Kiungo wakimataifa wa Simba, Clatous Chama amevunja ukimya na kuwatoa hofu mashabiki wa wa timu yake baada ya kuweka wazi kuwa kilichosababisha asisafiri na timu kuelekea Dodoma ni maumivu ya kifundo cha mguu aliyoyapata Dubai
Kiungo huyo raia wa Zambia alitolewa nje dakika ya 30 ya kipindi cha kwanza katika mchezo dhidi ya Mbeya City, baada ya kusumbuliwa na maumivu ya mguu, jambo ambalo liliwatia hofu mashabiki na kuhisi kwamba hana maelewano na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertonho’.
Chama kwa sasa anaongoza kwa kupiga pasi za mwisho kwenye timu hiyo na ligi kwa ujumla, baada ya kutengeneza pasi 12 na kufunga mabao manne kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, kitu ambacho kimesababisha mashabiki kutamani kuona akibaki uwanjani muda wote wa mchezo.
Akizungumza na HabariLEO, kiungo huyo amesema kuwa amebaki Dar es Salaam kwa ushauri wa daktari baada ya kushauri kufanyiwa uchunguzi kwenye maumivu yanayo msumbua ili kujua ukubwa wa tatizo hilo mapema.
“Ukweli sina tatizo na kocha, Robertinho na hata alivyonifanyia mabadiliko sikuwa nimechukia nilikwenda ndani kuvua kiatu sababu nilikuwa nahisi maumivu makali,” alisema Chama.
Kiungo huyo ameeleza kuwa maumivu hayo aliyapata kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya CSKA Moscow uliofanyika Dubai, ambako Simba ilipiga kambi ya siku saba kwa mwaliko wa Rais wa heshima Mohammed Dewji ‘MO’.
Alisema anaamini maumivu hayo hayatakuwa makubwa sana na hiyo nikutokana na timu ya madaktari kumpa huduma nzuri ambayo anaamini haitomweka nje kwa muda mrefu zaidi ya wiki au wiki na nusu.
Chama ameeleza kuwa bado anaamini timu yake inayo nafasi ya ubingwa licha ya kuzidiwa kwa pointi sita na watani zao Yanga wanaoongoza ligi hiyo kwa sasa wakiwa na pointi 53.