Habari njema kwa mashabiki wa Simba na Tanzania ni kwamba mastaa wote muhimu wa Mnyama unaowajua asubuhi hii watakuwa mazoezini kujiandaa na mechi ya Al Ahly iliyoingia mchemcheto mapeema.
Za ndani kabisa ni kwamba Ahly ilitanguliza mashushushu wao Dar es Salaam tangu wikiendi iliyopita ili kusoma mazingira na kuweka mikakati ambayo itawafanyia wepesi kwenye mechi ya Ijumaa jioni ya African Football League.
Ipo hivi: Mastaa sita wa kikosi cha kwanza cha timu hiyo ambao ni Clatous Chama, Henock Inonga, Kibu Denis, Mzamiru Yassin, Ally Salim, Israel Patrick Mwenda waliitwa timu zao za taifa, jambo lililokuwa likimuwia vigumu kocha, Oliveira Roberto 'Robertinho' kupangilia kikosi chake kuelekea mchezo huo muhimu.
Inonga ambaye alikuwa na timu yake ya Taifa ya Congo alijiunga kambini jana asubuhi, wakati Chama alitarajia kufika usiku, Mzamiru, Kibu, Ally Salim na Mwenda nao pia wapo kambini tangu juzi na jana jioni walikiwasha kwenye matizi Kwa Mkapa.
Keshokutwa Simba inaanza mchezo wake wa kwanza wa michuano hiyo yenye utajiri dhidi ya Al Ahly,hivyo imemrahisishia Robertinho kukipanga kikosi chake, tofauti na awali ambapo wachezaji hao walikuwa wanakosekana na wengi walitarajiwa kucheza michezo ya timu zao za taifa leo ndiyo waanze safari ya kuja Bongo.
"Ilibidi zifanyike harakati kubwa kuhakikisha kuwa wachezaji wote wanarejea kambini, kwa sasa sisi ni tupo kamili, kila kitu kinaenda vizuri na mashabiki wasubiri mziki mnene Ijumaa," kilisema chanzo cha ndani kutoka benchi la ufundi la Simba ambayo jana usiku walifanya kikao kizito Dar kuweka mikakati ya mwisho.
Jana kwenye Uwanja wa Mkapa kulikuwa na ulinzi mkali uliokuwa unawazuia shabiki kuangalia maandalizi ya mechi hiyo huku magari ya viongozi yakipishana, Simba walifanya mazoezi hapo usiku.
Wapinzani wao Al Ahly wanatua nchini leo tayari kuzoea hali ya hewa na kuweka mambo sawa tayari kwa michuano hiyo mipya.