Achana na kiwango bora alichoonyesha nyota wa Simba, Clatous Chama kwenye mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, juzi, wakati timu yake ikiichapa Jwaneng Galaxy kwa mabao 6-0 na kufuzu robo fainali.
Unachotakiwa kujua ni kwamba staa huyo wa timu ya taifa ya Zambia amezidi kusogea juu kwenye msimamo wa wafungaji bora wa muda wote katika michuano hiyo.
Bao alilolifunga Chama katika mechi ya juzi dhidi ya Jwaneng limemfanya kufikisha mabao 22 katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kufika nafasi ya saba kwenye orodha ya wapachikaji mabao katika ligi hiyo, akimshusha Mbwana Samatta aliyefunga mabao 21 akiwa na TP Mazembe.
Mabao 22 ya Chama ameyafunga akiwa na timu mbili ambapo 18 aliyafunga akiwa na Simba na mengine manne ameyafunga akiwa na Zesco United ya nchini kwao Zambia.
Kinara wa kucheka na nyavu kwa muda wote kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni Mkongomani Tresor Mputu aliyefunga mara 39 akiwa na TP Mazembe, akifuatiwa na Mohamed Aboutrika wa Misri aliyefunga 31 kisha Muangola Flavio Amado aliyetupia 30, Mmisri Mahmoud El Khatib aliyefunga 28 na Emad Motoeb akitupia 24 wote wakifanya hivyo wakiwa na Al Ahly kwa nyakati tofauti.
Nafasi ya sita wapo Mtunisia Ali Zitouni aliyekuwa Esperance na Mzimbabwe Edward Sodomba aliyekuwa Dynamos, Al Hilal na Al Ahly wote wakifungana kwa kufunga mabao 23, kisha anafuata Chama katika nafasi ya saba.
Nafasi ya Nane ni Samatta aliyefunga mabao 21, huku Mmorocco Mouhcine Lajour aliyewika na klabu za Moghreb Tetouan, Wydad na Raja Casablanca na Mkongomani Dioko Kaluyituka aliyekuwa TP Mazembe wakifuata wakiwa na mabao 20 kila mmoja.
Hata hivyo, Chama ana nafasi ya kuendelea kupanda kwenye orodha hiyo kwani ndiye mchezaji ambaye bado anacheza Afrika na yupo kwenye orodha ya 10 bora, huku mwingine ambaye bado anacheza kwenye orodha hiyo ni Samatta anayekipiga PAOK ya Ugiriki. Wengine wote kwenye 'Top 10' tayari wamestaafu soka.