Nyota wa Pamba Jiji, Haruna Chanongo amewaonya mastaa wenzake wa kikosi hicho kutobweteka na ushindi walioupata katika michezo miwili mfululizo ya ugenini.
Chanongo alisema kikosi chao kimefanya vizuri licha ya kukutana na upinzani mkali huku akisisitiza ligi ni ngumu na ushindani ni mkali na kila timu inataka kupanda.
“Tusibweteke kwa hizi alama sita tulizopata tuendelee kujituma na kujitoa naamini mechi mbili za mwisho raundi ya kwanza tutakazocheza nyumbani, basi tutashinda, Wana Mwanza tuwatoe hofu kwa sababu kwa hizi mechi mbili za ugenini wenyewe wameona kitu gani tumefanya,” alisema Chanongo na kuongeza;
“Naamini kwa jinsi tulivyocheza ugenini tukijituma kama vile naamini tutashinda na mashabiki wetu watafurahi kwa matokeo tutakayopata hapa nyumbani.
Mchezo dhidi ya Polisi ulikuwa mgumu kwa sababu wachezaji wao wengi wametoka Ligi Kuu na wengi tunafahamiana.”
Pamba iliichapa FGA Talents bao 1-0 na kuibamiza Polisi Tanzania 1-0 na kupaa hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Championship ikifikisha pointi 27 baada ya michezo 13 sawa na Biashara United iliyo nafasi ya pili huku Ken Gold ikiwa kileleni na alama 29.
Kuhusu kiwango chake na siri ya kudumu muda mrefu katika, nyota huyo wa zamani wa Simba na Mtibwa Sugar, alisema ni kujituma na kujitambua huku akishauri nyota wanaochipukia kujitunza na kutambua malengo yao.
“Wana Mwanza walikuwa na shauku ya kuiona timu yao ikiwa katika nafasi bora kupitia mchango wangu kwahiyo viongozi walipoweka ofa mezani haikuwa ngumu kukubaliana nayo niliamini mchango wangu utaongeza nguvu kwa timu ya Pamba.” alisema