Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Champioship ni vita kupanda Ligi Kuu

Prisons Vs JKT Champioship ni vita kupanda Ligi Kuu

Mon, 23 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kumekuwa na vita kali kwa timu za Ligi ya Championship zikipigania vikumbo kupanda Ligi Kuu msimu ujao ambapo juzi ligi hiyo iliingia raundi ya 16, vinara JKT Tanzania wakizidi kuonyesha kuwa safari hii wamepania kurudi, waliposhinda ugenini mabo 3-2 dhidi ya Copco.

Mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na kuwafanya maafande hao kufikisha pointi 37 wakiendelea kutesa kileleni, huku wapinzani wao kwenye vita hivyo, Kitayosce wakiangukia pua baada ya kutandikwa mabao 2-1 dhidi ya Pan African, mechi ikipigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kutokana na kipigo hicho, Kitayosce inabaki na pointi zake 35, ikizidiwa alama mbili na vinara JKT Tanzania, huku ikisalia kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo.

Pamba, timu kongwe nchini, imekwea hadi nafasi ya tatu ikifikisha pointi 31, baada ya kuidungua KenGold bao 1-0, mechi ikichezwa Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa, ikifufua matumaini ya kupanda moja kwa moja Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, au kwenda kwenye mechi za mchujo kuisaka nafasi hiyo.

Mbuni FC, timu ambayo iliongoza Ligi ya Champioship kwa raundi kadhaa za mzunguko wa kwanza, hivi sasa imeonekana kuchoka, kwani juzi pia ilipata kipigo cha mabao 2-1 kwa timu inayoonekana kuwa dhaifu kwenye ligi hiyo, Ndanda FC, mechi likipigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Matokeo hayo yamezidi kuiondolea matumaini Mbuni FC ya kupanda moja kwa moja Ligi Kuu, kwani imeshuka hadi nafasi ya sita ikiwa na pointi 24.

Timu ya Biashara United ikiwa kwenye Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara, iliiadhibu Fountain Gate bao 1-0, matokeo ambao yameishusha hadi nafasi ya nne timu hiyo inayotabiriwa kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live