UMEWAHI kumwona mwanadamu analia huku moyo wake unacheka? Umewahi kumwona mwanadamu anacheka huku moyo wake analia? Huwa inatokea mara nyingi tu, lakini ni vile Lady Jay Dee aliwahi kutuambia tusiusemee moyo.
Namna Clatous Chama anavyowachanganya Wanasimba. Kila kitu kilikwenda mrama wakati alipokaribia kufungiwa na Simba. Kila kitu kikaenda mrama wakati alipofungiwa na Simba. Baada ya hapo kila mtu akasubiri kuona matokeo.
Wakati mashabiki wakisubiri matokeo naamini asilimia tisini ilikuwa sambamba na uongozi. Kwamba Chama ni msumbufu na hana nidhamu.
Hata hivyo, mioyo ya mashabiki na viongozi kisirisiri iligawanyika wakati hukumu ya Chama ikisubiriwa. Kuna walionuna na kutaka waachane naye. “Hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu”. Wakati mwingine mashabiki na viongozi usema hivyo mdomoni ingawa mioyo inasita.
Wiki zikapita Chama akaenda zake Afcon 2023. Huku ilipotoka Chama alikuwa amesamehewa. Haikujulikana kama Chama alikuwa ameisamehe klabu au klabu ilikuwa imemsamehe Chama. Vyovyote ilivyokuwa ni wachache tulidadisi kwa namna timu ilivyoonekana Chama alikuwa muhimu kabla ya pambano dhidi ya ASEC Mimosas Ijumaa hii.
Hapa katikati kulikuwa na mechi za ligi. Kilikuwa kipimo kikubwa cha kupima hasira za Wanasimba dhidi ya Chama. Mpira wake wa faulo ukaenda moja kwa moja katika nyavu za Azam. Lilikuwa bao la kusawazisha katika mechi ambayo Azam walitawala sehemu kubwa ya pambano.
Akafunga bao pekee dhidi ya JKT Tanzania pale Uwanja wa Isamuyo. Mpira ulijaa vyema katika guu lake. Alipewa muda na nafasi ya kufikiria. Usimpe Chama hivi vitu viwili atakudhuru. Na ndicho alichofanya. Kumbuka pia Chama aliupiga mwingi katika mechi dhidi ya Mashujaa, kisha Tabora United. Na sasa ameuacha mpira katika mikono ya watu wa Simba.
Kama angerudi halafu akafanya ovyo Simba wangeelekea kupata majibu rahisi kuhusu hatima ya Chama. Kile ambacho walikuwa wanakifirikiria wakati wanamfungia kingekuwa kinaendelea kupata ushuhuda kwamba Chama alikuwa anawahujumu. Ni hisia ambazo zipo kwa muda mrefu kwa Wanasimba kindakindaki.
Wakati ilipotangazwa kwamba amesamehewa wengi tulielewa kwamba viongozi walikuwa wamemuweka katika kipindi cha uangalizi kuelekea katika pambano dhidi ya ASEC Mimosas. Kwa Simba hii viongozi waliona wazi Chama alikuwa muhimu lakini kwa tabia zake walipaswa kumuonyesha ukubwa wao.
Lakini sasa Chama amegeuza kibao na ni kipimo cha pili kwao cha hasira dhidi ya Chama kuelekea mwisho wa msimu. Kipimo cha kwanza viongozi wamefeli. Kipimo cha kwanza kilikuwa kumsamehe. Wengi walihisi wakati ule alipofungiwa huenda ungekuwa mwisho wa Chama Simba.
Kipimo kile kilifeli na kimethibitika kufeli baada ya Chama kufanya makubwa baada ya kurudi klabuni. Ameonyesha kiwango ambacho hakina hujuma wala makandokando ndani yake. Kipimo cha pili cha hasira zao ni hiki hapa.
Kuelekea mwisho wa msimu na Chama atakuwa anamaliza mkataba wake Simba, je Wekundu wa Msimbazi watakuwa tayari kupambana na vigogo wengine kumpa Chama mkataba mpya?
Hili ni swali gumu. Kuna ugumu mwingi hapa. Baada ya kutokuamini Chama kwa muda mrefu bado Simba watatakiwa mezani kukaa naye kumuongezea mkataba. Sio kitu rahisi sana. Inawezekana Chama mwenyewe akawa ana hisia za Simba si wenzake tena kwa yote waliyotenda ikiwemo kumfungia.
Simba wakiamua kumuongezea mkataba Chama bado vita itakuwa ngumu pia. Kuna watani watakuwa wanasubiri kumuunganisha Chama na Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki na Maxi Nzengeli. Kwa sasa wanaweza kujifanya hawataki lakini ni wazi kama kuna klabu imewahi kumtamani Chama duniani basi Yanga inaongoza.
Wanamtaka kwa sababu mbili. Wanaamini katika ubora wake, lakini pili wanataka tu kuwaumiza.
Mchezaji kipenzi anapokatiza mtaa mmoja kutoka Msimbazi kwenda Jangwani au kutoka Jangwani kwenda Msimbazi basi roho huwa kwatu maradufu kwa watani ambao wanakuwa wameshinda vita.
Lakini katika umri wake, ukiachana na kupenda kushangiliwa na mashabiki wa hizi timu, Chama anataka pesa. Kuna Azam wanaangalia pambano hili wakiwa na noti za kutosha. Kama hautaamini kuhusu noti zao basi kamuulize ni kipi kilibadilisha akili za Fei Toto akaamua kuondoka Jangwani kwenda Mbande kule Chamazi.
Kama litakuja suala la pesa linalomuhusisha Chama sioni ambaye ana ubavu wa kupambana na Azam. Huwa wanashindwa katika siasa za mpira wetu lakini hawajawahi kushindwa katika suala la noti. Wangeweza kutengeneza timu yenye Fiston Mayele, Mohammed Hussein Tshabalala, Shomari Kapombe, Yao Kouassi, Chama, Pacome na wengineo kama suala lingehusu pesa. Kuna mtu ana wasiwasi na utajiri wa familia ya Bakhresa? Hakuna.
Sasa tukielekea mwishoni mwa msimu kiwango ambacho Chama amekionyesha tangu atoke Afcon nadhani ni kipimo cha hasira cha mashabiki wa Simba dhidi yake. Huwa wanamnunia kweli kweli wanapohisi amewakosea lakini kiwango chake huwa kinakonga mioyo yao.
Lakini viongozi huwa wanachukia kweli kweli wanapohisi Chama anawakosea lakini wanapokifiria kuona Chama akitambulishwa kwa mbwembwe na Haji Manara au Maulid Kitenge au Ally Kamwe katika kile kinachoitwa ‘Wiki ya Mwananchi’, huwa inatoa sura ya kuchukiza katika mioyo yao. Wanastahili kwa sababu Chama ni fundi wa mpira.
Sasa ni wakati wa kusubiri na kuona filamu hii ya Chama na Simba itashia wapi. Hadi sasa ipo sehemu nzuri ambayo kwa kweli hatuelewi kama ‘sterling’ wa mchezo mzima ni Chama au Simba wenyewe.
Ninachoweza kujua ni kwamba kuanzia sasa mpaka sasa hivi ni nyakati tete kwa Simba kumtunza Chama kama wataamua hivyo.
Mechi mbili za Simba zilizobaki katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika hatua ya makundi zitaendelea kutupa mwanga zaidi kuhusu hatima ya Chama na Simba, lakini mpaka sasa hivi Chama anaonekana kuongoza kwa pointi nyingi tangu arudi kutoka Ivory Coast.
Tatizo kubwa la soka la Afrika na pengine duniani kote ni kwamba wachezaji wanaoonekana kuwa hawana nidhamu ndio huwa wachezaji wenye vipaji na muhimu klabuni.