Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chalobah aingia anga za Manchester United

Tottenham Hotspur Wanataka Kumsajili Beki Wa Chelsea Trevoh Chalobah Trevoh Chalobah

Sun, 28 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Manchester United imejitosa katika vita ya kuiwania saini ya beki wa Chelsea, Trevoh Chalobah katika dirisha hili.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka tovuti ya Football Transfer, Chalobah ambaye hakujumuishwa katika kikosi cha Chelsea kilichosafiri kwenda Marekani kwa ajili ya maandalizi ya msimu, hahitaji tena kubaki katika timu hiyo kwa kuwa hatopata nafasi ya kucheza.

Man United ambayo inasaka beki wa kulia, kwa sasa inaamini kumpata Chalobah itakuwa faida kubwa kwao kwani mbali ya uwezo wake wa kucheza eneo la beki wa kati pia anaweza kucheza kama beki wa kulia.

Beki huyu ambaye msimu uliopita aliandamwa sana na majeraha ya mara kwa mara yaliyosababisha asipate muda mwingi wa kucheza, mkataba wake unamalizika mwaka 2028.

Kwa mujibu wa watu wake wa karibu hata yeye amevutiwa na Manchester United na yupo tayari kujiunga nayo ikiwa watafikia mwafaka na Chelsea ambayo pia ipo tayari kumuuza.

BEKI kisiki wa Everton, Jarrad Branthwaite, 22, amewaambia mabosi wa timu hiyo kwamba anahitaji ofa ya mshahara utakaofikia Pauni 160,000 kwa wiki ambayo ameahidiwa na Man United ili kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia katika timu hiyo.

Branthwaite amekuwa akihusishwa na Man United tangu kuanza kwa dirisha hili lakini Everton haionekani kuwa tayari kumuuza na imeanza kufanya mpango wa kumuongeza mkataba.

MANCHESTER United inaangalia uwezekano wa kufanya mabadilishano ya wachezaji na Inter Milan ambapo inataka kumpeleka Aaron Wan-Bissaka kwenye timu hiyo kisha yenyewe iipate saini ya beki wa Inter Milan, Denzel Dumfries, 28, katika dirisha hili. Dumfries ambaye mkataba wake unaenda mwishoni, ili kumpata mbali ya kumtoa Bissaka, United pia inapaswa kutoa pesa kidogo.

MPANGO wa Brentford kutaka kumuuza straika, Ivan Toney katika dirisha hili unadaiwa kuingia mchanga baada ya Igor Thiago anayeonekana kama mbadala wake kupata majeraha yanayoweza kumweka nje kwa muda.

Staa huyu anawindwa na timu mbalimbali barani Ulaya ikiwa pamoja na Manchester United, Tottenham na West Ham.

ARSENAL imeanza mazungumzo na Paris St-Germain kwa ajili ya kumsajili kiungo wa timu hiyo, Fabian Ruiz, 28, katika dirisha hili lakini taarifa kutoka Football Transfer zinadai washika mitutu hao wanahitaji kuuza kwanza baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kabla ya kufanikisha dili hilo.

Ruiz ambaye mkataba wake unaisha 2027, msimu uliopita alicheza mechi 35 za michuano yote.

WEST Ham imewasilisha ofa ya Pauni 30 milioni pamoja na kiungo Lewis Orford kwenda Aston Villa ili kuipata saini ya straika wa timu hiyo na Colombia, Jhon Duran katika dirisha hili.

Lewis ambaye ni mmoja kati ya mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Villa, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.

MABOSI wa Juventus wamewaambia wawakilishi wa Liverpool kuwa ili kumpata beki wao Gleison Bremer, 27, watatakiwa kuwasilisha ofa isiyopungua Pauni 50 milioni. Staa huyu wa kimataifa wa Brazil anawindwa na Liverpool inayohitaji kuboresha eneo la ulinzi ambalo hadi sasa lipo katika hatihati ya kuondokewa na Trent Alexander Arnold na Virgil van Dijk.

PARIS St-Germain ipo katika hatua za mwisho kumsajili kiungo wa Benfica na Ureno, Joao Neves katika dirisha hili ambapo wameshafanya makubaliano binafsi na wawakilishi wa mchezaji na kilichobakia ni kuuvunja mkataba wake kupitia kipengele ambacho kinawataka kulipa Euro 120 milioni ili kufanikisha hilo. Neves 19, mkataba wake na Benfica unaisha 2028.

Chanzo: Mwanaspoti