Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama ameamua au ana hesabu zake?

Clatous Chama Tabora.jpeg Chama ameamua au ana hesabu zake?

Thu, 8 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ushindi wa mabao 4-0 ambao Simba imeupata ugenini dhidi ya Tabora United jana kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, umemfanya kiungo wake Clatous Chama kugeuka gumzo.

Hiyo ni kutokana na mchango mkubwa ambao Chama aliutoa kwenye mechi hiyo ambapo alipiga pasi mbili za mwisho zilizozaa mabao ya Omary Jobe na Che Fondoh Malone.

Lakini mbali na pasi hizo za mwisho, Chama alikuwa mwiba kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha kwa kuvunja mistari ya ulinzi ya Tabora United na kufanya mashambulizi mengi likiwemo lile la kipindi cha kwanza ambalo aliwatoka walinzi wa wapinzani wao na kupiga mpira ambao uliokolewa na Said Mbatty wa Tabora United ukiwa unaelekea wavuni.

Kiwango hicho bora cha Chama dhidi ya Tabora United kimekuwa kama ni cha ghafla kutokana na nyota huyo wa Zambia kutokuwa na mwanzo mzuri katika msimu huu.

Kabla ya mechi ya jana, Chama ambaye anatajwa kama mmoja wa viungo wenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho, alikuwa na pasi moja tu iliyozaa bao jambo ambalo lilikuwa likiwashangaza wengi.

Hii inaweza kuibua hoja fikirishi ya nini ambacho kimechangia kiungo huyo kurudi na nguvu kubwa katika mechi hiyo dhidi ya Tabora United tofauti na kile alichokionyesha katika idadi kubwa ya mechi msimu huu.

Ikumbukwe mbali na kuwa na kikosi cha Zambia katika fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), Chama pia alikuwa na adhabu ya kusimamishwa na Simba kutokana na kile kilichotajwa utovu wa nidhamu.

Wakati wa dirisha dogo la usajili, Simba ilikuwa katika mpango wa kumuacha kiungo huyo lakini kutokana na kukosa mbadala wake waliamua kumbakisha kikosini.

Lakini pia ikumbukwe mkataba wa Chama na Simba umebakiza muda wa miezi mitano ili ufikie tamati ambapo utamalizika mara baada ya msimu huu kwisha.

Kuna mambo mawili yanayofikirisha hasa ukikitazama kiwango bora cha Chama katika mechi dhidi ya Tabora United.

Jambo la kwanza ni kwamba pengine Chama baada ya adhabu ya kusimamishwa ameamua kuwa mtoto mwema kwa Simba na anataka kurudisha heshima yake na Ufalme alioujenga kwa muda mrefu ambao umetetereka siku za hivi karibuni.

Ni wazi kwamba wapo Wanasimba wengi ambao walipunguza au kuondoa mahaba yao kwa Chama tofauti na ilivyokuwa zamani.

Lakini jambo la pili ni kwamba huenda Chama ameamua kupiga mpira mwingi kwa vile mkataba wake unaelekea ukingoni hivyo anatengeneza mkataba mzuri baada ya huu wa sasa kumalizika.

Kiwango hiki kinaweza kusababisha presha ya mashabiki wa Simba kutaka aongezewe mkataba mpya na kusahau yaliyopita lakini hata ikitokea inaamua kumuacha, maana yake ataondoka akiwa wa moto na ataenda kwingine na kupata fedha nyingi na heshima kama mchezaji muhimu na sio makapi.

Muda utatupa majibu kama Chama ameamua kuwa mtoto mtiifu kwa Simba au ana hesabu zake za maisha ya baadaye akiondoka kwenye timu hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti