Achana na hamasa ya goli la mama ambalo Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kutoa Sh 10 milioni kwa kila bao litakalofungwa na Simba na Yanga katika robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mastaa wa timu hizo wakiwamo Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza, Stephane Aziz KI na Diarra Djigui wamepishana na mamilioni ya pesa walizoahidiwa kabla ya mechi za juzi usiku.
Timu hizo mbili zilitolewa robo fainali, Simba ikifungwa jumla ya mabao 3-0 na Al Ahly ya Misri, huku Yanga ikitolewa kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya kutoa suluhu nyumbani na ugenini mbele ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo iliingiza timu mbili robo fainali, lakini zote kwa bahati mbaya zimeaga, huku mastaa wa timu hizo wakiyakosa mamilioni waliyowekewa mezani iwapo wangevuka hapo salama kwenda nusu fainali.
Simba na Yanga zimekosa mamilioni ya pesa zile za Rais Samia ambazo aliahidi kutoa kwa kila goli na za hamasa kwa klabu ambazo ni jumla ya Sh 812 milioni.
Katika hatua ya makundi timu zote zilijikusanyia Sh 75 milioni, Simba ikiokota Sh 40 milioni baada ya kuifunga Wydad AC mabao 2-0 na Jwaneng Galaxy 6-0 huku Yanga ikiondoka na Sh 35 ikichapa CR Belouzdad mabao 4-0 na Medeama 3-0.
Mnyama Simba aliahidiwa kitita cha Sh 512 milioni na Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohamed Dewji 'Mo Dewji' kama itafuzu nusu fainali, huku Yanga ikiahidiwa Sh 300 na mdhamini wao, Ghalib Said 'GSM' milioni ukiachana na zile za wadau.
Hata hivyo, licha ya mastaa wa timu hizo kuyakosa mamilioni hayo, lakini kwa hatua ilizofikia Simba na Yanga kucheza robo imezifanya klabu hizo kila moja kuvuna kiasi cha Dola za Kimarekani 900,000 (zaidi ya Sh 2.3 bilioni )kutoka kwa wadhamini wa michuano hiyo inayoendeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).