Kagera Sugar pamoja na za marudiano dhidi ya Ihefu na Mashujaa.
MATOKEO YOTE YA YANGA
v KMC 5-0, 3-0 (pointi 6 mabao 8-0)- 1
v Simba 5-1, 2-1 (pointi 6 mabao 7-2)- 2
v Singida FC 2-0, 3-0 (pointi sita mabao 5-0)- 3
v Geita Gold 3-0, 1-0 (pointi 6 mabao 4-0)- 4
v Namungo 1-0, 3-1 (pointi 6 mabao 4-1)- 5
v Mashujaa 2-1, 1-0 (pointi 6 mabao 3-1)- 6
v Coastal Union 1-0, 1-0 (pointi 6 mabao 2-0)- 7
v JKT Tanzania 5-0, 0-0 (pointi 4 mabao 5-0)- 8
v Ihefu 1-2, 5-0 (pointi 3 mabao 6-2)- 9
v Mtibwa Sugar 4-1 (pointi 3 mabao 4-1)- 10
v Azam FC 3-2, 1-2 (pointi 3 mabao 4-4)- 11
v TZ Prisons 2-1 (pointi 3 mabao 2-1)- 12
v Tabora Utd 1-0 (pointi 3 bao 1-0)- 13
v Dodoma Jiji 1-0 (pointi 3 bao 1-0)- 13
v Kagera Sugar 0-0 (pointi 1 bao 0)- 15