Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama: Tulicheza pambano kwenye mvua kubwa

Rashid Idd (2).jpeg Chama: Tulicheza pambano kwenye mvua kubwa

Mon, 25 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yaani ilikuwa sisi tukishinda tunachukua ubingwa mbele ya KMKM kuna kitu kilichotokea uwanjani ambacho siwezi kukisahau. Mvua ya ajabu ilinyesha katikati ya uwanja na kutulowanisha sisi, huku mashabiki wote waliokuwa majukwaani walikuwa hawaloi licha ya kwamba uwanja ulikuwa wa wazi yaani haujafunikwa. juu.

Ndivyo anavyoanza kusema nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Rashid Idd ‘Chama’ mmoja ya wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa Stars wakati Tanzania iliposhiriki kwa mara ya kwanza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 1980).

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na gwiji huyo ambaye ameeleza mambo mengi juu ya safari yake kisoka na vituko alivyokutana navyo, lakini kubwa ni mvua ya ajabu waliyokutana nayo Pan Africans visiwani Zanzibar walipokuwa wakitwaa ubingwa mbele ya KMKM. Endelea naye...!

ALIKOTOKEA

Mkongwe huyo alianza kutamba kwa uwezo wake wa kusakata kandanda akicheza kama beki kuanzia miaka ya 1970 hadi miaka ya 1990 kupitia klabu mbalimbali zikiwamo Yanga, Pan Africans, Majimaji, Pamba, Ndovu FC pamoja na timu ya taifa.

Chama mzaliwa wa Tabora eneo la Ng’ambo, alianza kusakata soka akiwa katika Shule ya Msingi Miembeni kisha Sekondari  ya Kinondoni zote za jijini Dar es Salaam. Nyota yake ilianza kung’ara mwaka 1971 wakati alipokuwa akitumikia kikosi cha watoto katika timu ya Yanga kwa kipindi cha miaka 5 ambapo mwaka 1976 alisajiliwa rasmi kuchezea timu ya wakubwa ya Yanga.

Kutokana na umahiri wake mkubwa wa kucheza namba zote katika safu ya ulinzi alipata nafasi hiyo akiwa na umri wa miaka 17 ambapo bado alikuwa hajahitimu elimu ya msingi yani akiwa darasa la sita.

Gwiji huyo ambaye msimu uliopita aliipandisha Ligi Kuu Mashujaa FC ya Kigoma akiwa kocha lakini pia aliiwahi kuipandisha mara tatu AFC Arusha na hapa, analezea matukio mbalimbali ambayo hawezi kuyasahau enzi anacheza ambayo yanafurahisha na yenye funzo ndani yake.

ZALI LA YANGA

Anasema baada ya kucheza kwa muda katika timu ya vijana ya Yanga, mwaka 1976 uongozi wa timu hiyo ilifukuza wachezaji wote baada ya kugomea mazoezi ya kocha Tambwe Leya wakidai ni magumu ndipo akapata nafasi ya kupandishwa na nyota yake kung’ara.

“Ilikuwa ni timu mpya kwa sababu mashabiki wa Yanga walisema kwamba acha tuanze moja, acha tufungwe hata magoli 20 lakini wale wachezaji waliogoma wasirudi kwa sababu hawawezi kuwa wakubwa kuliko klabu.”

Anaweka wazi kuwa baada ya kupandishwa alijisikia furaha lakini moyoni alikuwa anasema amepandishwa kweli ataweza kupambana ila akajenga moyo wa ujasiri kwamba amepandishwa basi ataweza.

AGEUKA LULU

Anasema baada ya kupandishwa mechi yake  ya kwanza Yanga ilikuwa ya kirafiki dhidi ya TPC ya Moshi, kipindi hicho TPC ilikuwa ni timu kubwa sana, walicheza kwenye Uwanja wa Uhuru wakashinda magoli 4-1, akashangaa baada ya mechi mashabiki walikuja kumbeba na kumshangilia wakionyesha kuikubali shughuli yake uwanjani.

“Nilikuwa naishi Kurasini sasa wakati natoka kwenye mechi ile mashabiki njiani wakawa wananipa moyo sana wengine walikuwa wananiambia ile nafasi ni yako umeonyesha kitu kikubwa sasa usikate tamaa”.

DALADALA ZA MJINI BURE

Anasema baada ya kutoka Kurasini akawa anaishi Magomeni basi daladala zote zinazopita njia hiyo kwenda Kariakoo alikuwa anapanda bure kutokana na umaarufu wake na hakuwahi kutoa hela mfukoni kulipia usafiri.

“Yani ulikuwa unashtukia tu gari limesimama unaitwa kulikuwa na madereva teksi wengi ambao walikuwa wapenzi Yanga kwahiyo wakiona tu wanasimama nipande ili kuwahi mazoezini.

“Mimi nilishawahi kutoka Morogoro mpaka Dar bure kwenye basi kwahiyo si kwamba vitu hivyo vipo sasa tu, tangu zamani vilikuwapo na ilikuwa ni furaha kwetu na wale walevi sasa ndio usipime walikuwa wakiingia kwenye kumbi za starehe basi mpaka wanabebwa”.

YANGA, SIMBA MARA MOJA TU

Anaweka wazi kuwa wakati anacheza presha za mechi ya Dabi ilikuwa balaa kwani timu hizo kwani zilikuwa zinakutana kwa mwaka mara moja tu tofauti na sasa ambayo zinakutana mara mbili kwenye Ligi lakini pia inaweza kutokea wakakutana Kombe la Shirikisho za Azam Sports, Ngao ya jamii na Kombe la Mapinduzi.

Anasema sasa hivi Yanga na Simba zikiwa zinajindaa timu zote zinabaki katika kambi zao, tofauti na wakati wao ambao zilikuwa zinatoka nje ya mji utasikia mmoja kaenda Zanzibar, mwingine Morogoro.

“Sasa hivi wanacheza mara nyingi tofauti na kipindi cha nyuma enzi zetu tulikuwa tunacheza mechi moja tu kwa mwaka Yanga na Simba hapo ukifungwa ujue mpaka mwakani.”

“Hata mwamko wa zamani na sasa hivi ni tofauti kwa sasa watu wanachukulia kawaida kwasababu wanakutana kwenye ligi mara mbili, zamani mechi ni moja na ukifungwa unazomewa mwaka mzima una kuwa huna amani.”

ALIPIWA NYUMBA

Anasema wakati kiwango chake kiko juu kuna shabiki wa Yanga alimchukua akawa anaishi naye kwake Mwananyamala baada ya shabiki huyo kukataa kwamba Chama hawezi kuishi kambini na wachezaji wengine.

“Wachezaji wengine wa kigeni wa Yanga walikuwa wanakaa kambini yeye akasema huyu hawezi kukaa hapo nitakaa naye mimi basi akanichukua nikawa naishi silipi hata mia.”

MAYAI YA MGANGA

Chama anasema kuna mechi Yanga ilikuwa inajiandaa kucheza na RTC Kigoma waliweka kambi makao makuu pale Jangwani, wakati huo RTC ilikuwa imetoka kumfunga Simba goli 1-0, pale Uwanja wa Uhuru,mechi iliyokuwa inafuata ndio ikawa inawakutanisha wao.

Anasema ile homa ya mashabiki kuona kwamba hawa wamewafunga Simba na wao wasiwafanyie masihara ikafika siku moja kabla ya mechi wakafatwa mida ya saa sita za usiku na wazee ambao walikuja kumwamsha yeye na Allan Shomari.

“Tuligoma kwani Allan tulikuwa tunakaa naye chumba kimoja, ikabidi tuulizane tunaenda kufanya nini sasa hizi usiku badala ya kulala wakati kule watu walikuwa wakisema kisomo hakiwezi kuanza mpaka tutimie wote.

“Basi marehemu Juma Mkambi akaja kutubembeleza ikabidi tutoke, tukatoka tukateremka mpaka chini bwana kule chini nikakuta kuna trei mbili za mayai zimeandikwa Kiarabu nikamwambia kapteni sisi toka juzi tunadai mayai kwenye chai wanasema bado hayajafika sasa mbona hizi trei mbili kapelekewa mganga?

“Mimi nikaenda nikayakanyaga yakapasuka hali ya hewa ikaharibika pale vurugu ikawa sintofahamu, wachezaji si unawajua wakashangilia pale kila mtu akarudi chumbani kwake.”

Anasema baada ya hapo asubuhi taarifa zikawafikia uongozi kwamba Chama kavunja mayai ambayo yaliandaliwa kwa ajili ya kazi ya mganga huku akidai wao wakiulizia wanaambiwa hayajaletwa halafu mganga yeye anapelekewa basi wakaamua asimamishwe.

“Walisema sasa huyo si atasababisha timu ifungwe aondolewe kambini ilipofika saa tatu asubuhi tukapewa taarifa mimi na Allan hatutakiwi kambini. Wakati huo nilikuwa nakaa Ilala Bungoni tukaondoka.

“Kufika saa sita kocha wetu akatufuata akasema vipi bwana nasikia nyie mmeondoka tukamkubalia na kumweleza tumeondoka kwa sababu tumevunja masharti ya kambi akasema haiwezekani chukueni viatu vyenu twende klabuni kwa sababu wiki nzima mimi nilikuwa nawandaa ninyi halafu wewe Chama unajua kabisa upande wa kushoto tunakutegemea wewe.

“Akasema twendeni, kama kufukuzwa nitaanza mimi lakini nyinyi lazima mwende mkacheze, basi tukarudi klabuni. Ikatajwa timu mimi nikacheza namba tatu kwa sababu nilikuwa na uwezo wa kucheza kulia, kushoto, katikati.

“Basi tukaingia viongozi wakasema hii mechi tutafungwa kwa sababu hawa watu wamevunja masharti na mganga kakasirika kaondoka. Mimi sikujali, siku hiyo Mungu alinijalia nilicheza kama mlinzi wa kushoto na katika mchezo ule nilitoa asisti tatu kwa Edger Fongo ambazo alizifunga zote na tulishinda magoli 5-0.

“Mechi imeisha pale watu walishangilia sana mpaka viongozi ikabidi wajiulize mbona mganga kasusa lakini tumeshinda, kurudi kambini tukabadilisha jezi, mimi nikaondoka kurudi nyumbani. Kufika katibu akanifuata akatuomba msamaha.

“Akasema kumbe waganga wakati mwingine ni waongo sasa mbona kasusa yeye halafu timu imeshinda magoli mengi na wewe ambaye ulipasuapasua mayai ndio umetoa asisti tatu?”

Anaongeza aliwaambia wakati mwingine wawe wanaangalia kwasababu timu ni mazoezi, ni kujiandaa vizuri, haamini mambo ya ushirikina na tangu siku hiyo wakajua yeye katika vitu kama hivyo haitakiwi ashirikishwe.

“Mimi nilikuwa nikiitwa kwenye mambo kama hayo wala siendi na walikuwa wanajua kabisa na ikawa hivyo hawaniiti tena nilikuwa naamini ukijiandaa vyema kwa kufanya mazoezi unatoboa.”

Anasema katika muendelezo wake wa kutoamini ushirikina kwenye michezo aliwahi kupewa dawa kwenye mechi dhidi ya Simba aweke kwenye kiatu lakini yeye akatupa mchezo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Uhuru na Yanga ilishinda bao 1-0.

“Goli letu tulifunga mapema tu kona alipiga Omar Hussein ikamkuta Rashid Hanzurun kwenye posti ya pili mpira uliwapita watu wote ukamkuta yeye akaugusa ikawa ndio hilo hilo goli moja.

“Mimi nilikuwa siweki kitu kwenye kiatu wala kwenye soksi katika maisha yangu yote ya mpira, mama yangu aliniambia usikubali kuweka kitu chochote kwenye miguu yako wewe mwombe Mungu yeye ndo atakusimamia.

“Basi kabla ya mchezo nilipewa dawa niweke kwenye soksi nikatupa na bado timu ikashinda na ndio ilikuwa mechi ya kufuta uteja kwa Simba.”

JINA LATOKA MAZEMBE

Anasema jina ambalo limekuwa maarufu la Chama alipewa na mashabiki katika mchezo wa kirafiki wa Yanga dhidi ya TP Mazembe kwenye Uwanja wa Uhuru, Yanga ikishinda 2-1, baada ya kumdhibiti mshambuliaji hatari Lufumbo na hivyo walifananisha uchezaji wake na beki wa zamani wa timu ya Taifa ya Zambia, Dick Chama.

“Huyo mtu alikuwa ni hatari kwanza ana mwendo halafu alikuwa na mwili mkubwa, alitanguliziwa mpira fulani hivi akawa tayari ameshanizuia kwa mkono anaukaribia ule mpira ili afunge mimi nikapiga tackling hakuamini alikuja baadaye akauliza hivi yule mchezaji anacheza Ulaya au? Akaambiwa ni wa hapa hapa.”

MVUA YA AJABU

Anasema kati ya mechi ambazo hawezi kuzisahau ni ya Kombe la Muungano 1982 kati ya Pan African na KMKM ya Zanzibar, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, yeye akiwa anachezea Pan aliyojiunga baada ya kuondoka Yanga. Mchezo huo walishinda mabao 4-2.

Anasema kitu cha ajabu alichokiona ni mvua kunyesha lakini ikawa inanyesha uwanjani tu lakini majukwaani kwa mashabiki hapakuwa na kitu.

Anasema Pan African ilikuwa ya kwanza kuandika bao kupitia kwa Ali Katolila wakati mvua ikinyesha kitu ambacho kilikuwa cha ajabu siku hiyo kwani kila ikinyesha mvua Pan walikuwa wakiandika bao. KMKM wakapapatua na kuwasazisha bao lilifungwa na Mcha Khamis. Mvua ikasimama na iliponyesha tena Pan African wakaweka bao la pili mfungaji Mohammed Yahya ‘Tostao’. Mvua ikasimama na gemu kuendelea hadi Shaaban Ramadhan aliposawazisha na kufanya matokeo 2-2 na kwenda hivyo mapumziko.

Anasema kipindi cha pili walifunga magoli mawili ya haraka haraka yaliyowekwa wavuni na Peter Tino na Tostao baada ya kupokea krosi maridhawa kutoka kwa Ali Katolila na kupiga ‘bullet header’ iliyomshinda kipa Korosheni.

“Yani ilikuwa sisi tukishinda tunachukua ubingwa na KMKM akishinda anakuwa bingwa kitu ambacho siwezi kukisahau mashabiki wote ambao walikaa jukwaani walikuwa hawaloi mvua ilikuwa inanyesha pale katikati ya uwanja tu.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live