Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Cheki mambo magumu anayopitia Rashford

Marcus Rashford England.jpeg Cheki mambo magumu anayopitia Rashford

Wed, 7 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Februari 2016, mashabiki wa Manchester United walimaliza kuangalia mechi ya Man United na Arsenal wakiwa na furaha mara mbili. Moja ilikuwa ni ushindi wa mabao 3-2. Pia walikuwa na furaha ya kupata mshambuliaji mpya, Murcus Rashford ambaye ndio ilikuwa mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England.

Rashford alifunga mabao mawili kwenye mechi hiyo na ripoti zikadai kwamba baada ya mechi kesho yake alikuwa na mitihani shuleni kwani bado alikuwa anasoma.

Taarifa zake zilisambaa dunia nzima. Kila mtu alimzungumzia yeye. Haikuwa rahisi kwa mchezaji kutoka kwenye kikosi cha pili kufunga mabao mawili tena kwenye mechi ya kwanza kubwa dhidi ya Arsenal.

Kila mtu alimzungumzia vile alivyoona kuwa ni sahihi. Wakati Rashford anafanya hayo, mshahara wake kwa wiki ulikuwa Pauni 2,000. Baadhi ya mashabiki wanadai ilikuwa kama pesa ya chakula au nauli.

Kutokana na kiwango alichoonyesha kwenye mechi hiyo baada ya hapo Man United ilimsainisha mkataba mpya na kuufanyia maboresho mshahara ambao ulipanda hadi Pauni 20,000 kwa wiki.

Walikuwa wanaweza kumpa hadi Pauni 50,000 au zaidi ya hapo lakini ilishindikana kwa sababu ya sera kutoruhusu. Daima Man United imejiwekea kuwa mchezaji mwenye umri mdogo na anayechipukia anatakiwa apewe pesa kidogo kidogo kwa sababu ukimpa nyingi huenda zikaua kipaji chake.

Lakini baada ya kupandishwa Van Gaal hakudumu. Akaondoka. Wakaja makocha mbalimbali ambao nao hawakukaa zaidi ya miaka minne. Waliondoka kutokana na matokeo mabovu ya timu.

Staa huyo malezi yake kwa kiasi kikubwa yamekuwa ni kwa mashabiki ambao kwao wanamuona ni mchezaji muhimu na tegemeo kwenye timu.

Hajapata nafasi ya kukaa na kocha mmoja kwa muda mrefu akamjenga sawasawa. Hali hiyo imekuwa ni tofauti na jinsi ilivyowahi kutokea huko zamani wakati timu iko chini ya Sir Alex Ferguson.

Wachezaji wote bora walikuwa wakitii na kusikiliza kwa sababu nguvu ilikuwa inatoka kwa mtu mmoja tu ambaye ni yeye. Alifahamu ni muda gani ukifika mchezaji yupi apate mshahara flani na muda gani asipate.

Sera ya wachezaji wadogo kutopewa pesa nyingi pia ilianzishwa na yeye.

Ferguson alifahamu fika ni vingumu wachezaji wenye umri mdogo kujizuia kwa kula bata sana na kufanya anasa ikiwa watapata pesa nyingi. Wale ambao walishindwa waliondoka na kuiacha Old Trafford.

Haikuchukua muda mrefu baada ya Rashford kupewa Pauni 20,000 alipanda haraka hadi kufikia sasa ambapo analipwa Pauni 300,000 kwa wiki.

Tofauti na wachezaji wa kigeni, mshahara huo wa Rashford hukatwa kodi kidogo tu - asilimia kubwa ya pesa yake huingia kwenye akaunti bila mashaka.

Katika kipindi hicho ambacho wachezaji wa Man United wanaonekana hakuna wanayemhofia sana kwenye kikosi kwa sababu ya pesa wanazopata ilikuwa ni rahisi kuyafanya haya.

Muda mwingi staa huyo ameishi na walimwengu kuliko makocha, tofauti na kaka zake waliomtangulia kama Ryan Giggs, Paul Scholes na wengineo ambao sehemu kubwa ya makuzi ya soka ilikuwa kwenye viganja vya Sir Ferguson.

Inawezekana akawa anapitia changamoto nyingi nje ya uwanja ambazo zinasababishwa na watu wake wa karibu, lakini hawa pia ndio walimwengu wenyewe.

Ilikuwa ni ngumu kwao kudanganya wanaumwa kwa sababu walifahamu muda wote Ferguson angewasili wanapoishi. Ilikuwa ni ngumu kwao kudanganya wapo Manchester kumbe wamesafiri nje kwa sababu walifahamu ‘babu’ huyo muda wowote angeweza kutaka kuwaona.

Lakini kumekuwa na urahisi kwa Rashford kufanya atakacho kwa sababu walimwengu ndio wamemlea kwenye soka na sio watu wengine.

Anafahamu angeenda huko alikokwenda na kusingekuwa na mtu yeyote au kocha wake angekwenda anapoishi, lakini hata ikigundulika ataachwa? Hapana.

Amepigwa faini tu ya Pauni 600,000 ambayo ni sawa na mshahara wake wa wiki mbili.

Ni ngumu kwa wachezaji aina ya Rashford kushindwa kufanya makosa ya aina hii kwa sababu anafahamu walimwengu wanaomlea wanamhitaji sana. Ukiwauliza mashabiki 10 wa Man United ikiwa auzwe au abaki nusu na robo pengine watakwambia abaki.

Kabla ya kufanya alichofanya hivi karibuni kwa kudanganya anaumwa na kushindwa kwenda mazoezini kisha kukosa mechi wakati alikuwa nchini Ireland anakula bata, na akarudi siku ya mazoezi. Aliwahi pia kwenda kujirusha saa chache baada ya kufungwa na Man City.

Kosa moja tu kati ya haya lingetosha kabisa kumpa funzo supastaa huyu kama ingekuwa anacheza zama za Man United ya Wayne Rooney na Cristiano Ronaldo lakini yupo kwenye zama za malezi ya walimwengu.

Mbali ya kufanya hayo, Rashford ataonekana tu baada ya kukosa mechi moja au mbili. Yeye mwenyewe anafahamu kwamba Man United haiwezi kuwa tayari kumkosa kwa muda mrefu.

MATATIZO NJE ya UWANJA, FAMILIA Mbali ya hayo, pia inadaiwa kwamba mojawapo wa sababu zinazomfanya supastaa huyo awe katika hali hiyo ni mazingira yaliyopo kwenye familia yake.

Rashford ambaye anapokea Pauni 375,000 kwa wiki ambazo ni zaidi ya Sh1.1 bilioni amekuwa akisumbuliwa na ndugu zake ambao wengi wanamtegemea.

Ndugu zake hao wamekuwa wakichukua kadi za benki na kutumia pesa zake vile wanavyojisikia na kila uchao wamekuwa wakimuomba pesa.

Mbaya zaidi ni kwamba wengi wamemzidi umri, hivyo inakuwa ngumu kuwa na kauli mbele yao na hiyo inachangia kumfanya staa huyo awe mtu wa kulewa sana pombe akiamini huenda anapunguza mawazo.

Pia kuachana na mpenzi wake Lucia Loi ambaye amekuwa naye tangu utotoni inadaiwa kuwa chanzo cha nyota huyo kutokuwa sawa kiakili, kiasi cha kupenda sana starehe ili apunguze mawazo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka The Sun, Rashford bado anampenda Lucia lakini dada huyo anaonekana kuwa mgumu kumsamehe na kuanza upya.

MAONI YA WACHAMBUZI

Mchambuzi wa soka wa Sky Sports, Chriss Sutton anasema anachofanya staa huyo hakisameheki.

“Wote tunafahamu kwamba ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, lakini amekuwa akitoka kwenye mstari katika siku za hivi karibuni,” anasema Sutton.

“Amefanya kosa la tatu, kila mchezaji anafahamu mstari gani hatakiwi kuuvuka na Rashford pia anafahamu, lakini aliamua tu kuvuka mstari. Alikuwa amewakosea wachezaji wenzake na kocha inaonekana ule utamaduni na nidhamnu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya Man United vimepotea kabisa.”

Mchezaji wa zamani wa Manchester United, Michael Richards anasema Rashford anatakiwa kufahamu kwamba ni kioo cha jamii, hivyo anapokwenda nje watu wote watakuwa wanamtazama. Anatakiwa awe makini sana.

Supastaa wa zamani wa Manchester United, Andy Cole kwa upande wake anasema Rashford anatakiwa ajitazame mwenyewe na kujitathmini juu ya vitendo anavyofanya ndani na nje ya uwanja.

“Nilishangaa baada ya kuona Marcus amejiingiza kwenye haya mambo tena. Wakati wetu ilikuwa hakuna haya mambo na hata kama mtu angekuwa ametoka usiku, basi kesho yake ilikuwa lazima awepo mazoezini,” amasema mkongwe huyo.

“Huwezi ukaenda kula bata usiku halafu ukarudi na kusema unaumwa, huwezi kuja mazoezini huko ni kukosa heshima.”

REKODI ZA rashford

Akiwa na Manchester United, Rashford amefanikiwa kucheza mechi 387 za michuano yote akifunga mabao 128 na kutoa asisti 74 katika michezo yote.

Nyota huyo amekuwa mfungaji bora wa michuano ya Europa League akiwa na mabao sita katika msimu wa 2022/23 ambapo pia alikuwa mfungaji bora wa michuano ya Carabao akitupia mara sita pia. Vilevile amewahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Man United msimu wa 2019/20.

Tangu apandishwe kucheza katika kikosi cha Man United amefanikiwa kushinda mataji manne - mawili ya Carabao, moja la FA na Europa League. Pia amewahi kuchukua Ngao ya Jamii 2017.

Chanzo: Mwanaspoti