Ligi ya Championship inaendelea kushika kasi ambapo leo itapigwa michezo mitatu katika viwanja mbalimbali huku mchezo wa mapema saa 8:00, kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam utaikutanisha Cosmopolitan ikicheza dhidi ya Transit Camp.
Pamba iliyotoka kufungwa mabao 2-1 mechi iliyopita dhidi ya Mbeya City itakuwa kwenye Uwanja wa Nyamagana kuikaribisha KenGold iliyoinyuka Copco 3-2 huku Mbeya City ikiendelea kusalia kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kucheza na Copco.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa michezo mitatu kupigwa ambapo Pan Africans iliyotoka kufungwa bao 1-0 na Transit Camp katika mechi iliyopita itacheza na Maafande wa Green Warriors iliyotoka sare ya 1-1 na Cosmopolitan katika Uwanja wa Uhuru.
Biashara United iliyoifunga Ruvu Shooting mabao 3-0 itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kucheza na Mbeya Kwanza iliyoshinda bao 1-0 dhidi ya Stand United huku TMA ikisalia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kucheza na FGA Talents.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa TMA, Ngawina Ngawina alisema wakati ikisalia michezo michache kumaliza mzunguko wa kwanza wao wataendelea kupambana kadri ya uwezo wao huku akitoa presha kwa wachezaji kuacha kuangalia msimamo ulivyo.
“Moja ya jambo kubwa ni kutotaka kuingia kwenye mtego wa kuanza kuangalia tulipo kwa sasa kwa sababu itatutoa mchezoni wakati ligi ndio kwanza tuko mzunguko wa 11, lengo hasa ni kuhakikisha tunawekeza nguvu kwenye kila mchezo,” alisema.
Ligi ya Championship imeendeleza moto uleule ikishuhudiwa vigogo vikipapatuana na timu changa kuwania kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao.