Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Championship wachezaji hawalipwi

JKT TZ SQUAD Vinara wa Ligi ya Championship, Kikosi cha JKT Tanzania

Thu, 16 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Katika toleo lililopita tuliona jinsi ambavyo Ligi ya Championship inaendelea na timu kadhaa zimeshapigwa faini kibao na hadi sasa 20 milioni zimeshapatikana kutokana na faini tu, lakini pia tuliona jinsi timu ya Gwambina ilivyoivuruga ligi hiyo baada ya kujiondoa kwenye mashindano hayo.

Leo tunaendelea na sehemu nyingine ambayo inaeleza uhaba wa wadhamini unavyoathiri ligi hiyo, endelea...

UDHAMINI WA LIGI

Mwishoni mwa mwaka jana Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Almas Kasongo, akiwa jijini Mbeya alisema wamekamilisha makubaliano na Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa), kupitia mradi wa ‘Fifa Plus’ kutangaza mechi za Championship na First League na mapato kwenda kwenye klabu.

Pia, Kasongo ilielezwa tayari zipo zaidi ya kampuni mbili ambazo mazungumzo yako hatua za mwisho kuweza kudhamini Ligi ya Championship na muda wowote baada ya makubaliano zitatangazwa.

Mtendaji huyo alisema mamlaka hizo kwa ushirikiano mkubwa zinachukua hatua za makusudi kuhakikisha wanazisadia timu za Championship na First League kuwa na udhamini, huku akizitaka timu kuanza kujipambania kwanza.

Ikumbukwe aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Boniface Wambura alikiri moja ya vitu vinavyofanya uendeshaji wa Ligi ya Championship kuwa mgumu ni kukosekana kwa wadhamini sababu timu nyingi zinashindwa kujiendesha kwa kukosa pesa.

“Tatizo linaanza kwenye timu zenyewe hazina uthubutu wa kutafuta wadhamini, kwani zikishapanda zinashangilia baada ya kuanza kufanya mpango ya kutafuta watu wa kuwekeza japo kwa sasa kuna mwamko.

“Dhana ya udhamini lazima watu wajue, inahitaji ushawishi mkubwa ili mdhamini aone anapata kitu, hata uamuzi wa kusema mwenyeji achukue mapato ilikuwa ili naye aweze kuhamashisha kwa upande mwingine, lakini utakuta watu wanasema ligi hii ni ya bodi na kujisahau mwenyeji ndiye anayewajibu wa kulinda kila kitu kwenye mchezo,” alisema Wambura akiwa mtendaji wa TPLB.

Kiongozi huyo alisema ligi inahitaji fedha ili kuendeshwa na haiendeshwi kutokana na mapato ya mlangoni na hapohapo kuna timu za Ligi Daraja la Kwanza (Championship) na Ligi Daraja la Pili (First League) ndizo zinazonufaika zaidi lakini zipo nyuma katika kusaka udhamini binafsi.

JANGA KUBWA

Baraka Orogo aliyekuwa Mwenyekiti wa Biashara United anasema baada ya timu kushuka daraja mdhamini mkuu wa timu hiyo aliachana nayo na ilikuwa changamoto kubwa kwasababu timu nyingi zinajiendesha kwa mifuko ya watu binafsi.

“Timu ikikosa udhamini ni janga kubwa sana japokuwa tulikuwa na kikao na TFF ambapo walikuwa wanapambana kutafuta mdhamini wa ligi lakini hilo linaonekana bado halijafanikiwa.

“Ligi ya Championship inakosa ushindani kwa sababu ya ukata maana timu nyingi zinajikokota na ukiangalia timu zinazojiweza ni hizi za jeshi mfano JKT Tanzania lakini hizi nyingine 90% hazina uwezo.”

Orogo anaongeza changamoto kubwa ni timu kushindwa kumudu kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine, ndicho kilio kikubwa kwao katika kutekeleza majukumu.

Mmoja wa viongozi wa African Sports ambaye hakutaka kutajwa jina lake anasema hali ni tete zaidi sababu timu haina uhakika wa kesho yake kutokana na ukata.

“Kweli tuliweka bajeti ya msimu mzima ambayo ilikuwa zaidi ya Sh100 milioni lakini hatuna vyanzo vya mapato zaidi ya kutegemea wadau na viingilio vya milangoni.”

Hata hivyo, timu nyingi ambazo zinaonekana zina wadhamini lakini wanakuwa wamedhamini jezi, malazi au usafiri lakini sio kutoa pesa ambazo zingetumika kwenye usafiri na kuendesha timu.

Katibu wa Ndanda, Seleman Kachele anasema wao hawana udhamini ndio maana hata bajeti yao imekuwa ngumu kufanikiwa kupata kile walichokitarajia.

“Tungepata udhamini halafu ligi ingekuwa inaonyeshwa nina uhakika ligi ingekuwa na ushindani zaidi, hivyo kikubwa tunachokifanya ni kuongea na wadau.

“Tatizo ligi yenyewe haina udhamini, hivyo kama klabu tunatakiwa kupambana lakini tuwaombe TFF ambao ndio walezi wetu watusaidie kupata udhamini na kama itashindikana, basi ligi iendeshwe kikanda ili kuepuka hizi gharama.

“Ukiangalia kama Gwambina imejitoa na kutoa sababu zao lakini kikubwa tunachokabiliana nacho ni suala la ukata na niombe TFF dakika hizi iwe inaiangalia zaidi michezo hii ya mwisho,” anasema Kachele.

Katibu Mkuu wa Pamba, Johnson James anasema ipo haja kwa TPLB kuhakikisha ligi inapata mdhamini kama ilivyo kwa Ligi Kuu ili kuipa thamani zaidi ligi hiyo.

Makena anasema Copco haina mdhamini na inajiendesha kupitia mifuko ya viongozi ambao wanajichanganya pamoja na baadhi ya wadau ndio chanzo kukubwa cha mapato ya timu.

Kirai anasema upande wa Gwambina awali walikuwa na wadhamini ambapo mwingine alikuwa akihusika na usafiri, mwingine bonasi za wachezaji na malazi.

“Inategemeana na ukubwa wa mdhamini lakini mwisho wa siku ugumu unakuja kwenye hela pekee ndio maana watu wanaiona Championship ni ngumu kwa sababu watu hawana kitu.

“Timu inapokuwa na udhamini mzuri hamuwezi kushindwa kitu, mtajisafirisha, mtapata vifaa na hata kuwalipa posho wachezaji kwa wakati lakini hii yote inashindikana kwa sababu ya ukata.

“Ukifuatilia vizuri kuna shida ipo sehemu kuanzia uongozi wa juu hadi huku chini kwenye timu ubinafsi wa watu kutaka kuona sehemu fulani kusiwe na timu na pia uongozi wa timu nao umeshindwa kuwa waaminifu kwa wadau ndio maana hawapo tayari kutoa pesa,” anasema Kirai.

WACHEZAJI HAWALIPWI

Orogo anasema walishindwa kuiendesha timu hiyo na sasa ipo chini ya moja ya kampuni mkoani humo ambayo inaisimamia.

“Timu ilitushinda kutokana na gharama hata wachezaji wetu tulikuwa hatuwalipi mshahara zaidi ya kuwapa posho lakini bado ikatushinda.

“Tulianza msimu kwa kuiweka kambini na kama unavyojua lazima walale na wale sababu walitoka sehemu tofauti, hivyo lazima wakae pamoja lakini tatizo bado likaonekana kuwa kubwa.

Anaongeza kama timu inashindwa kuwalipa posho wachezaji, wanakosa morali na hapo timu inakosa kupata matokeo mazuri.

Kiongozi wa African Sports (jina kapuni) anasema hakuna anayelipwa mshahara ndani ya African Sports na wachezaji wote wanalipwa posho nayo haina kiwango maalumu.

“Posho yetu inategemeana na kile tutakachokipata kwa mdau au viongozi wakijichanga ndicho tunachoweza kuwapa wachezaji wetu ili mambo yaweze kwenda.”

Chanzo: Mwanaspoti