Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama akabidhiwa Mechi ya Horoya

Chama Vs Vipers Clatous Chama

Thu, 16 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Uongozi wa Simba ukishirikiana na benchi la ufundi,umefanya kikao cha mchezaji mmoja mmoja na kupanga mikakati mizito ya namna ya kuifunga Horoya, huku kiungo wao Clatous Chama akikabidhiwa shoo ya Horoya Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Simba inatakiwa kupata ushindi kwenye mchezo wa Jumamosi, ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu kwa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na pointi tisa kibindoni.

Timu hiyo ambayo inatumia uwanja wake wa Mo Simba Arena uliopo Bunju jijini Dar es Salaam kwa mazoezini, ilianza kujiwinda na timu hiyo juzi jioni na jana muda huohuo.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka ndani ya kambi hiyo ambayo ipo kwenye usiri mkubwa ni kwamba uongozi pamoja na benchi la ufundi wamekuwa wakifanya kazi kubwa vikiwemo vikao mbalimbali ili kuhakikisha wanapata ushindi huo Jumamosi.

Kwenye kikao kilichofanyika juzi kiungo Chama alitumia muda mrefu kuzungumza na kocha Roberto Oliviera na staa huyo alikabidhiwa majukumu ya kuhakikisha timu hiyo inapata ushindi kwenye mchezo huo.

Kwa nini Chama? Ipo hivi, Roberto amepewa mafaili ya staa huyo namna alivyohusika na mabao ya ushindi kwenye mechi mbalimbali muhimu za michuano ya CAF, hivyo alilazimika kutengeneza naye mipango ya namna ya kuisaidia timu dhidi ya Horoya, lakini pia akiwapa majukumu na mastaa wengine.

Mwanaspoti linafahamu ujumbe mkubwa ambao kocha aliwapa mastaa, alitaka kila mmoja kujua ukubwa wa Simba na jinsi ambavyo mashabiki wanasubiri furaha ya ushindi kwenye mchezo huo.

Chanzo cha uhakika kutoka kwa mmoja wa kiongozi wa klabu hiyo kilisema kuwa pamoja na Chama kupewa kazi hiyo, lakini mbinu za mazoezini zimeegemea zaidi kwake.

"Kikubwa ambacho kocha amemwambia kila mchezaji kwa muda wake ni amani na furaha ya mashabiki wao ipo kwenye mchezo wa Jumamosi dhidi ya Horoya, hivyo amemtaka kila mmoja atathimini ukubwa wa Simba na thamani yake na kujua yupo ndani ya klabu hiyo kwa ajili ya nini, lakini akiwakumbusha kuwa Simba wamepenya kwenye nyakati kama hizi mara nyingi.

Aliongeza "Chama amekaa naye kwa muda mrefu zaidi baada ya kujua namna alivyohusika kuibeba timu kwenye mechi mbalimbali za mashindano hayo, ameona kuna haja ya kumuongezea ujasiri zaidi kujua kuna kitu mashabiki wanakitegemea kutoka kwake, lakini wakati mwingine alionekana kuongea naye hata mara nyingi wakati wa mazoezi, hata Baleke, Kapombe, Tshabalala, Manula na wengine wengi kocha na viongozi wamezungumza nao na sasa kinachosubiriwa ni wao tu kuonyesha moto wao kwenye dakika tisini."

Alipotafutwa kocha Roberto hakutaka kufunguka mambo ya ndani ambayo amezungumza na mastaa hao, isipokuwa alizungumzia kiufundi namna alivyoandaa kikosi chake na kuwaomba mashabiki kujitokeza kuwapa sapoti.

"Najua tuna mechi muhimu, benchi la ufundi lipo vizuri na najaribu kuwapa vijana nafasi ili waonyeshe uwezo wao wa kuisaidia timu dhidi ya Horoya, najua mashabiki wanahitaji furaha ya ushindi, hivyo ni jukumu letu kama makocha na wachezaji kwa ujumla kulitimiza hilo,"alisema.

Umuhimu wa Chama kimataifa akiwa na Simba

2018, SIMBA VS NKANA

Chama aliwapa raha mashabiki wa Simba baada ya kufunga bao la tatu dakika ya 88 timu hiyo ikishinda 3-1 dhidi ya Nkana ya Zambia, ambapo ugenini ilichapwa mabao 2-1, hivyo ikatinga hatua ya makundi CAF (Desemba 23, 2018).

2019 Mei 16, SIMBA VS AS VITA

Chama alifunga bao dakika ya 90 Simba ikishinda mabao 2-1, Uwanja wa Benjamin Mkapa, ilianza kuona lango As Vita dakika ya 13 akifunga Kazidi Kasengu, Mohamed Hussein 'Tshabalala' alisawazisha dakika ya 36, lakini ugenini Simba ilifungwa mabao 5-0.

2021, SIMBA VS FC PLATINUM

Februari 6, 2021 (Benjamin Mkapa), Simba ikishinda mabao 4-0 dhidi ya FC Platinum Chama aliyefunga la mwisho lililoipeleka timu hiyo hatua ya makundi, ugenini Wanamsimbazi walipoteza kwa bao 1-0.

2021, SIMBA VS VITA

Aprili 12, 2021 hatua ya makundi katika ushindi wa Simba wa mabao 4-1 dhidi ya AS Vita (Benjamin Mkapa), Chama alifunga mabao mawili dakika ya 45+1, 84 mengine yalifungwa na Luis Miqquisone dakika ya 30 na Larry Bwalya dakika ya 66 pia timu hiyo ilishinda bao 1-0 ugenini.

SIMBA VS BIG BULLETS

Simba dhidi ya Big Bullets, ikishinda mabao 2-0 ugenini dakika ya 30 Moses Phiri alifunga bao la tikitaka mpira wa kutenga ulianzia kwa Chama kisha Kibu Denis akaupiga kwa kichwa, huku bao la pili lililofungwa na John Bocco dakika ya 83 asisti ilikuwa ya Chama (Sept 10, 2022). Mechi ya marudiano ya Septemba 14, Simba ilishinda mabao 2-0 yakifungwa na Phiri, Chama alitoa pasi ya bao la dakika ya 29 na bao la pili lilifungwa dakika ya 50.

MSIMAMO WA KUNDI C

Kundi C Ligi ya Mabingwa, Raja Casablanca inaongoza kwa pointi 12, Simba nafasi ya pili ina pointi sita, Horoya pointi nne na Vipers pointi moja.

Chanzo: Mwanaspoti