Bondia Yusuf Changalawe amefanikiwa kutinga RoboFainali Michezo ya Afrika (All Africans Games) inayoendelea nchini Ghana baada ya kumshinda Abdelgawwad Orabi Salah wa Misri kwa pointi katika pambano la uzito wa Light Heavy usiku wa Jumapili ukumbi wa Bukom Arena Jijini Accra.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya ndondi za Ridhaa inayojulikana kama Faru Weusi wa Ngorongoro anakuwa bondia wa pili tu wa Tanzania kutinga Robo Fainali baada ya Ezra Paulo Mwanjwango aliyemtoa William Mohamed wa Shelisheli kwa RSC (Refa Kusimamisha Pambano).
Salah ndiye bingwa wa All African Games iliyopita iliyofanyika Jijini Rabat nchini Morocco mwaka 2019 na ndiye aliyemshinda Changalawe kwa pointi katika Michezo ya Kufuzu Olimpiki ya Paris 2024 kwa Bara la Afrika walipokutana katika pambano la fainali Septemba mwaka jana Uwanja wa Dakar Arena Jijini Dakar, Senegal.
Changalawe alicheza pambano lake kwa ustadi wa hali ya juu sana na kusikiliza vizuri maelekezo ya walimu wake na kufanikiwa kumthibiti mpinzani wake huyo ambaye ameshafuzu kushiriki mashindano ya Olimpiki ya Paris 2024 kwa mara yake ya pili baada ya Olimpiki ya Tokyo, Japan 2020.
Katika hali ya kushangaza baada ya matokeo kutangazwa, Mmisri huyo alitumia muda mrefu kuduwaa ulingoni akiwa haamini kilichomtokea.
Sasa Changalawe atakutana na Bondia kutoka Equatorial Guinea katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Afrika Accra 2023.
Haikuwa siku nzuri kwa bondia wa kike, Zulfa Macho aliyepoteza kwa pointi katika Robo Fainali dhidi ya Gisele Nyembo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) uzito wa Fly.
Zulfa anakuwa bondia wa tatu wa Tanzania kuondoshwa kwenye michuano hiyo baada ya Abdallah Mafaume ‘Nachoka’ aliyetolewa na Gerald Kabinda wa Zambia kwa pointi uzito wa Welter Hatua ya 16 Bora na Abdallah Abdallah ‘Katoto’ aliyetolewa na Wibshet Bekele wa Ethiopia wote Hatua ya 16 Bora.
Abdallah Abdallah ‘Katoto’ alikuwa anaongoza vizuri pambano lake hadi raundi ya mwisho, lakini akalazimika kujiuzulu akufuatia kuvunjika mkono.