Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama aitisha Simba mechi Ngao ya Jamii

Aziz Chama Pacome Yanga 2 Chama aitisha Simba mechi Ngao ya Jamii

Tue, 30 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga, Clatous Chama, ameonyesha furaha kubwa baada ya timu yake kutwaa Kombe la Toyota na kuvaa medali ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kujiunga nayo akitokea Simba, huku akisisitiza kuwa yeye na wachezaji wenzake wanataka kuchukua kila kombe na taji lililo mbele yao, kwani ni muhimu sana kwa mashabiki wao.

Akizungumza juzi nchini Afrika Kusini, baada ya kutamatika kwa mchezo maalumu ulioandaliwa na Klabu ya Kaizer Chiefs, Chama alisema kombe walilopata limezidi kuwapa morali ya kwenda kutwaa taji lingine lililopo mbele yao.

Agosti 8, mwaka huu, Yanga itacheza mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao wa jadi, Simba ambao ndiyo wenye taji hilo, mchezo ukitarajiwa kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mechi iliyochezwa juzi, Uwanja wa Bloemfontein nchini Afrika Kusini, Yanga iliisasambua Kaizer Chiefs mabao 4-0, mawili yakifungwa na Stephane Aziz Ki, kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Burkina Faso, Mzimbabwe aliyejiunga msimu huu akitokea Azam FC, Prince Dube na straika wa Kitanzania, Clement Mzize.

"Mchezo mzuri na mgumu, lakini baada ya kufunga mabao mawili ya haraka, mechi ikawa rahisi, unajua lengo letu ambalo sisi wachezaji tumejiwekea ni kwamba kila kombe au taji lililo mbele yetu kwetu ni muhimu tutalisaka na kulichukua, na hii ni kwa ajili ya heshima na faraja ya mashabiki wetu ambao wamekuwa wakitupa sapoti.

"Nawaahidi Kilele cha Wiki ya Mwananchi watafurahi sana, waje kwa wingi uwanjani," alisema Chama ambaye amejiunga na klabu hiyo hivi karibuni akitokea Simba na katika mechi hiyo aliingia akitokea benchini kutwaa nafasi ya Aziz Ki.

Kwa upande wa beki wa kati, Dickson Job, alisema kikosi chao msimu huu kimeongeza baadhi ya wachezaji ambao wana uwezo mkubwa, hivyo wana kikosi kipana na bora kuliko msimu uliopita, akitabiri kuwa huenda kitakuwa bora na mafanikio zaidi kuliko hapo nyuma.

"Mchezo ulikuwa mgumu, bado hatujawa vizuri sana kwa sababu huu ni mwanzo wa maandalizi ya msimu mpya, kikubwa tuliweza kuwabana na kutumia makosa yao kuweza kupata ushindi.

"Naamini kwa mechi hizi tatu tumeshaanza kupata muunganiko kati yetu na wachezaji wapya waliosajiliwa msimu huu. Naamini msimu ujao tutafanya vizuri zaidi kwa sababu kuna kikosi kipana chenye wachezaji bora ukilinganisha hata na msimu uliopita," alisema.

Yanga imemaliza mechi zake tatu maalum nchini humo, ikishinda mbili na kupoteza moja, ambapo ilichapwa mabao 2-1 dhidi ya FC Augsburg ya Ujerumani, mchezo uliochezwa Julai 21, kabla ya kushinda kwa bao 1-0 katika mchezo wa pili dhidi ya wenyeji TS Galaxy, Jumatano iliyopita.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: