Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Championship ina Mastaa wa Kimataifa

Papy Pic Papy Shishimbi

Tue, 9 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Uwepo wa baadhi ya mastaa wa kigeni waliowahi kutamba na klabu za Ligi Kuu Bara zikiwamo Simba, Yanga na Azam FC katika Ligi ya Championship (zamani FDL) umetafsiriwa na wadau, soka la Tanzania linazidi kupiga hatua kuanzia madaraja ya chini na sasa ziangaliwe kwa jicho pana.

Majina makubwa kama ya Papy Kabamba Tshishimbi, Deo Kanda waliopo Kitayosce, Amissi Tambwe, Tafazwa Kutinyu na Nicholas Gyan wanaokipiga DTB, wanaichangamsha ligi hiyo na kuleta ushindani mkubwa sambamba na wakongwe wa zamani waliotamba klabu kubwa nchini.

Mwanaspoti lilizungumza na wadau hao kwa nyakati tofauti na jambo kubwa waliloliona ni soka la Tanzania limepiga hatua, kinachowafurahisha zaidi ni ushindani uliopo kwenye ligi hiyo.

Kipa wa zamani wa kimataifa, Steven Nemes alisema “Tulishazoea kuona wachezaji wetu wanapotoka nje, wanachezea timu za madaraja ya chini na Ligi Kuu, sasa imekuwa hapa nyumbani, tunawaona Tambwe, Tshishimbi ambao bado wana mpira mwingi mguuni, hii ni hatua kubwa kwa soka letu.”

Mbali na Nemes aliyewahi kutamba na timu kadhaa nchini ikiwamo Nyota Nyekundu, Simba, Yanga na Majimaji, Kocha wa Yanga B, Said Maulid ‘SMG’ alisema “Tuna kila sababu ya kujivunia soka letu, kwa sababu huko chini kuna wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao wakicheza Ligi Kuu watafanya maajabu, hilo siyo jambo dogo, linaoonyesha namna tulivyopiga hatua.”

Mchezaji mwingine wa zamani wa Yanga, Tito Andrew alikazia hoja hiyo, akisema; “Tanzania imepiga hatua kubwa sana, wapenzi wa soka tushindwe wenyewe, Ligi Kuu kuna burudani, ukienda Championship kuna burudani, sasa hapo tutake nini, ukiachana na hilo, timu ikipanda itaonyesha ushindani wa tofauti,” alisema Andrew.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz