Mimi sio mbaguzi wala siwachukii wageni na pia naheshimu maono ya Taasisi katika biashara zao. Naheshimu maamuzi ya kibishara na nawaheshimu kaka na dada zangu waliopo kwenye nafasi za maamuzi katika taasisi mbalimbali.
Tumeamua kujificha kwenye kivuli cha wageni ya kwamba wao bora kuliko wazawa. Wazawa hawapewi muda wala heshima katika nafasi za majukumu haswa kutoka kwa vigogo wa Kariakoo.
Licha ya moyo na ubora wa Juma Mgunda lakini kaonekana sio kitu kaletwa mgeni, wachezaji wetu wengi wazawa hawapewi thamani licha ya ubora wao na wala hawapewi muda wa kujirekebisha.
Nimeona Clatous Chama na Aziz Ki wamekula shavu la ubalozi wa Bank, unaweza usione shida lakini mimi napata shida sana kulipokea hili swala. Aziz Ki anapataje Deal mbele ya Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Zawadi Mauya, Kibwana Shomari, Feisal Salum au mchezaji yeyote mzawa ndani ya Yanga..? Why this mentality ya wageni inapenya kila sehemu..?
Unamnyimaje mzawa Jonasi Mkude, Shomari Kapombe, John Bocco au Aishi Manula kisha unampa Clatous Chama na ugeni wake…? Yaani Chama ni Maarufu mitaani kuliko Mkude au wazawa wote Simba..? Labda inawezekana lakini kwa nini pesa ya wawekezaji ndani ya nchi hii isibaki kwa wazawa na familia zao. Ukimpa Deal Mkude umeokoa mitaa na umefikisha huduma kwa walengwa.
Napigania Heshima ya wazawa, napigania kipato kisitoke nje zaidi ya mishahara, moyo wangu unasinyaa nikiona Mitaa haipati mashavu kwa vipaji vya wazawa.
Wanaosimamia wachezaji changamkeni wazawa wapige fedha, wazawa wana vigezo, wazawa wanaijua mitaa na wakipiga deal mitaa inafurahi na wazazi kule uswahilini yanabadilika. Kupeleka pesa Lusaka au Burkina Faso ni kulidhulumu jasho la vijana wazawa.
Wageni wanapaswa kupigana kwa asilimia mia tano kupata deal hapa kwetu, ukiniuliza mimi nitakwambia UTAIFA mbele na siku zote nitasimama na vijana wa mitaa ninayoijua. Vijana wetu ni maarufu na baada ya soka watarudi kuitumikia mitaa hivyo ubalozi unakua wa milele.
VALUE HOME BOYS.
NB: Hongera Home Boys, Zimbwe Jr na Farid Musa, Lets Make it more and more.
Wadau mna maoni gani katika hili?