Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Cheki dakika zao za moto AFCON

Stephane Aziz KI VS Diarra Cheki dakika zao za moto AFCON

Mon, 29 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zimenoga kwa sasa zikiwa katika hatua ya 16 bora huku mastaa kibao kutoka Ligi Kuu Bara wakiwa wamekiwasha kwenye hatua ya makundi. Msimu huu Ligi Kuu Bara imetoa wachezaji 17 walioshiriki michuano hiyo wakiwa na timu za mataifa tofauti.

Wengi wameaga mashindano baada ya mechi za hatua ya makundi kumalizika na sasa wamebaki watatu wanaopeperusha bendera ya ligi hiyo katika michuano hiyo inayoendelea Ivory Coast.

Aziz Ki akiwa na Burkina Faso, Henock Inonga yupo na DR Congo na Djigui Diara aliye na Mali ndio waliopenya hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.

Hata hivyo, haikuwa kinyonge kwa mastaa wa Ligi Kuu katika michano hiyo na kupitia makala haya, hizi hapa ni dakika walizowakilisha nchini Ivory Coast

DJIGUI DIARRA

Ni kipa ambaye hakuna aliyekuwa anatarajia kwamba ataweza kucheza dakika zote kwenye mechi za makundi ya michuano ya Afcon kutokana na kuwa kipa wa ziada, lakini amekuwa bora na kusimamia lango la Mali.

Katika mechi za makundi ilizocheza Mali, Diarra amecheza zote kwa dakika 90 akiruhusu bao moja. Alianza dhidi ya Afrika Kusini timu yake ikashinda mabao 2-0, dhidi ya Tunisia ikagawana nayo pointi kwa sare ya bao 1-1 na mechi ya tatu ilikuwa dhidi ya Namibia iliyomalizika kwa suluhu.

Diarra ambaye ni kipa namba moja wa Yanga ameivusha timu yake kwenda hatua ya 16 bora akitumika kwa dakika 270.

AISHI MANULA

Licha ya timu yake kuondolewa hatua ya makundi akiruhusu mabao manne kwenye mechi tatu za makunsi walizocheza kipa huyo alikuwa imara akicheza mechi zote akitumika kwa dakika 270.

Manula alianza dhidi ya Morocco akitunguliwa mabao 3-0, akaiongoza Stars kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia huku akilinda vyema lango dhidi ya DR Congo na kumaliza dakika 90 bila kuruhusu bao timu hizo zikigawana pointi baada ya suluhu.

MOHAMMED HUSSEIN 'TSHABALALA'

Beki namba moja wa kikosi cha Simba na timu ya taifa 'Taifa Stars' aliyecheza dakika 270 ikiwa ni baada ya kutumika kwenye mechi zote tatu za hatua ya makundi.

Licha ya kutumika kwa dakika hizo kwenye mechi za makundi, Tshabalala amekuwa mchezaji ambaye anacheza bila kuchoka kwani katika mechi tisa walizocheza za Ligi Kuu akiwa na Simba amecheza zote kwa dakika 90 na amekuwa bora.

IBRAHIM HAMAD 'BACCA'

Ni beki ambaye anajitengenezea ufalme wake mdogo mdogo ndani ya kikosi cha Stars na Yanga kuokana na ubora wake katika eneo hilo licha ya kutokuwa na muda mrefu tangu aanze kupata nafasi.

Bacca alijiunga na Yanga akitokea KMKM ya Zanzibar, ametua Jangwani akikuta ufalme wa Dickson Job na Bakari Mwamnyeto ambao pia walikuwa wakitumika Stars, lakini ameanza kumng'oa mmoja mmoja kila upande na kuanza kujenga himaya yake.

Bacca amemuweka benchi Job Stars akitumika kwa dakika 270 kwa kucheza mechi zote tatu kwa usahihi licha ya mchezo wa kwanza timu hiyo kuruhusu mabao 3-0 dhidi ya Morocco.

BAKARI MWAMNYETO

Nahodha wa Yanga na beki wa kutumainiwa Stars ametumika kwa dakika 270 akicheza michezo yote mitatu akiwa sambamba na Bacca ambaye amekuwa akicheza naye Yanga.

Wawili hao walikuwa na maelewano ya kutosha eneo la ulinzi Stars licha ya kuzingua katika mchezo wa kwanza ambao walimaliza wakiwa pungufu baada ya Novatus Dismas kuonyeshwa kadi nyekundu.

MUDATHIR YAHYA

Kiungo huyu amecheza dakika 65 kwenye mechi mbili akianza dhidi ya Morocco ambayo walikubali kichapo cha mabao 3-0 ambayo alicheza kwa dakika 45.

Mchezo uliofuata dhidi ya Zambia alianzia benchi na kuingizwa kipindi cha pili akichukua nafasi ya Himid Mao katika dakika ya 70, hivyo kufanya amalizie 20 za mwisho ambazo ziliipa Zambia nafasi ya kusawazisha bao katika dakika za jioni na kufanya mchezo umalizike kwa bao 1-1.

FEISAL SALUM 'FEI TOTO'

Hakuwa chaguo la kwanza kwenye mechi mbili za mwanzo zote akianzia benchi na kuingia kuchukua nafasi za waliomtangulia. Ubora wake kwenye dakika chache alizokuwa anapewa ulimpa nafasi ya kuanza mchezo wa mwisho dhidi ya DR Congo ambao pia hakumaliza dakika 90.

Katika mchezo dhidi ya Morocco ambao Stars ilikubali kichapo cha mabao 3-0 alicheza kwa dakika 21 akiingia kutokea benchi kuchukua nafasi ya nahodha Mbwana Samatta na mechi dhidi ya Zambia alicheza dakika 59 akianza na kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Morice Abraham.

Mechi ya mwisho dhidi ya DR Congo, kiungo huyu anayekipiga Azam FC alicheza kwa dakika 79 na kutolewa na nafasi yake ilichukuliwa na Kibu Denis ambaye anacheza Simba.

MZAMIRU YASSIN

Ni dakika 109 ndizo alizocheza kiungo huyu - akicheza dakika 90 dhidi ya Zambia Stars ikiambulia sare ya bao 1-1 na dakika 19 dhidi ya DR Congo timu yake ikitoka sare ya bao 1-1.

Kiungo huyu mkabaji uwepo wake eneo hilo ulichangia timu kuambulia pointi ambazo zimeandika historia kwani Stars licha ya kuwa ya mwisho kwenye msimamo ilipata pointi mbili tofauti na 2019 ambapo iliambulia pointi moja.

KIBU DENIS

Ametumika kwa dakika 81 katika mechi mbili alizopata nafasi ya kucheza hatua ya makundi akiwa na Taifa Stars. Alianza kucheza dhidi ya Zambia akicheza dakika 70 Stars ikiambulia sare ya bao 1-1.

Mechi yake ya pili ilikuwa ni dhidi ya DR Congo aliyoanzia benchi na kuingia dakika ya 79 kuchukua nafasi ya Fei Toto hivyo kumfanya acheze dakika 11 na kuisaidia Stars kuambulia sare.

CLATOUS CHAMA

Hana dakika nyingi kwenye kikosi chake licha ya ubora wake katika Ligi Kuu bara akiwa ametumika kwa dakika 21 kwenye mechi mbili za hatua ya makundi akikosekana kabisa kwenye mchezo mmoja na wa kwanza kwa Zambia.

Licha ya kucheza dakika chache, Chama ni chachu ya timu yake kuambulia pointi dhidi ya Stars baada ya kuingia akitokea benchi na kuchonga kona iliyopigwa kichwa na Patson Dhaka na kuzaa bao la kusawazisha.

Kiungo huyo mshambuliaji alicheza dakika saba dhidi ya Morocco na dakika 14 dhidi ya Stars, lakini timu yake hakwenda kokote kwani pia ilimaliza na pointi mbili kama Stars.

HENOCK INONGA

Uimara wake katika eneo la ulinzi kwenye kikosi cha Simba akiwa panga pangua katika kikosi cha kwanza ulimpa nafasi ya kuonekana na kuaminiwa na DR Congo - timu ambayo iliimpa nafasi ya kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Zambia wakiambulia pointi moja baada ya sare ya bao 1-1.

Ubora aliouonyesha ulimuaminisha kocha kumpa nafasi nyingine dhidi ya Morocco - mchezo ambao alicheza kwa ubora na kuisaidia timu yake kupata penalti licha ya kutokuwa na faida baada ya kukosa na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 huku beki huyo akitumika kwa dakika 45.

Inonga alicheza dakika 45 dhidi ya Morocco na kutolewa baada ya kuumia paji la uso na kufanya kutopata nafasi ya kucheza mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Tanzania ambao ulimalizika kwa suluhu, hivyo staa huyo wa Simba amecheza dakika 135. Timu yake ilitinga hatua ya 16 bora, na juzi iliiondosha Misri katika mchezo wa hatua hiyo.

KENEDDY MUSONDA

Ni mshambuliaji wa Yanga na timu ya taifa ya Zambia ambapo mchezo wa kwanza dhidi ya DR Congo hakuwa sehemu ya kikosi nchi yake ikiambulia sare ya bao 1-1.

Katika fainali hizo mshambuliaji huyo ametumika kwa dakika 34 kwenye mechi mbili za makundi - zote akianzia benchi. Mchezo wake wa kwanza dhidi ya Tanzania alicheza kwa dakika 14 akiingia kuchukua nafasi ya Kings Kangwa katika dakika ya 76, ambapo alichangia timu yao kusawazisha bao.

LUSAJO MWAIKENDA

Huyu ni beki wa kutumainiwa wa Azam FC na ni miongoni mwa mastaa 27 walioiwakilisha Tanzania kwenye Afcon ambayo ilimaliza nafasi ya mwisho katika Kundi F baada ya kukusanya pointi mbili.

Mwaikwenda alikuwa mmoja wa wachezaji 11 waliocheza mchezo dhidi ya DR Congo akitumika kwa dakika 90 na kuisaidia Stars kuambulia pointi moja.

Dakika alizocheza kwenye mchezo wa mwisho ndizo zilizotosha kwa upande wake baada ya mechi mbili za kwanza kukosa nafasi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live