Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama, Bocco wabebeshwa zigo Simba

BEF7D698 123C 4062 9A3F E57C9E044F94.jpeg Chama, Bocco wabebeshwa zigo Simba

Mon, 26 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Clatous Chama na John Bocco leo watakuwa na kibarua kigumu cha kuibeba safu ya ushambuliaji ya Simba wakati itakapokabiliana na KMC ugenini kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kuanzia saa 10:00 jioni.

Wawili hao katika siku za hivi karibuni ndio wamekuwa silaha ya ziada ya Simba katika kuipatia mabao pindi mshambuliaji tegemezi wa timu hiyo, Moses Phiri anapokosekana au akishindwa kufumania nyavu.

Phiri aliyeifungia Simba mabao 10 katika Ligi Kuu hadi sasa, atakosekana katika mchezo wa leo kutokana na majeraha aliyopata katika mechi iliyopita dhidi ya Kagera Sugar ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Wakati Chama akiwa tegemeo la Simba katika kupiga pasi za mwisho, Bocco yeye ndio amekuwa silaha ya pili ya Simba katika kufumania nyavu baada ya Phiri.Uthibitisho wa hilo ni katika mechi tano zilizopita za Ligi Kuu ambazo Simba imefunga jumla ya mabao 13, ambazo wawili hao wanamfuatia Phiri kwa kufumania nyavu, kwani kila mmoja amepachika mabao mawili, Bocco akipiga pasi moja ya mwisho na Chama akipiga pasi za mwisho nne.

Ni mechi muhimu kwa kila timu kuibuka na ushindi ambayo Simba ikivuna pointi tatu itafikisha pointi 41 na kuendelea kuzidi kujichimbia katika nafasi ya pili, wakati KMC ikishinda itafikisha pointi 25 zinazoweza kuipandisha hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi.

Kocha wa KMC, Hitimana Thierry alisema wamejiandaa kukabiliana na Simba leo.

“Tumetoka kufanya vizuri katika mechi mbili zilizopita na lengo letu ni kuwa na muendelezo mzuri wa kupata ushindi lakini tunakutana na timu nzuri yenye wachezaji bora hivyo tunapaswa kucheza kwa tahadhari kubwa. “Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huu tukifahamu hautakuwa rahisi na jambo la msingi ni kuhakikisha kile tulichokifanyia kazi mazoezini kinatekelezwa kwenye mechi,” alisema Hitimana.

Kocha wa Simba, Juma Mgunda alisema kuwa matokeo waliyoyapata dhidi ya Kagera Sugar hayajawafurahisha na watajitahidi kuhakikisha wanashinda leo.

“Tunajua tunakutana na timu nzuri ya KMC ambayo mechi ya kwanza tulitoka nayo sare. Kama timu tumejiandaa kukabiliana nao tukijua mechi itakuwa ngumu. Tunafahamu kwamba tunahitajika kupata ushindi katika mchezo huu, ili tuendelee kupambania ubingwa,” alisema Mgunda.

Timu hizo zinakutana zikiwa na mwenendo tofauti katika mechi za hivi karibuni za Ligi Kuu, ambapo Simba imeonekana kufanya vizuri kulinganisha na wenyeji wao KMC.

Katika mechi 10 zilizopita za timu hiyo kwenye Ligi Kuu, KMC imepata ushindi mara tatu, kutoka sare tatu na kupoteza mechi nne, ikifunga mabao manane na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane.

Simba yenyewe katika mechi 10 zilizopita za ligi, imeibuka na ushindi katika michezo saba huku ikitoka sare tatu, imefunga mabao 25 na imefungwa mabao manne tu.

Tangu KMC 2018/2019, timu hizo zimekutana mara tisa Simba imeshinda nane, sare 1.

Chanzo: Mwanaspoti