Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama aipasua Simba, mabosi watoa msimamo

Chama X Robertinho.jpeg Chama na Robertinho

Sun, 22 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Simba kipo jijini Dodoma kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Bara usiku wa leo dhidi ya wenyeji Dodoma Jiji, lakini mashabiki wa klabu hiyo wameingiwa na ubaridi kutokana na taarifa za kutokuwepo kwa kiungo fundi wa mpira kutoka Zambia, Clatous Chama.

Mashabiki hao waliingiwa na ubaridi tangu siku ya mechi ya timu hiyo dhidi ya Mbeya City ambapo Chama alitolewa uwanjani dakika ya 33 ya mchezo huo wa ligi uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku akiasisti bao lililofungwa kiufundi na Saido Ntibazonkiza.

Licha ya Simba kushinda mchezo huo kwa mabao 3-2, lakini mashabiki waliondoka uwanjani wakiwa hawana furaha kutokana na kitendo cha Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kutoka Brazil kumtoa fundi huyo sambamba na nahodha, John Bocco aliyekuwa ameumia.

Lakini wamepatwa na mshtuko zaidi baada ya kikosi hicho kusafiri hadi Dodoma bila ya fundi huyo anayedaiwa ni kama yupo kwenye ‘mgomo baridi’, licha ya taarifa zilizotolewa na uongozi wa klabu hiyo kudai Chama anaumwa mafua.

Mwanaspoti lilidokezwa juzi jioni kwamba, Chama alifanya mazoezi ya timu hiyo asubuhi ya siku hiyo na kung’ara, alichomoa kuambatana na timu kwenda Dodoma kwa madai anajisikia kuumwa, japo benchi la ufundi lilijaribu kumbembeleza kuepuka kuleta sintofahamu kwa mashabiki.

Hata hivyo, mchezaji huyo alishikilia msimamo wake kidai anaumwa mafua makali na kubeba mizigo yake na kutimka kambini wakati wenzake wakienda Uwanja wa Ndege kwa safari hiyo ya Dodoma na saa chache baadaye uongozi ulitoa taarifa ya kukosekana kwa Chama na wenzake tisa.

Simba ilitoa taarifa kwamba Chama ni kati ya wachezaji 10 watakaokosa mchezo huo akiwa katika kundi la majeruhi akidaiwa kuugua homa na mafua, huku wengine wakiwa ni wanne wanaotumikia adhabu ya kadi tatu za njano ambao ni Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Joash Onyango na Pape Ousmane Sakho. Jonas Mkude yeye hayupo kambini tangu timu irejee kutoka Dubai, UAE.

Wengine ambao ni majeruhi na walioshindwa kuondoka na timu kwenda Dodoma ni; Henock Inonga aliyerejea mazoezini kutoka majeruhi akiungana na kina Peter Banda na Moses Phiri ambao walishaanza kujifua mapema tangu timu ikiwa kambi ya muda mfupi Mjini Dubai, huku Israel Mwenda ikielezwa ana matatizo binafsi.

Kitendo cha Chama kushindwa kuambatana na timu hiyo kinaelezwa sio kimewavuruga benchi la ufundi tu, lakini hata viongozi wa klabu hiyo nao wamegawanyika na kuhofia kuleta mpasuko kati ya wachezaji kwani hata wao wanaona kama mwenzao hayupo sawa kwa alichokifanya muda mchache baada ya mazoezi ya mwisho ya jijini Dar es Salaam.

Inaelezwa watu wa benchi la ufundi na hasa wanaoratibu safari hiyo walimbembeleza wakimtaka asafiri katika hali hiyo hiyo ya mafua kwani jina lake lilikuwa miongoni mwa waliokuwa kwenye msafara na maamuzi ya kuchezeshwa au la lingebaki kwa kocha kwa maelekezo ya daktari wa timu.

Hata hivyo, chanzo chetu kilifichua kuwa, Chama alishikilia msimamo wake kwa kuchukua vitu vyake na kuondoka kambini akiwaacha wenzake wakisafiri.

MBRAZILI AMEKAZA

Kocha mkuu mpya wa Simba, Robertinho alinukuliwa akisisitiza hana tatizo lolote na Chama na hatua yake ya kumtoa dakika ya 33 dhidi ya City haikuwa na sababu nyingine zaidi ya kutafuta ubora zaidi wa timu kutokana na kuhitaji watu wenye kasi hasa winga mchezoni.

“Sina tatizo lolote na Chama, ni mmoja kati ya wachezaji wangu bora ninaowaheshimu, nadhani ilihitajika kuwa vile kwani nilitaka tucheze kwa kasi zaidi ambayo Chama hakuwa nayo ili kushinda mbinu za mpinzani wetu, ilikuwa lazima nifanye vile.

Wengi wanajiuliza maswali juu ya Chama baada ya mabadiliko hayo kuondoka moja kwa moja hadi vyumba vya kubadilishia nguo, japo baada ya muda alirejea akiwa anachechemea ingawa hakuonyesha kupata matibabu yoyote ya madaktari wa timu hiyo kuthibitisha aliumia.

Tayari umeibuka mgawanyiko kwa kukosekana kwa Chama anayeongoza kwa asisti akipiga 13 na kufunga mabao matatu, ikianzia kwa mashabiki ambao bado wanajilazimisha kukubaliana na uamuzi wa kocha juu ya hatua yake ya kumtoa katika mchezo uliopita, japo uongozi wa Simba umemkingia kifua uamuzi wa Kocha Robertinho.

Bosi mmoja wa juu wa Simba (jina tunalo), aliliambia Mwanaspoti, uongozi upo upande wa kocha kwani yeye ndiye mkuu wa benchi la ufundi na ana uhuru wa kumtumia mchezaji anayemtaka kwa muda wowote anaoona unafaa kwa maslahi ya timu.

“Sisi kama viongozi wengi tuko upande wa kocha kwa maamuzi yoyote ya ufundi anayoyachukua, unajua tufike sehemu tujaribu kuheshimu taaluma za watu, kocha ameona huyu mchezaji kwa sasa hataweza kumudu mchezo ili timu ifanikiwe na alipofanya mambo yakawa sawa timu ikashinda, isingeshinda hapo tungesema kuna tatizo,” alisema bosi huyo wa juu ndani ya bodi inayomaliza muda wake na kuongeza;

“Sijaona kosa lililofanywa kwa Chama, nafikiri shida iko kwa mashabiki wetu tu ambao wanatamani mambo mengi ambayo mengine hayana nguvu sana kwenye timu nafikiri tutaishia hapo labda lije lingine.”

MSIKIE PAWASA

Nyota na nahodha wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa amesema inawezekana Chama ameharibiwa akili na upepo na maneno ya mashabiki baada ya kutolewa kwake katika mchezo uliopita kutokana na mashabiki bado hawajakubaliana na kutomuona kiungo huyo akiwa uwanjani.

Pawasa amemtaka Chama kukubaliana na uamuzi wa kocha kisha kutumia ukongwe wake kukaa chini na kocha na kuzungumza juu ya nini anakitaka kwake.

“Ukiangalia kwenye mchezo uliopita kocha alifaulu kwa maamuzi yake, lakini Chama anaonekana kuathirika na kelele za mashabiki wa Simba ambao wao wanachohitaji inawezekana kisiwe kile kocha anachokitaka kifanyike kwa mchezaji,” alisema Pawasa na kuongeza;

“Kocha Robertinho anaonekana ni kocha anayetaka falsafa ya soka la kushambulia moja kwa moja (direct football), falsafa kama hii inahitaji wachezaji wenye kasi ambao watakwenda kumfanya mpinzani kufanya makosa kwa haraka.

“Falsafa kama hii lazima mashabiki waelewe kuna vitu vitapungua kwa Chama, hakuna anayeweza kukataa ubora wake, nadhani hata kocha alisema lakini yapo maeneo atahitaji kitu tofauti, nadhani Chama kwa nafasi yake anaweza kukaa chini na kocha kisha akamuuliza kipi anataka akifanye ndani ya Simba, hapo atakuwa ameisaidia Simba na amejiweka katika maeneo huru zaidi.”

Hii sio mara ya kwanza kwa Chama kutofautina na makocha, Kocha Mhispania, Pablo Franco aliwahi kutibuana na nyota huyo wa kimataifa wa Zambia baada ya kumtoa katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga.

Chama alionekana kulalamika kwenye benchi na inadaiwa sababu hiyo ilichangia Pablo kuondolewa Simba. Kocha wa zamani wa Simba, Zoran Manojlovic ‘Zoran Maki’ aliwahi kudaiwa kuwakataa baadhi ya wachezaji wa Simba akiwemo Chama akidai hawana kasi na hawawezi kwenda na mfumo wake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live