Baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba SC akitokea Coton Sports ya Cameroon, beki Che Malone Fondoh amefunguka akisema amekuja kwa ajili ya kuwapa furaha Wanasimba.
Malone aliyeibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Cameroon kwa msimu uliopita ni miongoni mwa nyota waliosajiliwa Simba SC, kwa kulazimika kuvunja mkataba ili kutua Msimbazi.
Simba SC imetambulisha wachezaji wengine wapya wa kigeni, mshambuliaji Willy Onana (Cameroon) aliyeibuka mfungaji bora na mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Rwanda akiichezea Rayon Sports na winga wa Ivory Coast, Aubin Kramo kutoka Asec Mimosac.
Akizungumza jijini Dar es salaam kabla ya safari ya kuelekea Uturuki, Malone ameeleza furaha yake kujiunga na Simba SC, huku akiweka wazi kuwa na deni la kuwapa mafanikio Wanachama na Mashabiki wa Msimbazi.
“Nafurahi kujiunga na Simba SC, ni timu kubwa inayo mashindano fanya vizuri kwenye Afrika. Napaswa kujituma na kufanya vizuri zaidi ili nisiwaangushe bali kuwaheshimishe,”
“Simba SC ina wachezaji bora na wazuri, kwa kushirikiana tufafanya vizuri na kufikia lengo la klabu. Naamini katika umoja na kujituma kutatusaidia.” Amesema Che Malone
Katika hatua nyingine, beki huyo miaka mwenye 24, anayetarajiwa kutengeneza pacha ya ukuta imara wa Simba SC na Henock Inonga, amesema anaamini umoja, kujituma na ubora wa kikosi kizima ndiyo utaifanya klabu hiyo kuwa tishio zaidi kwa msimu ujao.
Katika hatua nyingine, Simba SC imewaongeza mkataba wa miaka miwili mabeki wake, Shomari Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, ambao watabaki Msimbazi hadi 2025.
Wakati Simba SC ikifanya hivyo, kikosi chake kinaondoka leo Jumanne (Julai 11) saa 5 asubuhi kwenda Uturuki kwa ajili ya kuanza kambi ya takribani majuma matatu kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya.