Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chadrack Boka ni Mwananchi

Chadrack Boka Dfbs Chadrack Boka ni Mwananchi

Mon, 8 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu Yanga imethibitisha usajili wa mlinzi wa kushoto Chadrack Boka kutoka klabu ya Fc Lupopo ya DR Congo

Ilikuwa ni suala la muda kwa Yangaa kumtambulisha Boka aliyetua kuchukua nafasi ya Joyce Lomalisa.

Boka alikuwa mchezaji tegemeo katika kikosi cha Lupopo na pia amepata nafasi ya kuitumikia timu ya Taifa ya DR Congo katika michuano ya CHAN.

Unaweza kusema Yanga imetoa chuma upande wa kushoto na imeshusha chuma kwelikweli.

Boka mwenye umri wa miaka 24 anasifika kwa kasi ya kupandisha mashamulizi na umahiri katika ulinzi.

Anakuwa mchezaji wa tatu kutambulishwa katika dirisha hili baada ya Clatous Chama na Prince Dube.

TAARIFA YA YANGA;

"TUMEKAMILISHA usajili wa beki wa kushoto Chadrack Issaka Boka kutoka FC Saint Eloi Lupopo ya nchini DR Congo.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 24 ambaye ni mzaliwa wa Kinshasa nchini DR Congo, anakuja kuimarisha eneo la ulinzi upande wa kushoto akisaidiana na Nickson Clement Kibabage.

Ubora wa beki huyo hauna mashaka kutokana na kwamba ndani ya kikosi cha FC Saint Eloi Lupopo alikuwa panga pangua kikosi cha kwanza.

Nyota huyo pia amekuwa akiitumikia Timu ya Taifa ya DR Congo ambapo alijumuishwa kwenye kikosi kilichoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) iliyofanyika Algeria mwaka 2022.

Katika michuano hiyo ambayo DR Congo ilikuwa Kundi B, Boka alicheza mechi zote tatu hatua ya makundi dhidi ya mabingwa Senegal, Ivory Coast na Uganda.

Usajili wa Boka ni muendelezo wa kuimarisha kikosi chetu kuelekea msimu ujao wa 2024-2025 ambapo tuna malengo ya kutetea mataji yetu ya Ligi Kuu ya NBC na Kombe la Shirikisho la CRDB Bank.

Sambamba na hilo, tunahitaji kubeba Ngao ya Jamii na kufika mbali Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya msimu uliopita 2023-2024 kuishia hatua ya robo fainali.

Mpaka sasa, tayari tumesajili wachezaji wapya watatu ambao ni Kiungo Clatous Chama, mshambuliaji Prince Dube na beki wa kushoto Chadrack Boka.

Pia tumewaongezea mikataba Djigui Diarra, Aboutwalib Mshery, Nickson Kibabage na Bakari Nondo Mwamnyeto na Farid Mussa."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live